I am targeted to change youth's mind set towards positivity.

I am targeted to change youth's mind set towards positivity.
I am targeted to change youth's mind set towards positivity

Friday 17 February 2017

HOMILIA HAITOSHI.

Ee Mungu tupe shauku ya kujifunza neno lako, ndilo taa ya miguu yetu.

Tumsifu Yesu Kristu. Shairi hili ni sehemu ya mahubiri na mafundisho yangu ya kila siku ambalo kwa neema ya Mungu lilichapishwa katika gazeti letu la kanisa Katoliki , gazeti la Kiongozi kwa matoleo mawili mfululizo yani toleo la  tarehe  8-14/5/2015   na toleo la   15-21/5/2015 .  Kama hukupata nafasi ya kupata nakala ya gazeti lile na kusoma basi ni wakati wako sasa kupata ujumbe uleule. Lipo pia shairi langu lililochapishwa katika gazeti la kimisionari la Enendeni ambalo hutolewa na Wamisionari wa Consolata , lakini maudhui yake yamepita (yalijikita kukemea tukio la muda mfupi) hivyo sitaliweka humu.

HOMILIA HAITOSHI, CHIMBA ZAIDI IMANI


01
Tumsifu Yesu Kristo, Enyi watoto wa Mungu,
Nawaletea kijito, cha umande na ukungu,
Sifanye moyo mzito, kukionja hiki chungu,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

02
 Marakadha husikia, Wakatoliki wavivu,
 Kitaka kufatilia, ni kauli ya kichovu,
 Kanisa lataka jua, liwalisheni kwa nguvu?
 Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

03
Kama hujanielewa, namaanisha usome,
Vitabu kede twapewa, kwanini usijitume?
Kama hautaki sawa, mimi ninakupa shime,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

04
Amigu na Kamugisha, na wengine waandishi,
 Vitabu vingi kutosha, kuvisoma ni mbishi,
 Ujue unachekesha, nafsiyo hushibishi,
 Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

05
Huenda hauna pesa, semina wahudhuria?
Muumba umemsusa, wadhani achekelea?
Baraka unazikosa, na kwake hutaingia,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

06
Misa unahudhuria, sawa hiyo njema sana,
Vipi kwenye jumuia, mbona unakwepa bwana?
 Hebu acha kusinzia, uyasahau ya jana,
 Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.
07
Katekisimu wajua, mafundisho imejaa,
 Ukurasa kifungua, hutaacha kurudia,
 Changanya na biblia, roho itashiba pia,
  Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

08
Imani sio kikombe, Useme umeoteshwa,
Ni wamuumba ujumbe, nafsiyo kushibishwa,
Hivyo lazima uchimbe, pasipo kubabaishwa,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

09
Huenda nakuchefua, Tulia utaelewa,
Lengo hapa ni kukua, Imani kuielewa,
Sasa ukinishushua, utashindwa kutambua,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

10
Muda wa kazi unao, sawa wataka riziki,
Basi acha singizio, sala haziepukiki,
Nong’oneza jiranio, Shetani mtoe nduki,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

11
Wajua watakatifu, Yasome maisha yao,
Tena haitakukifu, watakuombea hao,
Uchambuzi akinifu, Utakupandisha huo,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

12
Theresia dada yangu, Angelina mama pia,
Na wote rafiki zangu, mimi nawakumbushia,
Upendo tu ndio rungu, shetani mkung’utia
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

13
Huyu atajiuliza, kwani kusali lazima?
Namimi nakuuliza, Ni wamhimu uzima?
Hapo ukijiongeza, jibu unalitazama,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

14
Imani sio pambio, la kujua siku moja,
Tena si ya kivamio, Eti ni mtu wa hoja,
Machweo hata mawio, nidhamu  ndonambamoja,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

15
Kwaleta afya kusali, pole kama hutambui,
Novena na taamuli, hapo ndio silegei,
Fikara pia Rozali, ni Zaidi ya mayai.
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

16
Mimi ninakukumbusha, Tena mimi sio kitu,
Ukiona nakuchosha, ndo udhaifu wa mtu,
Jitahidi hakikisha, kusali unathubutu,,
Homilia haitoshi,Chimba Zaidi imani.

17
Kanisa letu tajiri, kwa vipawa vya kutosha,
Walimu na wahubiri, hima watuhamasisha,
Ila tu ni ujeuri, tamaa watukatisha,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

18
Nguki naishia hapa, kazi kwako kuyashika,
Sidhani ‘metoka kapa,  kwa machache niloshuka,
Kusali acha kukwepa, Baraka zipate shuka,
HOMILIA HAITOSHI,CHIMBA ZAIDI IMANI.
 Namini umepata chochote kwa kupitia shairi hili. Ubarikiwe sana.
Eng Nguki Herman
0763 639 101/0679 639 101
Email: ngukiherman@ymail.com
Thank you for visiting my blog. Click ‘ view the web version’  to see other topics OR SEE THE  LIST ON THE FOOTER BLOCK which have been categorized by months posted.  You are welcome also for Professional information about Agriculture, water resources, soil and environmental conservation visit www.wadcotanzania.blogspot.com  .Eng Nguki