Kama maandishi hayasomeki kwa mobile version, shusha mwishoni utakuta "View web version" click hapo. |
Natambua fika hatari ya kujamiiana
kabla ya ndoa na matokeo yake. Moja wapo ni mimba, na ikumbukwe hapa tatizo sio
mimba bali ni mfumo wa kuipata/kusababisha na uwezo wa kuhudumia mimba yenyewe
na mtoto atakayezaliwa. Hili nalitambua vizuri sana na nimekuwa nikiliongea na
kuliandika kila uchwao, sio kwa kuhukumu hapana, hii ni kwasababu kuzaliwa
ndani ya ndoa au nje ya ndoa hakufanyi azaliwe kiumbe tofauti, japo kuna hatari
ya myumbo katika malezi na kumkosesha mtoto baadhi ya haki fulani za msingi au
kukosa uhuru.
Katika hali isiyo ya kawaida
nilijikuta nimempata msichana fulani na kufanya naye ngono, na kumpa mimba siku
hiyo hiyo. Mimi sikutambua kuwa nimempa mimba na yeye alisema kuwa hawezi
kupata mimba. Basi baada ya muda fulani wazazi wake waliniita na kuniambia
nimempa mimba mtoto wao na wanachotaka ni ndoa kabla mtoto hajazaliwa kwa maana
hawataki mjukuu wa nje ya ndoa. Na ikiwezekana nimuoe ndani ya wiki moja.
Mungu wangu weee, presha ilinipanda,
viungo vyote viliishiwa nguvu, nikawaza na kuwazua nitaishije na kumlea huyu
binti, tena sina kazi na akaunti yangu benki inapumulia mashine hata elfu kumi
hakuna. Nikawaza juu ya makazi na kugundua nina chumba kimoja tu nacho wanakaa
wadogo zangu wawili wanaosoma tena ninawahudumia mimi mwenyewe na hawana sehemu
ya kwenda. Rafiki yangu mmoja akaniambia ‘Nguki hapa komaa tu mzee
baba, ndani ya wiki hii oa tu’.
Ukweli nilikuwa na hamu sana ya kuitwa
baba, eh, niwe na mtoto. Lakini sasa njia niliyotumia ndiyo inayonipa majuto.
Nikawa nawaza juu ya rafiki zangu na watu wa karibu, wataelewaje kuona ndoa
imeibuka kama uyoga hakuna cha kuvalishana pete wala send off wala nini? Huku
wazazi wa yule binti ndio kwanza hawataki kusikia chochote. Basi nikajikaza
kisabuni hadi kwa baba yangu mlezi, akasema ‘hiyo changamoto umeizalisha
mwenyewe na hakuna kukwepa. Mimi nitakuongezea hela kidogo kwaajili ya hizo
harakati zako, kama utaongezea kwenye harusi sawa, kama ni kwemnye maisha
utajua mwenyewe’
Kichwa kiliniuma sana, hadi nikahisi
yule msichana ananidanganya. Nikampigia simu ili aje niliangalie tumbo vizuri
kama linaonekana kuongezeka ukubwa. Alikuja na kunikuta nipo na rafiki zangu
nimejiinamia kwa mawazo. Akafika pale akiwa ameniletea na mikate,
nikamuaangalia kichovu na kumuuliza kama yuko serious kweli nilimpa mimba kwa tendo
lile moja au ananipima tu akilia, akanisogelea kwa karibu, mamamamamamama
weeeeeee, katumbo kamejaa mwanawane, yani hakuna ubishi. Akanishika kichwa
changul kwa tabasamu na kuniambia kingereza ‘Nguki, do you think I am
lying to you? This pregnancy is yours’. (Akiwa na maana nisidhani
anadanganya, hiyo mimba ni yangu). Aliongea kwa kujiamini, bila wasiwasi huku
akinishika kidevu changu kilichokauka kama mti mkavu kwa presha tangu nizipate
hizi habari.
Kwakweli sijawahi pata maumivu ya
kichwa na mawazo makali kama haya, nilitazama juu na kuona kama Mungu kaniacha,
jeuri yangu ya kuwashauri vijana wenzangu ikayeyuka ghafla, nikiangalia wazazi
wangu hawana uwezo wa kujitwisha hii changamoto. Nikajiuliza, nini kinafuata
bado sikupata jibu. Nilijikuta nalowa jasho mchana na usiku sipati cha kufanya
na wiki moja niliyopewa na wazazi wake yule binti niliye mtumbilize ndio
hiyoooo inaisha.
Rafiki yangu akaniambia niende kwa
wazazi wa yule binti kuwaambia nimeshindwa kutekeleza masharti yao na kama kuna
lolote wanataka kufanya juu yangu kwakweli wafanye tu, maana sioni cha kufanya
juu wala chini, zaidi najikuta nakonda tu ndani ya wiki moja. Basi yule jamaa
yangu akanipakia kwenye pikipiki yake, haooooo hadi nyumbani kwa wazazi wa yule
binti..
Tulimkuta mama yake akiwa nje,
alipotuona tu, akamuita mumewe aliyekuwa ndani. La haulaaaaa, yule mzee
alipotoka alinikata jicho hilo kwa muda katika tano bila kuongea chochote! Ohh
Mungu wangu weeee, hofu ikanitanda, huku navuja jasho nikadondoka chini kama
fulushi puuuuuu!, Wakati nahangaika kusimama kwa kuishika mikono ya yule
rafiki yangu, nikagundua nimeshikilia neti na nilikuwa nimezinduka kutoka
kwenye ndoto yangu! Loooh, nilikuwa navuja jasho, nikainuka na kukaa,
nikajikuta natamka kwa nguvu ‘Mungu, nini lakini jamani’. Asikwambie mtu,
sijawahi ota ndoto yenye kashkash kama hii ya usiku wa kuamkia 25/11/2017.
Nilipoamka nikawa nawaza hivi hizi
presha ni katika ndoto, je ingekuwa live?
Narudia tatizo sio mimba bali mfumo.
Aisee hizi presha sizitaki kabisaa,hii ni ndoto lakini imenipa picha nzima ya
hali ambayo nitakutana nayo endapo nitajitoa ufahamu. Nakushauri na wewe kijana
mwenzangu amini katika subira na jiwekee tu malengo, haya yote uyafaidi ndani
ya ndoa. Narudia tena hapa hatunyoosheani vidole au kuhukumu, hapana, bali kama
umewahi kukosea, basi fanya ukarabati mkubwa (Major rehabilitation) wa nafsi
ili usikosee tena na kujiwekea nafasi nzuri ya kuwa mlezi bora wa
familia.KUSUBIRI INAWEZEKANA, ANZA SASA.
Katika kujifunza pia nakukaribisha
uniunge mkono kwa kununua kitabu nilichokiandika (DHAMIRI NA UTASHI
VIMETEKWA) ambacho ndani nimeeleza mambo mengi yahusuyo mahusiano,
upendo, subira, kuweka malengo, na malezi. Nimekielekeza kwa vijana, lakini pia
wazazi na walezi kitawafaa sana ili kuongea na watoto/vijana wao. Ili kukipata
waweza nitafuta kwa namba zangu hapo chini. Lakini pia
kinapatikana Dar es Salaam (Doloka Investment Company Ltd Millenium
Towers Makumbusho-0655 266 993 na Pia Kijichi-0686 971 623), Morogoro
kinapatikana chuoni Sua (nipigie nikuunganishe na wanaokiuza), Kinapatikana pia
Fransalian Bookshop-Kola Morogoro na Iringa ofisi za UCE Tanzania,
Kihesa-Kichangani.Karibu sana ujifunze.
Eng Nguki Herman. M