I am targeted to change youth's mind set towards positivity.

I am targeted to change youth's mind set towards positivity.
I am targeted to change youth's mind set towards positivity

Saturday, 19 May 2018

Comments zinavyoweza kuvunja mahusiano/ ndoa

Mungu ndio anajua siri ya wapendanao


Rafiki yako akipost picha katika mitandao ya kijamii, kabla ya kuwaza kusema chochote kuihusu (ku-comment) huwa unachukua hata dakika moja kuwaza madhara yatakayotokana na comment yako? Au huwa unatiririka tu kuandika, tafakari itafuata badaye? Mara ngapi umeshuhudia comment ya mtu kwenye post ya mtu mwingine imezua varangati na majibizano yanayoashiria mmoja kaumizwa nafsi?
Nitajikita sana kwenye matukio ambayo ni ya kawaida kwa mapito ya mwanadamu kulingana na mazigira aliyopitia na watu aliokutana nao (exposure). Mara kadhaa nimekua nikisema kuwa mambo tunayofanya hayafutiki mioyoni mwa watu, ndio yanakaa na kuhifadhiwa. Na ndio maana kama ulikuwa na tabia fulani nzuri au mbaya wakati unasoma, basi hata kama baada ya miaka ishirini, wale uliosoma nao wanaweza wakawa wanawasimulia watu wengine ile tabia yako kwa maana wanaikumbuka! Ndio maana vijana tunatakiwa kuwa makini sana na kila tunachokifanya ili watoto wetu wakija kusimuliwa tusiumie mioyo au wakaona kumbe baba/mama yao alikuwa hamnazo.

Inakuwaje hii?
Inakuwa hivi: Unakuta Mkaka/mdada kapost picha yake mtandaoni anavalisha/anavalishwa pete ya uchumba (engagement) au amefunga ndoa safi kabisa. Ndio amefunga ndoa Mungu kambariki na kufikia hapo. Sasa mtu mwingine labda kasoma naye sekondari huko anakuja na kuona ile picha, na anakumbuka tabia za yule mdada/mkaka kuwa labda zilikuwa mbaya, au alikuwa na mahusiano motomoto na mkaka/mdada mwingine ambaye sio huyu aliyefunga naye ndoa! Bila hata kufikiria mara mbili unakuta anadondosha comment kama hii hapa:

v  Heh! Jamani mbona huyu sio yule shemela XY mliyekuwa naye shule jomoni? Mm we mdada/mkaka mhuni jamani, kha! Mlivyokuwa mnapendana vile kumbe ni uzushi tu? Hongera lakini.

v  Wacha weee, kumbe XY ulimpiga chini, koh,koh,koh simpatii picha povu lake akiona jamaa mwingine kakubeba.

v  Wapi XY?? Nani kamasaliti mwenzake?

v  Mhhhh, sitaki kuamini, yani XY alikuwa anakuhudumia hadi ukiugua, kumbe ilikuwa drama tu?
v  Hivi huyu ni XY kweli? Au macho yangu yananidanganya? Teh,the,teh

v  Duuuhhh kweli mapenzi ni kizungumkuti, kumbe XY mlikuwa mnachezeana tu, hongera lakini mwaya.

v  Heh, jomoni, wewe si ulitutambulisha XY kuwa ndio shemela mtarajiwa? Mliishia wapi tena? Hihihiiiii

v  Mwingine anaamua kuchukua hiyo picha na kupost kwenye ukurasa wake au kwenye magrupu ambako wewe huna uwezo wa kufuta comments wala kuona ili wakujadili vizuri. Tena anasindikiza na vi-emoji vya kinafikiii!!

Ukiangalia kwa makini hizo comments zinaonnesha huyu mtu anamfahamu vizuri mhusika na mapito yake. Na ukweli ni kwamba comment yake ipo sahihi kabisa!! Lakini je, unajua madhara yake kwa mhusika?
Mahusiano yana siri kubwa. Usiwavuruge waliopiga hatua chanya


Sikiliza kwa makini! Kila binadamu ana mapito yake aliyopitia, napengine aliingia kwenye mahusiano kwa sababu ya ujinga, shinikizo, kuiga , kujaribu au kwa nia njema lakini humo njiani akakuta mambo siyo yenyewe na kubadili gia angani. Ni kweli msichana au mvulana huyo alikuwa hivyo sekondari au chuo, lakini je, unajua yaliyomkuta? Wakati tunaongea na vijana huwa mara zote tunasisistiza kugeuka iwapo wapo kwenye mahusiano yasiyo na tija (Second chance). Hii inamaana kama ulijipachika mahala na ukagundua ulikurupuka au mambo tu huyaeleweki, basi jitoe ili upate nafasi ya kukua zaidi na kufanya uchaguzi mwingine.

Kuna mtu anasema;  ‘weeeee, maumivu yake ni hatareee!!!’ Ndio, kuna maumivu makubwa sana, utalia, utaapiza, utatoa matamshi ya laana, utajiona mjinga, hufai na mengine mengi, na kubwa zaidi unaumizwa na maswali ya waliokuwa wanajua mko pamoja! Lakini hayo yote ni mapito tu, chukua hatua, utapona na kuendelea kusonga mbele! Ukiona hauna amani, unaenda tu kama unamsindikiza mtu, na matarajio yako huyaoni au yule uliye naye analalamika kuwa matarajio yake hayaoni na mnasukumwa na huruma tu, chondechonde (kama maridhiano yamegonga mwamba) vunjeni huo uhusiano kabla hamjafika mbali kwa maana mnatengeneza bomu la kuja kusalitiana badaye. Haijalishi wangapi wanajua, sio marafiki, unaosali nao, wazazi wako, umempost sana mitandaoni nakadharika, HAO WOTE HAWATAKUJA KUISHI NA NYIE, NI WAPAMBE TU, LAKINI CHUMBANI MTAJIFUNGIA WAWILI PEKE YENU NA MUNGU WENU!

Acha akili za kijinga kucomment negative side ya mtu ambaye kapiga hatua. Ulitaka umuoe wewe? Au ulitaka akuoe wewe? Au ulikuwa unampenda akakugomea? Ameshavalishwa pete sasa! Unasemaje? Ndio ameshaoa/olewa, unatakaje? Unaandika maneno yanaingiza ndoa ya watu migogoro, mtoto wa watu anapata kazi ya kujielezaaaa kwa mume wake kisa nyau tu mmoja umekurupuka huko. Ulilazimishwa U-comment?? Wao wanajua walielezanaje mapito yao ya nyuma, na wamekubali kubebeana mizigo. Uliacha kumsema kipindi kile kapotea, sahizi kabadilika ndio unaleta maneno yako kwa reference ya mambo ya nyuma! Stop it please! Waache waoane, waache waoaneeeee!!
Ndoa na iheshimiwe na watu wote. Mambo waliyopitia kila mmoja huko nyuma hayakuhusu wewe mwingine (Third party)


Kitu cha msingi ukiwa kwenye mahusiano ni kuepuka kufanya ngono! Hii itakupunguzia maumivu siku ukiona mahusiano hayana tija na unaamua kuyavunja. ‘Nyanyachungu and 12 others reacted to your photo’, Heh, sawa tu endelea ku-react but wenzako wameshapanda madhabahuni na wanaazisha familia!! Sio lazima u-comment, unaweza kupita tu na kuacha kuwaza. Mwingine wanaonana kwenye daladala anaanza kumhoji, Oh fulani vipi, XY yuko wapi, Siamini kama hamkuoana naye, ilikuwaje , ooo,, iiii , kwikwiiii, Heh! Kazi ipo.

Kama unataka kujua yaliyowakuta, mitandao yooote ina inbox. Nenda huko inbox kamuulize nini kilitokea kwenye mahusiano yao, hata hivyo sio lazima akuambie kwa maana wewe sio stakeholder wa maisha yake. Na sio kukurupuka ku-comment maneno yatakayozua mzozo kati yake na mwenzi wake. Na bahati mbaya zaidi siku hizi unakuta karibu familia nzima ipo mtandaoni (pande zote mbili). Wazazi, wakwe, mashemeji, mawifi wote wapo huko. Sasa wewe unaleta comment kwenye post ya uchumba au ndoa ya mtu kutoa kashfa na ndugu wa upande wa pili wanaona, hapo lazima utaanzisha mjadala huko kwamba mtoto wetu kaoa/olewa na mtu asiyefaa na kuna uwezekano mkubwa wa ndoa kuingia shubiri kuanzia mwanzo kabisa!!

MWANAMKE: Furaha yako, amani ni zaidi ya mtu! Hivyo usiyumbishwe au kutishwa na mtu kwa maamuzi uliyofanya na umejiridhisha kuwa yana tija.
MWANAMME:Ujasiri wako na amani yako ni muhimu kuliko mtu. Ikiwa unaona matarajio ya binti wa watu huyafikii na unaishia kumtesa tu kwa mawazo ni bora umuache ili akajitafutie mtu ambaye atampa amani.
Ikumbukwe pesa, elimu au kazi ya mtu haina mchango mkubwa kwenye upendo, bali ni amani uliyonayo kuwa na mtu na matarajio ya hatua chanya mtakazopiga kwa pamoja.
Hata hivyo haya ni mawazo  yangu tu, sio lazima yafanane na ya kwako! Kwa moyo mkunjufu nikutakie tafakari njema.

Eng Nguki Herman. M

Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman

Asante kwa kusoma katika blog hii.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com



Friday, 5 January 2018

Heh! Kumbe Wavaa Hirizi Bado Wapo?

Kwa dunia ya sasa kubadili fikira zetu ni lazima sio ombi!
Habari. Namshukuru Mungu pamoja nawe kwa kutuwezesha kufika mwaka mpya wa 2018, hakika ni neema ya upendeleo kabisa kutoka kwa Mungu wetu. Na sio jambo la kulichukulia kawaida hata kidogo, bali litutafakarishe na kutufanya tuishi  vyema kwa busara na mipango akinifu.
Sasa tuje kwenye mada yetu ya kufungulia mwaka!. Kwa kipindi kirefu nimekuwa nikisikia tu neno hirizi na kwamba kuna watu wanavaa kama kinga kwa imani za kishirikina, wakiamini kuwa zinawakinga au kuwalinda dhidi ya  maadui wanaotaka kuwadhuru. Nilipoendelea kudodosa, nikasikia hizo hirizi watumiaji huwa wanavaa kwa kificho maeneo ambayo sio rahisi kuonekana kama viunoni nakadhalika.

Kwa bahati mbaya huwa sijichoshi sana kufuatilia kama nikiona jambo halina tija au haliwezi kuniathiri kwa namna yoyote (labda iwe ni kwaajili ya kuwatahadharisha wengine au kujifunza). Sasa juzijuzi hapa nikiwa ugenini mkoa fulani, kunarafiki yangu  mmoja tulikuwa tunafanya naye kazi akawa ananisimulia juu ya mdada mmoja ambaye ametokea kumpenda, na mdada mwenyewe kaanza kuonesha ukaribu japo bado hajamwambia. Kwakweli alinisimulia jinsi huyo mdada alivyo mzuri na ambavyo akimsogelea tu network inakata na anasahau kila kitu na kumuwaza yule mdada; hahahaaa

Akaniambia niende mtaa anakokaa (rafiki yangu) ili nimuone huyo mdada kwa maana akitoka kazini huwa wanapiga stori na ni nyumba jirani, nikamkubalia. Basi nikaenda kama tulivyokubaliana, na nilimkuta yule mdada hapo. Ki ukweli hana tatizo, ni mzuri wa sura na ni haki yake yule jamaa kuchanganyikiwa. Yule dada alivaa gauni la mikono ya kukatwa (nakosa jina zuri, lakini naamini umenielewa), wakati namuangalia vizuri nikaona kwenye mkono wake wa kushoto katikati ya kiwiko na bega amejifunga kamba nyeusi kama rangi ya kaniki zile za zamani na inakitu fulani kimefungwa. Mhhhhh,

Nikamuliza mtu fulani alikuwa karibu kuwa kile ni nini alichojifunga yule mdada? Akajibu ‘HIRIZI’, ati nini??? Mbona nilisikia wavaaji huwa wanaficha? Imekuwaje huyu ana ujasiri wa kuvaa hadharani na tena ni binti mdogo kabisa, anaoneka mjuaji wa vitu vingi, na muonekano wa kimjini-mjini. Duh, niliishiwa pozi aisee.
Ujue kuna vitu vingine kuvielewa kuwa huo ni ujinga na ni utumwa kifikra sio lazima uwe mtu wa kanisani au msikitini. Kwa elimu na utandawazi ulipofikia sasa kubadili mmfumo wa kufikiria sio ombi tena bali ni lazima. Sasa inapotokea kuna mtu tena kijana anaamini juu ya kuvalishwa hirizi leo hii eti awe salama? Mwisho  wa siku unakuwa mtu wa kujihami na kutuletea shida tu kwenye jamii yetu.
Jamii ya kishirikina ni jamii 'sindikizaji'. Haitafanya maendeleo kamwe!!

 Ikitokea malaria imekushika ghafla unaanza kuwaza labda anakuchezea mtu mwenye hirizi kubwa kuliko yako. Ikitokea umepata ajari, watu wanakuja kukuokoa wanakuta umejifunga hirizi lako, nao watahusisha ajari hiyo na ushirikina. Ikitokea Mungu kakuita ghafla ndio kabisaaaa, ndugu waliobaki wanaaanza kutafuta mchawi utadhani wao wataishi milele. Dunia ya leo kuwa na imani za mfumo huo ni mzigo na nikujitengenezea mabalaa na kurithisha watoto na wajukuu ujinga. Nasema hili kwa maana hata huyu binti niliyemuona mimi mwenyewe najua fika haya atakuwa amejifunza kwa wazazi wake tangu utoto na hapa tayari amekomaa na imani hiyo, hivyo ukijichanganya tu na kumuoa wakati kafungamana na hayo madudu yao lazima watatafuta mbinu kuyaapenyeza kwa watoto wenu ili urithi uendelee kwa maana watoto watakuwa wanaenda kumtembelea bibi mzaa mama yao. Mama weeeeeee, !!!!

Wakati tunataka kuanzisha mahusiano yenye tija, kama vijana, tusijisahau na kuangalia uzuri wa sura pekee au elimu. Kipengere cha mila na desturi pia tamaduni zao huyo mwenzako jitahidi uzifahamu. Inaweza isiwe rahisi sana kutokana na baadhi yao kuficha na utakuja kustukia madhara, lakini tumuombe tu Mungu atusaidie katika kipengere hicho ili ukigundua usipoteze muda wako na kujikuta anakuja na begi ukidhani ni nguo kumbe ni mihirizi ambayo haimsaidii chochote zaidi ya kumpa presha tu kisaikolojia. Na ndio maana kuna mtu fulani aliniambia kwamba mtu ambaye ana amini katika hirizi, ikitokea siku hajavaa au imepotea katika mazingira yasiyoeleweka, mhusika ataugua hoiiiii napengine kufa kabisa. Sio kwasababu hajavaa, bali kwasababu anaamini hayuko salama.


Hebu huu mwaka 2018 uwe mwaka wa mabadiliko kwa wenye imani za ajabu na zisizo na tija kama hizi. Inasikitisha sana na wakati fulani inachekesha. Tumuombe Mungu kwa imani zetu atusaidie kutuongezea uelewa kuwa hatuwezi kukimbizana katika safari ya  maendeleo na uzalishaji mali kama bado mawazo na fikira zetu zipo kwenye imani za kishirikina. Natafuta mbinu za kuongea na yule mdada ili nimuulize mimi mwenyewe kuwa ‘kile ni kinini na kwanini kakivaa’ huenda ni ki-kuku cha kiasili, hahahaaaa. Akiijibu nitakuja ku-edit hii mada yangu. Sikubali nataka kupata majibu kutoka kwenye kinywa chake!!! Sasa kali ya mwaka mpya ni kwamba yule rafiki yangu hajawahi kujisumbua kuumiza kichwa kuliwaza lile lihirizi la yule mdada japo lipo waziwazi na kila siku linaonekana,yeye kapoteana na sura tu ya yule mdada hahahaaaaaaa, Khaaa!! Hatari sana.

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Asante kwa kusoma katika blog hii.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com