I am targeted to change youth's mind set towards positivity.

I am targeted to change youth's mind set towards positivity.
I am targeted to change youth's mind set towards positivity

Monday 18 September 2017

BANDO LA MUNGU HALICHACHI.


Upendo wa Mungu hauna kipimo

Tumsifu Yesu Kristu/Bwana aifiwe/Shalom. Leo tutatafakari sehemu ndogo ya maandiko matakatifu kutoka kitabu cha nabii Isaya ambapo tutaona ukuu wa maneno yenye pumzi ya Mungu hivyo kujenga hoja ya ‘Bando la Mungu kuwa la kudumu, yaani halichachi.’

Tunasoma Isaya 43:1-5
1 Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu.
 2 Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.
 3 Maana mimi ni Bwana, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako.
 4 Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.
 5 Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi.

NOTE: Aliyekuhuluku=Aliyekuumba

Kuna uwezekano mkubwa baada ya kusoma sehemu hiyo ndogo ya maandiko matakatifu, kuna ujumbe fulani mfano wa mwale wa mwanga unapita kwa haraka kichwani mwako. Sasa mimi nitapita na baadhi ya dondoo na kuzipa maelezo kidogo lengo likiwa ni kushirikishana ukuu wa Mungu.
Mungu ni Upendo


  • Usiogope, maana nimekukomboa. Kuna wakati fulani nikawa najiuliza, mbona haijaandikwa usiogope maana NITAKUKOMBOA, bali NIMEKUKOMBOA? Herufi ‘ME’ ni wakati uliopita mtimilifu (past participle), sasa inakuwaje tumeambiwa tusiogope kama suala la ukombozi lilishafanyika? Yani mwanafunzi anakuwaje na hofu wakati kashakabidhiwa mkononi majibu ya mtihanai wake na amefaulu?. Kilichopo hapa ni kwamba bado kuna kundi kubwa la watu (huenda nikawa mmoja wapo) ambao zawadi ya ukombozi iko mikononi mwao, lakini bado wamejawa na hofu na kutumia nguvu nyingi sana kushughulikia mambo madogo na ya kawaida kana kwamba kuna mtu fulani kashikilia maisha yao zaidi ya Mungu. Kumbe Mungu mwenyewe kwa kinywa cha nabii Isaya anatuambia leo tutupilie mbali hiyo hofu na kujivunia ukombozi ambao kwa hiyari yake ameamua kutuzawadia.
  •  Nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Mtu akikuita kwa jina lako ina maana anakufahamu vizuri. Hata wanyama tu wa kufugwa, ukiwaita kwa majina wanakuwa na amani kuwa wewe ndio mchungaji wao na watakuja miguuni pako na kunyenyekea, japo hawana utashi. Nabii Isaya anatukumbusha kuwa Mungu hajaishia kutuita majina tu, bali anatusisitiza kuwa sisi ni mali yake kwa maana hata mpita njia anaweza kukuita jina lako. Kuna wakati tu kwa makusudi tunaziba masikio na kutosikia atuitapo. Kila mara inawezekana dhamira yako ikawa inakutuma kufanya jambo fulani au kukuonya kutofanya jambo fulani lakini  ukatumia nguvu nyingi kupambana na kujikuta hauitii, ina maana unajitengenezea ukuta kati yako na Mungu. Mara nyingi dhamiri huwa ipo sahihi na ndio maana kama mwili unakusukuma kufanya jambo lisilo jema , dhamiri hai hupingana na wewe kwa kuleta ugumu (resistance) katika mjongeo utakaokupeleka huko.
  • Maji mengi na mito havitakugharikisha, moto hautakuteketeza. Katika sehemu hii ya maandiko, majina moto na maji vimetumika kuwakilisha matatizo, mahangaiko na changamoto za kila siku. Kumbuka Biblia haijasema kuwa hautakumbana na huo moto au maji, bali imesema utakumbana navyo lakini havitakudhuru. Kwa lugha rahisi ni kwamba matatizo, changamoto na magumu tutaendelea kukutana nayo lakini hayataweza kutukengeusha na kututoa kwenye msitari wa imani. Yote hayo ni kutokana na upendo wa Mungu usio na kikomo kwetu, hivyo kama shukurani kwa Mungu tuzishinde changamoto kwa kuonesha ustahimilivu na ukomavu wa imani ili Mungu kwayo ajitwalie utukufu.
Mungu anatutetea dhidi ya maovu ili matendo yetu yazidi kuangaza

  • Ulikuwa wa thamani na kuheshimiwa machoni pangu, nimekupenda. Kumbe kupendwa ni zao la kuthaminiwa. Mtu hawezi kukupenda kama hajuwi thamani yako, ‘Value brings love’. Ndivyo ilivyo kwa Mungu, ametupandisha hivi hata kutuita wa thamani na heshima machoni pake, naam ndipo haswaaa anasisitiza kuwa ametupenda. Upendo wa Mungu hauna kipimo kwetu, na ndio maana kuna wakati huwa natafakari ingelikuwa ukifanya kosa na kurudia basi Mungu anachukua roho yako, je ingekuwa ni miaka mingapi tangu nizikwe? Jiulize pia wewe mwenzangu binafsi. Hakika ni wa huruma sana, sawasawa na neno lake katika Zaburi 130:3 Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?
  • Nitatoa watu kwaajili yako na kabila za watu kwaajili yako. Ndio, hili liko wazi na shuhuda kwa watu wengi nikiwemo mimi nisiyestahili. Kuna wakati fulani mambo yanakaba kila upande, inafika kipindi unauona mwisho wako uleeee unakaribia. Ghafla bin vuu anatokea mtu, watu au familia fulani inakuokoa kwenye changamoto au tatizo lako, mwisho wasiku unajiuliza hivi walikuwepo wahitaji wangapi ambao yamewakaba zaidi yangu? Imekuwaje iwe kwangu? Huyu ndio Mungu tunayemuabudu, Mungu wa surprise, Mungu wa kuinua watu pale usipotarajia ili uyaone matendo yake makuu na kushuhudia ukuu wa jina lake. Katika hili, nakukumbusha kuwatembelea wahitaji wa aina zote na kufanya lile uwezalo kwaajili yao.
  •  Usiogope kwa maana mimi ni pamoja nawe. Hapa ndipo penye uhakika wa kuendelea kumuamini na kutembea kifua mbele huku taa yetu ikiwa ni Msalaba wake (Marko 8:34). Ndio kasema mwenyewe kuwa hofu tuididimize huko shimoni, nasi tuwe na uhakika wa uwepo wake kutupigania. Sasa kama baba yako ameshasema ‘usiogope nitakupa unachotaka’, hivi unaanzaje kutapatapa huko kusikojulikana? Tulia ujichotee neema bwerere kutoka kwa mchungaji wako ambaye anakujua kwa jina na sikuzote anapita kwenye mlango wa boma lako.
Usiogope, Mungu yupo kwaajili yako


Hakika bando la Mungu halichachi, tena kwa upekee wake halina kiwango, wewe ni kupiga tu kwa maana umechorwa kwenye viganja vya mikono yake, anajua hofu zako na kila kitu. Basi Mungu awe nasi tunapotafakari matendo yake makuu na ya kuogofya, huku tukijibidiisha kutenda mema kwa wenzetu, unyenyekevu na utii ni baba wa yote. Kama ukiwa na nyongeza au swali unakaribishwa kupitia sehemu ya ku-comment hapo chini, au hata kwa mitandao mingine ya kijamii utakakokuta link ya mada hii. Neema ya Mungu Baba, na upendo wa Yesu Kristu na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nasi sote, sasa na hata milele. Tumsifu Yesu Kristu

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela

Phone: 0763 639 101/ 0679 639 101
Asante kwa kusoma katika blog hii.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

9 comments: