I am targeted to change youth's mind set towards positivity.

I am targeted to change youth's mind set towards positivity.
I am targeted to change youth's mind set towards positivity

Saturday, 22 April 2023

Je kushika/kutumia au kuwa na mazoea na simu ya mumeo/mkeo kunaweza kuvunja ndoa?







Nimejaribu kutafakari juu ya jambo hili ambalo kwakweli sio jipya miongoni mwa jamii yetu. Ni kawaida kusikia makundi mawili yakikinzana juu ya kuwa na mazoea na simu ya mwenza wako hasa mke amekuwa akionywa sana kutokuwa na mazoea na simu ya mumewe. Hoja zimekuwa nyingi sana ambapo nyingi zimekuwa za kufikirika zaidi na zimejaa hofu ya kupigwa na adui usiyemjua.

Usiri kwenye simu ni uchochoro wa usaliti na kuishi kinafiki kwenye ndoa. Kwa bahati mbaya na jamii inawadanganya, Ohh usishike usije kupata presha, oh ana mambo yake sio lazima uyajue, what? Unapoingia kwenye ndoa hakuna mambo yako, kila kitu lazima kifahamike kwa wote. Ofcourse kuna vingine sio vya maana sana hata ukiviacha havina madhara. Nasisitiza kama hauna uhuru na simu ya mwenza wako, hujuwi password wala huwezi kuitumia, umepigwa marufuku kupokea wala chochote "basi mnaishi maigizo kwa asilimia kadhaa. 

NB: Kama uko comfortable keep going na maumivu yako.

Natoa pole kwa dada zangu ambao kwenye kitchen party na sendoff wamama wanawaambia simu ya mumeo ni sumu, sasa unakwenda kufanya nini kwa mtu mwenye sumu? halafu hapohapo wanakwambia nyie ni mwili mmoja, mwili what? mwili who? where? Which mwili my friend,  hakuna mwili wala ubavu hapo, ni maigizo mwanzo mwisho. Watu wakosee namba kwako/kwake tu? Mwenza ni wakili (advocate) lazima ajue vyote na ndio atakuwa wa kwanza kuulizwa/kukutetea likitokea lolote. Ni ngumu kumeza lakini ndio ukweli utakuja kuelewa siku moja.

Ok sawa, ulikuwa na mahusiano kabla ya huyu, si unasema tu? Na si unawaambia tu hao X,Y na Z kwamba sasa umeshaoa/olewa na unakata rasmi mawasiliano ya mahusiano  nao?. Kama hatakuelewa ujue na yeye hajakomaa kuwa mke/mume. Mpasuko unaanza mara tu utakaposema 'tunachat tu kwa siri, hatajua, siku unaumbuka ndio unasema 'tulikuaga.....au she/he is just a friend'

'Ee Bwana ukiokoe kizazi chetu'. Ni kweli hakuna mtu mkamilifu lakini mengine ni ujeuri wetu, kiburi chetu, ujinga wetu na kusahau au kujisahaulisha maana halisi ya agano la ndoa.

Ok bado hamjafunga ndoa, vipi ukimuuliza mtakuwa huru kila mtu kwenye simu ya mwenzake mkishafunga ndoa? Nasisitiza mkishafunga ndoa kwasababu kama sijafunga ndoa na wewe maana yake bado niko mawindoni at any time t seconds akipatikana aliyekuzidi vigezo nitafunga naye ndoa. Hivyo wakati huo kuna uwezekano wa kuwa na mitego mingi. Swali hapa ni ndani ya ndoa anasemaje? Majibu yake tu yatakupa picha kama hapa ni tia-maji tia-maji au la! Sasa jichanganye 'oh mapenzi upofu, hayaangalii sijuwi nini" sawa mwiba ukiingia vizuri I tell you utaona hata kwa lazima na utalia machozi! Nasema 'maacho yatafongokaaaaa'

Ee Bwana utuokoe sisi!

Nguki Herman.M

Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman

Asante kwa kusoma katika blog hii.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini

Saturday, 19 May 2018

Comments zinavyoweza kuvunja mahusiano/ ndoa

Mungu ndio anajua siri ya wapendanao


Rafiki yako akipost picha katika mitandao ya kijamii, kabla ya kuwaza kusema chochote kuihusu (ku-comment) huwa unachukua hata dakika moja kuwaza madhara yatakayotokana na comment yako? Au huwa unatiririka tu kuandika, tafakari itafuata badaye? Mara ngapi umeshuhudia comment ya mtu kwenye post ya mtu mwingine imezua varangati na majibizano yanayoashiria mmoja kaumizwa nafsi?
Nitajikita sana kwenye matukio ambayo ni ya kawaida kwa mapito ya mwanadamu kulingana na mazigira aliyopitia na watu aliokutana nao (exposure). Mara kadhaa nimekua nikisema kuwa mambo tunayofanya hayafutiki mioyoni mwa watu, ndio yanakaa na kuhifadhiwa. Na ndio maana kama ulikuwa na tabia fulani nzuri au mbaya wakati unasoma, basi hata kama baada ya miaka ishirini, wale uliosoma nao wanaweza wakawa wanawasimulia watu wengine ile tabia yako kwa maana wanaikumbuka! Ndio maana vijana tunatakiwa kuwa makini sana na kila tunachokifanya ili watoto wetu wakija kusimuliwa tusiumie mioyo au wakaona kumbe baba/mama yao alikuwa hamnazo.

Inakuwaje hii?
Inakuwa hivi: Unakuta Mkaka/mdada kapost picha yake mtandaoni anavalisha/anavalishwa pete ya uchumba (engagement) au amefunga ndoa safi kabisa. Ndio amefunga ndoa Mungu kambariki na kufikia hapo. Sasa mtu mwingine labda kasoma naye sekondari huko anakuja na kuona ile picha, na anakumbuka tabia za yule mdada/mkaka kuwa labda zilikuwa mbaya, au alikuwa na mahusiano motomoto na mkaka/mdada mwingine ambaye sio huyu aliyefunga naye ndoa! Bila hata kufikiria mara mbili unakuta anadondosha comment kama hii hapa:

v  Heh! Jamani mbona huyu sio yule shemela XY mliyekuwa naye shule jomoni? Mm we mdada/mkaka mhuni jamani, kha! Mlivyokuwa mnapendana vile kumbe ni uzushi tu? Hongera lakini.

v  Wacha weee, kumbe XY ulimpiga chini, koh,koh,koh simpatii picha povu lake akiona jamaa mwingine kakubeba.

v  Wapi XY?? Nani kamasaliti mwenzake?

v  Mhhhh, sitaki kuamini, yani XY alikuwa anakuhudumia hadi ukiugua, kumbe ilikuwa drama tu?
v  Hivi huyu ni XY kweli? Au macho yangu yananidanganya? Teh,the,teh

v  Duuuhhh kweli mapenzi ni kizungumkuti, kumbe XY mlikuwa mnachezeana tu, hongera lakini mwaya.

v  Heh, jomoni, wewe si ulitutambulisha XY kuwa ndio shemela mtarajiwa? Mliishia wapi tena? Hihihiiiii

v  Mwingine anaamua kuchukua hiyo picha na kupost kwenye ukurasa wake au kwenye magrupu ambako wewe huna uwezo wa kufuta comments wala kuona ili wakujadili vizuri. Tena anasindikiza na vi-emoji vya kinafikiii!!

Ukiangalia kwa makini hizo comments zinaonnesha huyu mtu anamfahamu vizuri mhusika na mapito yake. Na ukweli ni kwamba comment yake ipo sahihi kabisa!! Lakini je, unajua madhara yake kwa mhusika?
Mahusiano yana siri kubwa. Usiwavuruge waliopiga hatua chanya


Sikiliza kwa makini! Kila binadamu ana mapito yake aliyopitia, napengine aliingia kwenye mahusiano kwa sababu ya ujinga, shinikizo, kuiga , kujaribu au kwa nia njema lakini humo njiani akakuta mambo siyo yenyewe na kubadili gia angani. Ni kweli msichana au mvulana huyo alikuwa hivyo sekondari au chuo, lakini je, unajua yaliyomkuta? Wakati tunaongea na vijana huwa mara zote tunasisistiza kugeuka iwapo wapo kwenye mahusiano yasiyo na tija (Second chance). Hii inamaana kama ulijipachika mahala na ukagundua ulikurupuka au mambo tu huyaeleweki, basi jitoe ili upate nafasi ya kukua zaidi na kufanya uchaguzi mwingine.

Kuna mtu anasema;  ‘weeeee, maumivu yake ni hatareee!!!’ Ndio, kuna maumivu makubwa sana, utalia, utaapiza, utatoa matamshi ya laana, utajiona mjinga, hufai na mengine mengi, na kubwa zaidi unaumizwa na maswali ya waliokuwa wanajua mko pamoja! Lakini hayo yote ni mapito tu, chukua hatua, utapona na kuendelea kusonga mbele! Ukiona hauna amani, unaenda tu kama unamsindikiza mtu, na matarajio yako huyaoni au yule uliye naye analalamika kuwa matarajio yake hayaoni na mnasukumwa na huruma tu, chondechonde (kama maridhiano yamegonga mwamba) vunjeni huo uhusiano kabla hamjafika mbali kwa maana mnatengeneza bomu la kuja kusalitiana badaye. Haijalishi wangapi wanajua, sio marafiki, unaosali nao, wazazi wako, umempost sana mitandaoni nakadharika, HAO WOTE HAWATAKUJA KUISHI NA NYIE, NI WAPAMBE TU, LAKINI CHUMBANI MTAJIFUNGIA WAWILI PEKE YENU NA MUNGU WENU!

Acha akili za kijinga kucomment negative side ya mtu ambaye kapiga hatua. Ulitaka umuoe wewe? Au ulitaka akuoe wewe? Au ulikuwa unampenda akakugomea? Ameshavalishwa pete sasa! Unasemaje? Ndio ameshaoa/olewa, unatakaje? Unaandika maneno yanaingiza ndoa ya watu migogoro, mtoto wa watu anapata kazi ya kujielezaaaa kwa mume wake kisa nyau tu mmoja umekurupuka huko. Ulilazimishwa U-comment?? Wao wanajua walielezanaje mapito yao ya nyuma, na wamekubali kubebeana mizigo. Uliacha kumsema kipindi kile kapotea, sahizi kabadilika ndio unaleta maneno yako kwa reference ya mambo ya nyuma! Stop it please! Waache waoane, waache waoaneeeee!!
Ndoa na iheshimiwe na watu wote. Mambo waliyopitia kila mmoja huko nyuma hayakuhusu wewe mwingine (Third party)


Kitu cha msingi ukiwa kwenye mahusiano ni kuepuka kufanya ngono! Hii itakupunguzia maumivu siku ukiona mahusiano hayana tija na unaamua kuyavunja. ‘Nyanyachungu and 12 others reacted to your photo’, Heh, sawa tu endelea ku-react but wenzako wameshapanda madhabahuni na wanaazisha familia!! Sio lazima u-comment, unaweza kupita tu na kuacha kuwaza. Mwingine wanaonana kwenye daladala anaanza kumhoji, Oh fulani vipi, XY yuko wapi, Siamini kama hamkuoana naye, ilikuwaje , ooo,, iiii , kwikwiiii, Heh! Kazi ipo.

Kama unataka kujua yaliyowakuta, mitandao yooote ina inbox. Nenda huko inbox kamuulize nini kilitokea kwenye mahusiano yao, hata hivyo sio lazima akuambie kwa maana wewe sio stakeholder wa maisha yake. Na sio kukurupuka ku-comment maneno yatakayozua mzozo kati yake na mwenzi wake. Na bahati mbaya zaidi siku hizi unakuta karibu familia nzima ipo mtandaoni (pande zote mbili). Wazazi, wakwe, mashemeji, mawifi wote wapo huko. Sasa wewe unaleta comment kwenye post ya uchumba au ndoa ya mtu kutoa kashfa na ndugu wa upande wa pili wanaona, hapo lazima utaanzisha mjadala huko kwamba mtoto wetu kaoa/olewa na mtu asiyefaa na kuna uwezekano mkubwa wa ndoa kuingia shubiri kuanzia mwanzo kabisa!!

MWANAMKE: Furaha yako, amani ni zaidi ya mtu! Hivyo usiyumbishwe au kutishwa na mtu kwa maamuzi uliyofanya na umejiridhisha kuwa yana tija.
MWANAMME:Ujasiri wako na amani yako ni muhimu kuliko mtu. Ikiwa unaona matarajio ya binti wa watu huyafikii na unaishia kumtesa tu kwa mawazo ni bora umuache ili akajitafutie mtu ambaye atampa amani.
Ikumbukwe pesa, elimu au kazi ya mtu haina mchango mkubwa kwenye upendo, bali ni amani uliyonayo kuwa na mtu na matarajio ya hatua chanya mtakazopiga kwa pamoja.
Hata hivyo haya ni mawazo  yangu tu, sio lazima yafanane na ya kwako! Kwa moyo mkunjufu nikutakie tafakari njema.

Eng Nguki Herman. M

Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman

Asante kwa kusoma katika blog hii.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com



Friday, 5 January 2018

Heh! Kumbe Wavaa Hirizi Bado Wapo?

Kwa dunia ya sasa kubadili fikira zetu ni lazima sio ombi!
Habari. Namshukuru Mungu pamoja nawe kwa kutuwezesha kufika mwaka mpya wa 2018, hakika ni neema ya upendeleo kabisa kutoka kwa Mungu wetu. Na sio jambo la kulichukulia kawaida hata kidogo, bali litutafakarishe na kutufanya tuishi  vyema kwa busara na mipango akinifu.
Sasa tuje kwenye mada yetu ya kufungulia mwaka!. Kwa kipindi kirefu nimekuwa nikisikia tu neno hirizi na kwamba kuna watu wanavaa kama kinga kwa imani za kishirikina, wakiamini kuwa zinawakinga au kuwalinda dhidi ya  maadui wanaotaka kuwadhuru. Nilipoendelea kudodosa, nikasikia hizo hirizi watumiaji huwa wanavaa kwa kificho maeneo ambayo sio rahisi kuonekana kama viunoni nakadhalika.

Kwa bahati mbaya huwa sijichoshi sana kufuatilia kama nikiona jambo halina tija au haliwezi kuniathiri kwa namna yoyote (labda iwe ni kwaajili ya kuwatahadharisha wengine au kujifunza). Sasa juzijuzi hapa nikiwa ugenini mkoa fulani, kunarafiki yangu  mmoja tulikuwa tunafanya naye kazi akawa ananisimulia juu ya mdada mmoja ambaye ametokea kumpenda, na mdada mwenyewe kaanza kuonesha ukaribu japo bado hajamwambia. Kwakweli alinisimulia jinsi huyo mdada alivyo mzuri na ambavyo akimsogelea tu network inakata na anasahau kila kitu na kumuwaza yule mdada; hahahaaa

Akaniambia niende mtaa anakokaa (rafiki yangu) ili nimuone huyo mdada kwa maana akitoka kazini huwa wanapiga stori na ni nyumba jirani, nikamkubalia. Basi nikaenda kama tulivyokubaliana, na nilimkuta yule mdada hapo. Ki ukweli hana tatizo, ni mzuri wa sura na ni haki yake yule jamaa kuchanganyikiwa. Yule dada alivaa gauni la mikono ya kukatwa (nakosa jina zuri, lakini naamini umenielewa), wakati namuangalia vizuri nikaona kwenye mkono wake wa kushoto katikati ya kiwiko na bega amejifunga kamba nyeusi kama rangi ya kaniki zile za zamani na inakitu fulani kimefungwa. Mhhhhh,

Nikamuliza mtu fulani alikuwa karibu kuwa kile ni nini alichojifunga yule mdada? Akajibu ‘HIRIZI’, ati nini??? Mbona nilisikia wavaaji huwa wanaficha? Imekuwaje huyu ana ujasiri wa kuvaa hadharani na tena ni binti mdogo kabisa, anaoneka mjuaji wa vitu vingi, na muonekano wa kimjini-mjini. Duh, niliishiwa pozi aisee.
Ujue kuna vitu vingine kuvielewa kuwa huo ni ujinga na ni utumwa kifikra sio lazima uwe mtu wa kanisani au msikitini. Kwa elimu na utandawazi ulipofikia sasa kubadili mmfumo wa kufikiria sio ombi tena bali ni lazima. Sasa inapotokea kuna mtu tena kijana anaamini juu ya kuvalishwa hirizi leo hii eti awe salama? Mwisho  wa siku unakuwa mtu wa kujihami na kutuletea shida tu kwenye jamii yetu.
Jamii ya kishirikina ni jamii 'sindikizaji'. Haitafanya maendeleo kamwe!!

 Ikitokea malaria imekushika ghafla unaanza kuwaza labda anakuchezea mtu mwenye hirizi kubwa kuliko yako. Ikitokea umepata ajari, watu wanakuja kukuokoa wanakuta umejifunga hirizi lako, nao watahusisha ajari hiyo na ushirikina. Ikitokea Mungu kakuita ghafla ndio kabisaaaa, ndugu waliobaki wanaaanza kutafuta mchawi utadhani wao wataishi milele. Dunia ya leo kuwa na imani za mfumo huo ni mzigo na nikujitengenezea mabalaa na kurithisha watoto na wajukuu ujinga. Nasema hili kwa maana hata huyu binti niliyemuona mimi mwenyewe najua fika haya atakuwa amejifunza kwa wazazi wake tangu utoto na hapa tayari amekomaa na imani hiyo, hivyo ukijichanganya tu na kumuoa wakati kafungamana na hayo madudu yao lazima watatafuta mbinu kuyaapenyeza kwa watoto wenu ili urithi uendelee kwa maana watoto watakuwa wanaenda kumtembelea bibi mzaa mama yao. Mama weeeeeee, !!!!

Wakati tunataka kuanzisha mahusiano yenye tija, kama vijana, tusijisahau na kuangalia uzuri wa sura pekee au elimu. Kipengere cha mila na desturi pia tamaduni zao huyo mwenzako jitahidi uzifahamu. Inaweza isiwe rahisi sana kutokana na baadhi yao kuficha na utakuja kustukia madhara, lakini tumuombe tu Mungu atusaidie katika kipengere hicho ili ukigundua usipoteze muda wako na kujikuta anakuja na begi ukidhani ni nguo kumbe ni mihirizi ambayo haimsaidii chochote zaidi ya kumpa presha tu kisaikolojia. Na ndio maana kuna mtu fulani aliniambia kwamba mtu ambaye ana amini katika hirizi, ikitokea siku hajavaa au imepotea katika mazingira yasiyoeleweka, mhusika ataugua hoiiiii napengine kufa kabisa. Sio kwasababu hajavaa, bali kwasababu anaamini hayuko salama.


Hebu huu mwaka 2018 uwe mwaka wa mabadiliko kwa wenye imani za ajabu na zisizo na tija kama hizi. Inasikitisha sana na wakati fulani inachekesha. Tumuombe Mungu kwa imani zetu atusaidie kutuongezea uelewa kuwa hatuwezi kukimbizana katika safari ya  maendeleo na uzalishaji mali kama bado mawazo na fikira zetu zipo kwenye imani za kishirikina. Natafuta mbinu za kuongea na yule mdada ili nimuulize mimi mwenyewe kuwa ‘kile ni kinini na kwanini kakivaa’ huenda ni ki-kuku cha kiasili, hahahaaaa. Akiijibu nitakuja ku-edit hii mada yangu. Sikubali nataka kupata majibu kutoka kwenye kinywa chake!!! Sasa kali ya mwaka mpya ni kwamba yule rafiki yangu hajawahi kujisumbua kuumiza kichwa kuliwaza lile lihirizi la yule mdada japo lipo waziwazi na kila siku linaonekana,yeye kapoteana na sura tu ya yule mdada hahahaaaaaaa, Khaaa!! Hatari sana.

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Asante kwa kusoma katika blog hii.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

Sunday, 3 December 2017

NIMEMPA MIMBA, WAZAZI WAKE WANATAKA NDOA NDANI YA WIKI MOJA,

Kama maandishi hayasomeki kwa mobile version, shusha mwishoni utakuta "View web version" click hapo.

Natambua fika hatari ya kujamiiana kabla ya ndoa na matokeo yake. Moja wapo ni mimba, na ikumbukwe hapa tatizo sio mimba bali ni mfumo wa kuipata/kusababisha na uwezo wa kuhudumia mimba yenyewe na mtoto atakayezaliwa. Hili nalitambua vizuri sana na nimekuwa nikiliongea na kuliandika kila uchwao, sio kwa kuhukumu hapana, hii ni kwasababu kuzaliwa ndani ya ndoa au nje ya ndoa hakufanyi azaliwe kiumbe tofauti, japo kuna hatari ya myumbo katika malezi na kumkosesha mtoto baadhi ya haki fulani za msingi au kukosa uhuru.

Katika hali isiyo ya kawaida nilijikuta nimempata msichana fulani na kufanya naye ngono, na kumpa mimba siku hiyo hiyo. Mimi  sikutambua kuwa nimempa mimba na yeye alisema kuwa hawezi kupata mimba. Basi baada ya muda fulani wazazi wake waliniita na kuniambia nimempa mimba mtoto wao na wanachotaka ni ndoa kabla mtoto hajazaliwa kwa maana hawataki mjukuu wa nje ya ndoa. Na ikiwezekana nimuoe ndani ya wiki moja.

Mungu wangu weee, presha ilinipanda, viungo vyote viliishiwa nguvu, nikawaza na kuwazua nitaishije na kumlea huyu binti, tena sina kazi na akaunti yangu benki inapumulia mashine hata elfu kumi hakuna. Nikawaza juu ya makazi na kugundua nina chumba kimoja tu nacho wanakaa wadogo zangu wawili wanaosoma tena ninawahudumia mimi mwenyewe na hawana sehemu ya kwenda. Rafiki yangu mmoja akaniambia ‘Nguki hapa komaa tu mzee baba, ndani ya wiki hii oa tu’.
Ukweli nilikuwa na hamu sana ya kuitwa baba, eh, niwe na mtoto. Lakini sasa njia niliyotumia ndiyo inayonipa majuto. Nikawa nawaza juu ya rafiki zangu na watu wa karibu, wataelewaje kuona ndoa imeibuka kama uyoga hakuna cha kuvalishana pete wala send off wala nini? Huku wazazi wa yule binti ndio kwanza hawataki kusikia chochote. Basi nikajikaza kisabuni hadi kwa baba yangu mlezi, akasema ‘hiyo changamoto umeizalisha mwenyewe na hakuna kukwepa. Mimi nitakuongezea hela kidogo kwaajili ya hizo harakati zako, kama utaongezea kwenye harusi sawa, kama ni kwemnye maisha utajua mwenyewe’ 


Kuna wakati mambo yanakaba hadi unajionea aibu wewe mwenyewe.


Kichwa kiliniuma sana, hadi nikahisi yule msichana ananidanganya. Nikampigia simu ili aje niliangalie tumbo vizuri kama linaonekana kuongezeka ukubwa. Alikuja na kunikuta nipo na rafiki zangu nimejiinamia kwa mawazo. Akafika pale akiwa ameniletea na mikate, nikamuaangalia kichovu na kumuuliza kama yuko serious kweli nilimpa mimba kwa tendo lile moja au ananipima tu akilia, akanisogelea kwa karibu, mamamamamamama weeeeeee, katumbo kamejaa mwanawane, yani hakuna ubishi. Akanishika kichwa changul kwa tabasamu na kuniambia kingereza ‘Nguki, do you think I am lying to you? This pregnancy is yours’. (Akiwa na maana nisidhani anadanganya, hiyo mimba ni yangu). Aliongea kwa kujiamini, bila wasiwasi huku akinishika kidevu changu kilichokauka kama mti mkavu kwa presha tangu nizipate hizi habari.

Kwakweli sijawahi pata maumivu ya kichwa na mawazo makali kama haya, nilitazama juu na kuona kama Mungu kaniacha, jeuri yangu ya kuwashauri vijana wenzangu ikayeyuka ghafla, nikiangalia wazazi wangu hawana uwezo wa kujitwisha hii changamoto. Nikajiuliza, nini kinafuata bado sikupata jibu. Nilijikuta nalowa jasho mchana na usiku sipati cha kufanya na wiki moja niliyopewa na wazazi wake yule binti niliye mtumbilize ndio hiyoooo inaisha.

Rafiki yangu akaniambia niende kwa wazazi wa yule binti kuwaambia nimeshindwa kutekeleza masharti yao na kama kuna lolote wanataka kufanya juu yangu kwakweli wafanye tu, maana sioni cha kufanya juu wala chini, zaidi najikuta nakonda tu ndani ya wiki moja. Basi yule jamaa yangu akanipakia kwenye pikipiki yake, haooooo hadi nyumbani kwa wazazi wa yule binti..
Kichwa kinazungukaaa kama mpira, lakini hakuna pa kutokea!


Tulimkuta mama yake akiwa nje, alipotuona tu, akamuita mumewe aliyekuwa ndani. La haulaaaaa, yule mzee alipotoka alinikata jicho hilo kwa muda katika tano bila kuongea chochote! Ohh Mungu wangu weeee, hofu ikanitanda, huku navuja jasho nikadondoka chini kama fulushi puuuuuu!, Wakati nahangaika kusimama  kwa kuishika mikono ya yule rafiki yangu, nikagundua nimeshikilia neti na nilikuwa nimezinduka kutoka kwenye ndoto yangu! Loooh, nilikuwa navuja jasho, nikainuka na kukaa, nikajikuta natamka kwa nguvu ‘Mungu, nini lakini jamani’. Asikwambie mtu, sijawahi ota ndoto yenye kashkash kama hii ya usiku wa kuamkia 25/11/2017. 
Nilipoamka nikawa nawaza hivi hizi presha ni katika ndoto, je ingekuwa live?


Narudia tatizo sio mimba bali mfumo. Aisee hizi presha sizitaki kabisaa,hii ni ndoto lakini imenipa picha nzima ya hali ambayo nitakutana nayo endapo nitajitoa ufahamu. Nakushauri na wewe kijana mwenzangu amini katika subira na jiwekee tu malengo, haya yote uyafaidi ndani ya ndoa. Narudia tena hapa hatunyoosheani vidole au kuhukumu, hapana, bali kama umewahi kukosea, basi fanya ukarabati mkubwa (Major rehabilitation) wa nafsi ili usikosee tena na kujiwekea nafasi nzuri ya kuwa mlezi bora wa familia.KUSUBIRI INAWEZEKANA, ANZA SASA.


Kitabu changu Kipya


Katika kujifunza pia nakukaribisha uniunge mkono kwa kununua kitabu nilichokiandika (DHAMIRI NA UTASHI VIMETEKWA) ambacho ndani nimeeleza mambo mengi yahusuyo mahusiano, upendo, subira, kuweka malengo, na malezi. Nimekielekeza kwa vijana, lakini pia wazazi na walezi kitawafaa sana ili kuongea na watoto/vijana wao. Ili kukipata waweza nitafuta kwa namba zangu hapo chini. Lakini pia kinapatikana  Dar es Salaam (Doloka Investment Company Ltd Millenium Towers Makumbusho-0655 266 993 na Pia Kijichi-0686 971 623), Morogoro kinapatikana chuoni Sua (nipigie nikuunganishe na wanaokiuza), Kinapatikana pia Fransalian Bookshop-Kola Morogoro na Iringa ofisi za UCE Tanzania, Kihesa-Kichangani.Karibu sana ujifunze.

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Asante kwa kusoma katika blog hii.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com




Monday, 18 September 2017

BANDO LA MUNGU HALICHACHI.


Upendo wa Mungu hauna kipimo

Tumsifu Yesu Kristu/Bwana aifiwe/Shalom. Leo tutatafakari sehemu ndogo ya maandiko matakatifu kutoka kitabu cha nabii Isaya ambapo tutaona ukuu wa maneno yenye pumzi ya Mungu hivyo kujenga hoja ya ‘Bando la Mungu kuwa la kudumu, yaani halichachi.’

Tunasoma Isaya 43:1-5
1 Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu.
 2 Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.
 3 Maana mimi ni Bwana, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako.
 4 Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.
 5 Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi.

NOTE: Aliyekuhuluku=Aliyekuumba

Kuna uwezekano mkubwa baada ya kusoma sehemu hiyo ndogo ya maandiko matakatifu, kuna ujumbe fulani mfano wa mwale wa mwanga unapita kwa haraka kichwani mwako. Sasa mimi nitapita na baadhi ya dondoo na kuzipa maelezo kidogo lengo likiwa ni kushirikishana ukuu wa Mungu.
Mungu ni Upendo


  • Usiogope, maana nimekukomboa. Kuna wakati fulani nikawa najiuliza, mbona haijaandikwa usiogope maana NITAKUKOMBOA, bali NIMEKUKOMBOA? Herufi ‘ME’ ni wakati uliopita mtimilifu (past participle), sasa inakuwaje tumeambiwa tusiogope kama suala la ukombozi lilishafanyika? Yani mwanafunzi anakuwaje na hofu wakati kashakabidhiwa mkononi majibu ya mtihanai wake na amefaulu?. Kilichopo hapa ni kwamba bado kuna kundi kubwa la watu (huenda nikawa mmoja wapo) ambao zawadi ya ukombozi iko mikononi mwao, lakini bado wamejawa na hofu na kutumia nguvu nyingi sana kushughulikia mambo madogo na ya kawaida kana kwamba kuna mtu fulani kashikilia maisha yao zaidi ya Mungu. Kumbe Mungu mwenyewe kwa kinywa cha nabii Isaya anatuambia leo tutupilie mbali hiyo hofu na kujivunia ukombozi ambao kwa hiyari yake ameamua kutuzawadia.
  •  Nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Mtu akikuita kwa jina lako ina maana anakufahamu vizuri. Hata wanyama tu wa kufugwa, ukiwaita kwa majina wanakuwa na amani kuwa wewe ndio mchungaji wao na watakuja miguuni pako na kunyenyekea, japo hawana utashi. Nabii Isaya anatukumbusha kuwa Mungu hajaishia kutuita majina tu, bali anatusisitiza kuwa sisi ni mali yake kwa maana hata mpita njia anaweza kukuita jina lako. Kuna wakati tu kwa makusudi tunaziba masikio na kutosikia atuitapo. Kila mara inawezekana dhamira yako ikawa inakutuma kufanya jambo fulani au kukuonya kutofanya jambo fulani lakini  ukatumia nguvu nyingi kupambana na kujikuta hauitii, ina maana unajitengenezea ukuta kati yako na Mungu. Mara nyingi dhamiri huwa ipo sahihi na ndio maana kama mwili unakusukuma kufanya jambo lisilo jema , dhamiri hai hupingana na wewe kwa kuleta ugumu (resistance) katika mjongeo utakaokupeleka huko.
  • Maji mengi na mito havitakugharikisha, moto hautakuteketeza. Katika sehemu hii ya maandiko, majina moto na maji vimetumika kuwakilisha matatizo, mahangaiko na changamoto za kila siku. Kumbuka Biblia haijasema kuwa hautakumbana na huo moto au maji, bali imesema utakumbana navyo lakini havitakudhuru. Kwa lugha rahisi ni kwamba matatizo, changamoto na magumu tutaendelea kukutana nayo lakini hayataweza kutukengeusha na kututoa kwenye msitari wa imani. Yote hayo ni kutokana na upendo wa Mungu usio na kikomo kwetu, hivyo kama shukurani kwa Mungu tuzishinde changamoto kwa kuonesha ustahimilivu na ukomavu wa imani ili Mungu kwayo ajitwalie utukufu.
Mungu anatutetea dhidi ya maovu ili matendo yetu yazidi kuangaza

  • Ulikuwa wa thamani na kuheshimiwa machoni pangu, nimekupenda. Kumbe kupendwa ni zao la kuthaminiwa. Mtu hawezi kukupenda kama hajuwi thamani yako, ‘Value brings love’. Ndivyo ilivyo kwa Mungu, ametupandisha hivi hata kutuita wa thamani na heshima machoni pake, naam ndipo haswaaa anasisitiza kuwa ametupenda. Upendo wa Mungu hauna kipimo kwetu, na ndio maana kuna wakati huwa natafakari ingelikuwa ukifanya kosa na kurudia basi Mungu anachukua roho yako, je ingekuwa ni miaka mingapi tangu nizikwe? Jiulize pia wewe mwenzangu binafsi. Hakika ni wa huruma sana, sawasawa na neno lake katika Zaburi 130:3 Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?
  • Nitatoa watu kwaajili yako na kabila za watu kwaajili yako. Ndio, hili liko wazi na shuhuda kwa watu wengi nikiwemo mimi nisiyestahili. Kuna wakati fulani mambo yanakaba kila upande, inafika kipindi unauona mwisho wako uleeee unakaribia. Ghafla bin vuu anatokea mtu, watu au familia fulani inakuokoa kwenye changamoto au tatizo lako, mwisho wasiku unajiuliza hivi walikuwepo wahitaji wangapi ambao yamewakaba zaidi yangu? Imekuwaje iwe kwangu? Huyu ndio Mungu tunayemuabudu, Mungu wa surprise, Mungu wa kuinua watu pale usipotarajia ili uyaone matendo yake makuu na kushuhudia ukuu wa jina lake. Katika hili, nakukumbusha kuwatembelea wahitaji wa aina zote na kufanya lile uwezalo kwaajili yao.
  •  Usiogope kwa maana mimi ni pamoja nawe. Hapa ndipo penye uhakika wa kuendelea kumuamini na kutembea kifua mbele huku taa yetu ikiwa ni Msalaba wake (Marko 8:34). Ndio kasema mwenyewe kuwa hofu tuididimize huko shimoni, nasi tuwe na uhakika wa uwepo wake kutupigania. Sasa kama baba yako ameshasema ‘usiogope nitakupa unachotaka’, hivi unaanzaje kutapatapa huko kusikojulikana? Tulia ujichotee neema bwerere kutoka kwa mchungaji wako ambaye anakujua kwa jina na sikuzote anapita kwenye mlango wa boma lako.
Usiogope, Mungu yupo kwaajili yako


Hakika bando la Mungu halichachi, tena kwa upekee wake halina kiwango, wewe ni kupiga tu kwa maana umechorwa kwenye viganja vya mikono yake, anajua hofu zako na kila kitu. Basi Mungu awe nasi tunapotafakari matendo yake makuu na ya kuogofya, huku tukijibidiisha kutenda mema kwa wenzetu, unyenyekevu na utii ni baba wa yote. Kama ukiwa na nyongeza au swali unakaribishwa kupitia sehemu ya ku-comment hapo chini, au hata kwa mitandao mingine ya kijamii utakakokuta link ya mada hii. Neema ya Mungu Baba, na upendo wa Yesu Kristu na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nasi sote, sasa na hata milele. Tumsifu Yesu Kristu

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Asante kwa kusoma katika blog hii.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

Monday, 11 September 2017

KUWA MAKINI NA WATU HAWA. NI HATARI

Masikio yako yachuje kila unaloambiwa kabla ya kuchukua hatua.

Leo ni siku ya kutafakari baadhi ya aina ya watu ambao tunatakiwa kuwa nao makini sana hasa wale wenye nafasi ya kuweza kubadilisha mawazo yako. Kuna kundi la watu huenda wapo kwako kama marafiki maalumu sana kama ambavyo kilatini wanaitwa familiaritas au confidential friendship kwa kingereza. Hawa ukiwashirikisha mipango yako, na ikatokea wakakupatia marekebisho au mapendekezo lazima kuna uwezekano wa zaidi ya 70% kuyakubali.

Sasa nikupe orodha ya baadhi ya watu ambao inabidi unatakiwa kujua hawafai kuwaamini na wanaweza kukupeleka porini na kukwamisha mipango yako:

01.  Mtu anayeona yeye ni bora kuliko wengine wote:
Hapa lazima tuwekane sawa tafadhari. Point hii hailengi kumfanya mtu ajione dhaifu, la hasha!. Hapa nalenga mtu ambaye katika mazungumzo yake yote hufanya marejeo ya udhaifu wa wengine ukilinganisha na uimara wake. Mfano ukiona mtu kwenye mazunumzo yake kauli kama ‘Usinifananishe mimi na fulani, mimi nina uwezo zaidi/ unapoteza muda kuwa na fulani, mimi ndio ninauwezo wa kukuhudumia/ umempendea nini yule? Ona mimi nina x,y,z ambazo yule hana uwezo wa kuwa nazo/ Mimi ni mzuri sana, siendani na wewe, au unaniona kama fulani, mimi ni msomi kuliko fulani, mimi nina akili kuliko fulani’ hazikosekani basi ujue mtu huyu kuna uwezekano mkubwa wa kukupoteza au kutokuwa na mchango chanya kwenye ushauri wake, na pia wengi ni waongo.

02.Mtu anayejihami bila sababu (Defensive people).
 Hii ni aina ya watu ambao wao huwa wanajitanguliza kuona wapo sahihi kabla hujaanza kuhoji utendaji wao. Kwa mfano ukiona mtu unamwambia; ‘hapo umekosea’ halafu yeye anajibu ; ‘unadhani nilifanya makusudi? Sasa unadhani kwa mazingira haya ningefanyeje? Hata ungekuwa wewe ungefanya hivihivi’. Mtu kama huyu kufanya marakebisho baada ya kukosea huwa ni mgumu sana. Unatakiwa kuwa naye makini sana, na kama ni mwanafamilia (mke/mume) itakuwa vyema ukimtambua kwenye kipengere hiki, vinginevyo unaweza kuwa unaumia moyo kila siku na wakati mwingine kukosa amani ndani ya moyo wako.

03.Mtu anayelazimisha wote kuamini njia yake ya mafanikio ndio pekee ya kufuata
Hapa ndio kwenye shida zaidi, na watoto wadogo ndio walio kwenye hatari kubwa sana ya kuambukizwa huu ugonjwa. Kwa mfano, wapo watu ambao wamefanikiwa nje ya mfumo wa taaluma, sio kwasababu waliamua tu kuelekea huko, bali kuna mazingira yaliwatoa kwenye taaluma na kujikuta wanafanikiwa kutumia vipaji binafsi au kusaidiwa na watu wa karibu walio na msingi bora kwa kifedha. Watu wa aina hii baadhi yao hujikuta wanawaweka njiapanda walio kwenye taaluma kwa kuwaambia kuwa wanapoteza muda huko na hawatafanikiwa, na afadhari wajiunge nao nje ya mfumo wa taaluma kitu ambacho ni hatari sana kwa maana sio kila mtu anaweza kufanya kila kitu katika mazingira yote. Wapo pia ambao kwasababu wamefanikiwa kwa njia ya taaluma, basi wanawavuruga vichwa wale wanaopambana nje ya taaluma na kujikuta hawaweki bidii huko waliko. Huu ni upotoshaji, acha kila mtu afuate njia ambayo Mungu amempangia, kikubwa iwe sahihi na yenye kukubalika. Watie moyo watu kule waliko, sio lazima wote uwalazimishe kufanya kama wewe, na mambo yakiwachachia huko, utaanza kuwacheka tena kwa kuwaambia wanazembea au hawakusikilizi vizuri.
Kazi kwako, utamsikiliza yupi na uache yupi
.
04. Mtu anayesifia uovu kama njia ya kawaida ya maisha.
Vijana wengi tupo kwenye huu mtego wa kushawishiana. Kwa mfano mtu anajisifia uhodari wake wa kuwa na mahusiano holela kwa siri, udanganyifu, wizi, matusi, kutoheshimu wazazi au walezi, unyanyasaji katika mahusiano au katika mazingira yoyote. Ukiona katika mazungumzo yake mtu haoni aibu kujisifia katika mambo haya huyo ni hatari katika mustakabali na ustawi wa jamii yoyote ile, na haaminiki kwa lolote kwa maana dhamiri yake imesheheni dumuzi na uso usio na huruma kwa wanaoteseka kwa matokeo ya maamuzi yake.

05. Mtu asiye na ratiba. 
Hora argentum’; ni msemo wa kilatini unaofanana na ule wa kiingereza ‘time is money’ ikiwa na maana muda ni pesa/mali. Mtu ambaye hana mpango mkakati wa kuhakikisha anafanya jambo fulani kwa muda fulani mambo yake kamwe hayawezi kwenda. Ukiona mtu yupo tayari kwenda mahali popote anapoambiwa aende kwa muda wowote huyo hana ratiba , hafahamu namna ya kufanya kwanza jambo la kwanza. Yaani kuna watu rafiki yake akimwambia waende mjini anakubali bila kuhoji anaenda kufanya nini na je lilikuwa kwenye ratiba yake? Wakiwa njiani akipigiwa simu na  rafiki yake mwingine kuwa waende porini anakubali, hehhh, jamani, yani ikifika jioni yuko hoi na hakuna hata moja la kujivunia alilofanya katika ratiba yake. Kiukweli mtu asiyejari muda mimi huwa hazipandi kabisa. Lazima tufahamu kuwa muda ni rasilimali ya kipekee ambayo ni kama haionekani (invisible resource) lakini ikipotea hairudi tena, hivyo mtu asiye na ratiba unatakiwa kuwa naye makini sana ili usije ungana naye kuelekea shimoni.

06. Mtu asiyetaka kurekebishwa/asiyefundishika.
 Hili ni kundi jingine ambalo unatakiwa kuwa nalo makini sana. Baadhi ya watu wakisikia maonyo, wao hukimbilia kusema ‘hili halinihusu’ , yani kila kitu kinachomgusa yeye anaona kina wahusu watu fulani na sio yeye. Na hata ukigundua ana udhaifu fulani na ukaanza kumuelekeza, anaona kama unamtuhumu na anaanza kukwepa na kuhakikisha hauendelei kuongea, hasa mambo yanayoonekana kuwa binafsi kama mahusiano, lakini ukweli ni kwamba siyo ya binafsi kwa maana madhara yake huenda hadi kwa jamii iayokuzunguka kwa namna moja ua nyingine hata kama sio moja kwa moja.


07. Mtu mwenye mafungamano na ushirikina.
Nikisema hivi mtu anadhani namzungumzia mshirikina wa moja kwa moja. Hapana, huko ni mbali sana, mimi nazungumzia mtu wa kawaida ambaye muda mwingi anawaza kulogwalogwa tu, story zake ni za wahirikina tu, anataka aishi kama jiwe, yaani hata akipata kakipele tu kutokana na baridi, basi anakosa usingizi na kusema kuna mtu amemloga. Anajichagulia mfumo wa uuguaji, yani anampangia Mungu kuwa anataka asiugue ghafla, maana ikitokea tu hivyo kwake yeye tuhuma zake ni kwa wachawi tu, anajisahau kuwa mwili ni kama maua ya miti, hata upepo ukipuliza, lazima utayumba kidogo. Watu wa aina hii mfumo wao wa kufanya maamuzi ni mbovu, kiufupi hata aina ya ushauri wanaotoa huwa sio wa kujiamini na wameweka rehani amani yao kwa mambo yanayofikirika ambayo hawana uhakika nayo. Epuka kuwarithisha watoto hofu ya aina hii kwa maana inawafanya hata wao kuwa washirikina indirectly. Kuna wakati hata madhehebu ya dini hunasa kwenye huu mtego kwa kwa kuwajaza hofu ya kuwaza mapichapicha yasiyo na mashiko kwa mfumo huu.


Kwa leo niishie na hizo tabia chache angalau tupate nafasi ya kutafakari. Kitu cha msingi ni kuwa makini sana unapokuwa karibu na watu wenye tabia hizo, na ikumbukwe wengi hujiona kama wapo sahihi na busara kubwa sana inahitajika wakati wa kuwaelekeza ili wabadilike au hata kupunguza madhara yake kwao binafsi au watu wanaowazunguka. Kama ukiwa na swali au maoni unakaribishwa hapo chini kwa sehemu ya comment. Tafakari njema!
Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman

Asante kwa kusoma blog yangu.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com