Kwa dunia ya sasa kubadili fikira zetu ni lazima sio ombi! |
Habari. Namshukuru Mungu pamoja nawe kwa kutuwezesha kufika
mwaka mpya wa 2018, hakika ni neema ya upendeleo kabisa kutoka kwa Mungu wetu.
Na sio jambo la kulichukulia kawaida hata kidogo, bali litutafakarishe na kutufanya
tuishi vyema kwa busara na mipango
akinifu.
Sasa tuje kwenye mada yetu ya kufungulia mwaka!. Kwa kipindi
kirefu nimekuwa nikisikia tu neno hirizi na kwamba kuna watu wanavaa kama kinga
kwa imani za kishirikina, wakiamini kuwa zinawakinga au kuwalinda dhidi ya maadui wanaotaka kuwadhuru. Nilipoendelea kudodosa,
nikasikia hizo hirizi watumiaji huwa wanavaa kwa kificho maeneo ambayo sio
rahisi kuonekana kama viunoni nakadhalika.
Kwa bahati mbaya huwa sijichoshi sana kufuatilia kama nikiona
jambo halina tija au haliwezi kuniathiri kwa namna yoyote (labda iwe ni
kwaajili ya kuwatahadharisha wengine au kujifunza). Sasa juzijuzi hapa nikiwa
ugenini mkoa fulani, kunarafiki yangu mmoja tulikuwa tunafanya naye kazi akawa ananisimulia
juu ya mdada mmoja ambaye ametokea kumpenda, na mdada mwenyewe kaanza kuonesha
ukaribu japo bado hajamwambia. Kwakweli alinisimulia jinsi huyo mdada alivyo
mzuri na ambavyo akimsogelea tu network inakata na anasahau kila kitu na
kumuwaza yule mdada; hahahaaa
Akaniambia niende mtaa anakokaa (rafiki yangu) ili nimuone
huyo mdada kwa maana akitoka kazini huwa wanapiga stori na ni nyumba jirani,
nikamkubalia. Basi nikaenda kama tulivyokubaliana, na nilimkuta yule mdada
hapo. Ki ukweli hana tatizo, ni mzuri wa sura na ni haki yake yule jamaa
kuchanganyikiwa. Yule dada alivaa gauni la mikono ya kukatwa (nakosa jina zuri,
lakini naamini umenielewa), wakati
namuangalia vizuri nikaona kwenye mkono wake wa kushoto katikati ya kiwiko na
bega amejifunga kamba nyeusi kama rangi ya kaniki zile za zamani na inakitu
fulani kimefungwa. Mhhhhh,
Nikamuliza mtu fulani alikuwa karibu kuwa kile ni nini alichojifunga yule mdada? Akajibu
‘HIRIZI’, ati nini??? Mbona
nilisikia wavaaji huwa wanaficha? Imekuwaje huyu ana ujasiri wa kuvaa hadharani
na tena ni binti mdogo kabisa, anaoneka mjuaji wa vitu vingi, na muonekano wa
kimjini-mjini. Duh, niliishiwa pozi aisee.
Ujue kuna vitu vingine kuvielewa kuwa huo ni ujinga na ni
utumwa kifikra sio lazima uwe mtu wa kanisani au msikitini. Kwa elimu na
utandawazi ulipofikia sasa kubadili mmfumo wa kufikiria sio ombi tena bali ni
lazima. Sasa inapotokea kuna mtu tena kijana anaamini juu ya kuvalishwa hirizi
leo hii eti awe salama? Mwisho wa siku
unakuwa mtu wa kujihami na kutuletea shida tu kwenye jamii yetu.
Jamii ya kishirikina ni jamii 'sindikizaji'. Haitafanya maendeleo kamwe!! |
Ikitokea malaria
imekushika ghafla unaanza kuwaza labda anakuchezea mtu mwenye hirizi kubwa
kuliko yako. Ikitokea umepata ajari, watu wanakuja kukuokoa wanakuta umejifunga
hirizi lako, nao watahusisha ajari hiyo na ushirikina. Ikitokea Mungu kakuita
ghafla ndio kabisaaaa, ndugu waliobaki wanaaanza kutafuta mchawi utadhani wao wataishi
milele. Dunia ya leo kuwa na imani za mfumo huo ni mzigo na nikujitengenezea
mabalaa na kurithisha watoto na wajukuu ujinga. Nasema hili kwa maana hata huyu
binti niliyemuona mimi mwenyewe najua fika haya atakuwa amejifunza kwa wazazi
wake tangu utoto na hapa tayari amekomaa na imani hiyo, hivyo ukijichanganya tu
na kumuoa wakati kafungamana na hayo madudu yao lazima watatafuta mbinu
kuyaapenyeza kwa watoto wenu ili urithi uendelee kwa maana watoto watakuwa
wanaenda kumtembelea bibi mzaa mama yao. Mama weeeeeee, !!!!
Wakati tunataka kuanzisha mahusiano yenye tija, kama vijana,
tusijisahau na kuangalia uzuri wa sura pekee au elimu. Kipengere cha mila na
desturi pia tamaduni zao huyo mwenzako jitahidi uzifahamu. Inaweza isiwe rahisi
sana kutokana na baadhi yao kuficha na utakuja kustukia madhara, lakini
tumuombe tu Mungu atusaidie katika kipengere hicho ili ukigundua usipoteze muda
wako na kujikuta anakuja na begi ukidhani ni nguo kumbe ni mihirizi ambayo
haimsaidii chochote zaidi ya kumpa presha tu kisaikolojia. Na ndio maana kuna mtu fulani aliniambia kwamba mtu ambaye ana amini
katika hirizi, ikitokea siku hajavaa au imepotea katika mazingira
yasiyoeleweka, mhusika ataugua hoiiiii napengine kufa kabisa. Sio kwasababu
hajavaa, bali kwasababu anaamini hayuko salama.
Hebu huu mwaka 2018 uwe mwaka wa mabadiliko kwa wenye imani
za ajabu na zisizo na tija kama hizi. Inasikitisha sana na wakati fulani
inachekesha. Tumuombe Mungu kwa imani zetu atusaidie kutuongezea uelewa kuwa
hatuwezi kukimbizana katika safari ya
maendeleo na uzalishaji mali kama bado mawazo na fikira zetu zipo kwenye
imani za kishirikina. Natafuta mbinu za kuongea na yule mdada ili nimuulize
mimi mwenyewe kuwa ‘kile ni kinini na kwanini kakivaa’ huenda ni ki-kuku cha
kiasili, hahahaaaa. Akiijibu nitakuja ku-edit hii mada yangu. Sikubali nataka
kupata majibu kutoka kwenye kinywa chake!!! Sasa kali ya mwaka mpya ni kwamba yule
rafiki yangu hajawahi kujisumbua kuumiza kichwa kuliwaza lile lihirizi la yule
mdada japo lipo waziwazi na kila siku linaonekana,yeye kapoteana na sura tu ya
yule mdada hahahaaaaaaa, Khaaa!! Hatari sana.
Eng Nguki Herman. M