Hofu na mashaka yote, hutoweka kwa kushiriki Jumuiya |
Tumsifu Yesu Kristu na heri ya mwaka mpya. Ninakupa salamu za mwaka mpya kwakuwa tangu mwaka huu uanze sijaandika mada hata moja humu na hii ndiyo mada inayofungua mlango wa mada moto moto kwa mwaka 2017.
Tukiwa tunaendelea kumshukuru Mungu kwa uzima pamoja na changamoto kadha wa kadha ikiwemo uhaba wa mvua na mengineyo leo nataka nikupakulie kidogo juu ya mada muhimu sana inayokumbushia umuhimu wa jumuiya ndogo ndogo. hasa zinazoundwa na wanafunzi.
Katika miaka yangu minne nikisoma chuo kikuu SUA-Morogoro 2012-2016 nimeyaona na kujifunza yafuatayo kutoka katika jumuiya ya wanafunzi wakatoliki (Tanzania Movement of Catholic Students-TMCS)
- Jumuiya ndio mahali pekee unapoingia ukiwa mgonjwa na kutoka mzima. Ndio vijana tunaumwa sana tu sio kidogo. Tunaumwa mawazo yakumiliki vitu tusivyo na uwezo navyo, tunaumwa ulevi, tunaumwa fitina, tunaumwatamaa za mwili, tunaumwa wivu, tunaumwa kukosa huruma nakadharika. Katika kushiriki jumuiya utakutana na watu wenye vipawa vya kuhubiri, vipawa vya kushauri, vipawa vya kufariji ambao hao wote humfanya aliyehudhuria kutoka akiwa mtu mwingine kabisa huku akiwa na moyo uliotakata na matarajio mema yanayoshikika.
- Jumuiya ndio mahali pekee ambapo utatua mizigo yako ya msongo wa mawazo. Chuo/Shule ni ngumu sana (huenda ilikuwa hivyo kwangu pekee) kiasi kwamba kuna wakati unatamani kumuazima mwenzako kichwa chako ili upumzike kidogo kuwaza. Unaweza kuamka asubuhi na kugundua hujamaliza kazi inayotakiwa kukusanywa leo, wakati huo huo kesho kuna test na inabidi ufanye marudio ya notes nyingi sana, kama hiyo haitoshi leo siku nzima kuna vipindi, (saa moja asubuhi hadi saa moja na nusu usiku) na ni masomo ambayo ukikosa kipindi kimoja basi huko mbele ya safari utaona vumbi tu, Kwa njia hii inafika jioni umejaa msongo wa mawazo, hapo bado hujapigiwa simu nyumbani huko kuna matatizo nakadharika. Ukienda kusali na wenzako katika jumuiya lazima utaokota kitu hata kimoja cha kukufaa. Mungu ana watu wake wataalamu wa ucheshi na kukufanya ufurahi huku ukibarikiwa kwa sala za jioni, nyimbo na tafakari ya neno la Mungu. Nkuhakikishia ukiondoka hapo na kwenda kushika madaftari yako unakuwa na nguvu mpya (you gain new momentum). Iwe kwenda kusoma kwenye kundi au peke yako, utaona kuna wepesi wa hali ya juu baada ya kutoka sala.
Tukifurahi na kuimba kwenye jumuiya. Baada ya hapo vichwa vyetu viko safi kuyakabili masomo. Kuna wepei fulani Mungu anajaza ndani yetu. |
- Jumuiya ndio kituo cha afya ambako chanjo dhidi ya magonjwa sugu ya uchonganishi, majivuno, wizi , dhambi zote na vilema vyake hutolewa. Ni kweli kwamba kuhudhuria jumuiya huku ukiendelea kufanya mambo mabaya haina maana. Lakini ni ukweli wa mchana kwamba mtu anayeshiriki jumuiya anaenda kukutana na neno la Mungu ambalo ni moto wa kuteketeza dhambi na vilema vyake. Mahubiri yanachoma na kufukunyua ndani ya uvungu wa moyo wa kila asikiaye hasa linapozungumzwa jambo ambalo ni kilema chako. Kama kweli dhamiri yako ipo hai, utaumia moyoni, utafanya kitubio na kuweka mikakati ya kuto kukosea tena. Hii ni chanjo kwa waliokuwa hawajafanya kosa fulani na ni dawa kwa aliyekuwa tayari muhanga wa kilema hicho.
- Jumuiya ndipo mahali pekee ambapo unakwenda kupata walezi watakaokubeba ukipata changamoto nzito isiyobebeka na marafiki wengine. Natambua kila mtu ana rafiki au marafiki anaowaita wakushibana, lakini kuna wakati betri zinaweza kugeukiana, umeme unazima kila kona, ndipo utajua kuwa ni wakushibana au wa kunjaana. Kwa mtu ambaye anashiriki na wenzake kusali katika jumuiya, anatengeneza mtandao wa watu sahihi ambao watatumia mbinu zote kuhakikisha anapata msaada. Nikiwa chuoni nimeona wanafunzi wakipata matatizo makubwa ambayo hata wazazi hawawezi kutatua kwa haraka, lakini jumuiya imekuwa ikijitoa binafsi au kushirikisha wanajumuiya na kutoa msaada wa haraka kwa njia ya huduma na ufariji.
- Jumuiya ndipo mahali wanakopikwa wazazi bora, wachakarikaji, wapambanaji na watakaowajibika katika familia zao . Hakika hili halihitaji ubishi. Matharani katika jumuiya kumekuwa na semina za WAWATA, mafungo, huduma katika vituo vya watoto yatima, wazee na wasiojiweza na mengi ynayofanana na hayo. Hii ni tabia njema na ishara ya kujiandaa kuyabeba majukumu ya familia na jamii ambayo inatarajia makubwa sana kutoka kwako. Mambo mengi sana hata mimi binafsi niliyachukua moja kwa moja na yanatakiwa kufanyiwa utekelezaji bila ubishi kama kweli nataka kuwa baba bora wa familia. Mzazi asiye na huruma kwa wahitaji, kuwafundisha watoto kujitoa, kufariji, tabia njema na matendo ya huruma huyo sio mkristu, bali ni wakala wa shetani. Labda unaweza kusema mbona wapo wakristu ambao bado wanatabia chafu na malezi ya vumbi kwa familia zao? Ngugu yangu hayo ni mapungufu ya mtu binafsi kutokana na malezi yaliyomkuza na watu wanaomzunguka, lakini sio ishara ya Ukristo.
- Jumuiya ni mahali pa kukata kiu ya mafundisho ya kikristu na kukufanya uwe mwalimu hodari wa familia na jamii. Hebu tafakari zile misa za katikati ya juma, novena za Roho Mtakatifu, novena kwa Mt Rita wa Kashia, semina za wanajumuiya, mapadre, watawa, yale mafungo ya Fransalian mara mbili kila muhula (kwa wanafunzi wa SUA), Joint Prayers, hija kwa kila mwaka wa masomo, jamani Mungu akupe nini mkristu wewe mwanafunzi? Hii kwangu ni chakula bora tena mlo kamili. Tatizo ni uvivu tu wakupuuza haya mambo na kujifanya tumetingwa na mambo mengine (busy) kumbe tunajikosesha mambo muhimu kwa roho zetu amnbayo ni chakula cha roho zetu hivyo unakufa kwa utapiamlo huku chakula bora kipo mezani, na kimeandaliwa na mama yako mzazi ambaye ni mpishi hodari mwenye viwango vya aina yake.
Mungu anajidhihirisha kwa watu kupitia upendo wa jumuiya, chamsingi usimuumize mtu au usitende dhambi. |
Baada ya masomo, tafakari ya neno la Mungu tunapata nafasi ya kushiriki matukio ya kupongezana na ucheshi kama jumuiya. Tukitoka hapo mambo yanaingia vizuri kichwani |
Kutembelea vituo vya wahitaji ni kujifunza malezi katika jumuiya. Shiriki na wenzako. (Mgolole sister's orphanage centre, Mehayo centre, Fungafunga, Amani centre etc ) |
- Jumuiya ni mahali pa kutengeneza mtandao mkubwa wa mawasiliano ya kijamii, kibiashara ndani na nje ya nchi. Katika kusali kwenye jumuiya watu wamepata watu waliowapa taarifa za kibiashara maeneo mbali mbali, wengine wameunda umoja na kufanya uzalishaji wa pamoja, wengine wameoana (iwe kwa makusudi ya Mungu na sio kulazimisha). Kila mkoa utakaoenda unajikuta kuna mtu anakufahamu kwasababu mlikuwa mnasali pamoja. Kwa hili hata mimi ni shahidi, nimepata mambo mengi sana kupitia ndugu zangu katika Kristu ambao nilikutana nao katika kusali jumuiya. Uitegemee kmengine yote ya jumuiya kana kwamba wewe ndio mmiliki wa chombo hiki (Active participation).
Mungu akutie nguvu, neema na baraka zake zisikupungukie, na uwe na wakati mwema. Karibu kwenye mtiririko wa mada motomoto kwa mwaka huu mpya 2017, usisitete kuuliza chochote au kuchangia kwa comment, email au simu. Tumsifu Yesu Kristu
'JUMUIYA NDOGONDOGO ZA KIKRISTU, ROHO MOJA, MOYO MMOJA KATIKA KRISTU!
Eng Nguki Herman. M