|
Chagua moja, usichanganye, usipotoshe. Mungu hana mshindani. |
Ukiulizwa ushirikina ni nini labda utakuwa na tafsiri (definition)
yako. Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi naweza kusema USHIRIKINA ni imani anayokuwa
mtu kwa nguvu za giza ambayo huchagizwa kwa mafungamano na mizimu, wapiga ramli,
tabiri chonganishi, uchawi, mazindiko na vyote vyenye undugu na hayo.
Naomba tuwekane sawa hapa, neno IMANI ZA KISHIRIKINA haliwahusu tu wanaofanya pekee, bali hata
wanaosadiki, kutetemekea na kuyahusudu hayo ndio maana kuna neno IMANI. Kwa
bahati mbaya baadhi ya Wakristu wanachanganya kati ya ushirikina na kutumia
mitishamba kujitibu. Wapo wakristu wengi ambao wanajitokeza kifua mbele kusema
Mungu anakataza kutumia miti, mbogamboga na matunda kujitibu kama
havijatengenezwa katika maabara na kutolewa hospitali.
Hili ni tatizo kubwa la uelewa ambalo limewafanya baadhi ya watu
hasa vijana kuwa limbukeni kwa kuaminishwa vitu vya kijinga kwa mgongo wa
kuijua Biblia. Ni kweli Biblia imeutaja sana uchawi na ushirikina na imesem
wazi kuwa vitu hivyo havina nguvu tena kwa wale wamuaminio Kristo.
Dawa zote tunazotumia malighafi zake ni miti, mbegu nakadharika,
hivyo nitakubaliana na mtu anayepinga matumizi ya dawa za asili kwa sababu moja
tu nayo ni uhakika wa vipimo kutokana na umri wa mgonjwa na ukubwa wa athari.
Yaani zile 2x3, au 1x 4 ambazo huwa tunaziona zinaandikwa kwenye dawa za hospitali
ni ngumu kuzifuata kwa dawa ya asili hivyo kuna uwezekano mkubwa waa kuzidisha
kipimo (over dose), pia changamoto ya uhifadhi (storage) LAKINI SIO KWAMBA
KUZITUMIA NI USHIRIKINA.
|
Dawa zote tunazotumia ni mazao ya miti, mbegu, matunda na mboga mboga. Tusiwadanganye watu kuwa kutumia miti kujitibu ni dhambi. |
JE UCHAWI UPO?
Ndio, uchawi upo na ni dhambi,
tena haujaanza leo, upo tangu enzi za agano la kale na ulishapigwa marufuku na
Mungu. Tutazame mifano hii michache
Kwani kuasi ni kama dhambi ya UCHAWI, Na ukaidi ni kama
ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa
wewe usiwe mfalme.( 1 Samuel 15:23)
Lakini mambo haya mawili yatakupata katika
dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kitimilifu,
UCHAWI wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno.( Isaiah 47:9)
Nami nitakatilia mbali UCHAWI, usiwe mkononi
mwako; wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana.( Micah 5:12)
Wala nuru ya taa haitamulika ndani yako tena
kabisa; wala sauti ya bwana-arusi na bibi-arusi haitasikiwa ndani yako tena
kabisa; maana hao wafanya biashara wako walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa
mataifa yote walidanganywa kwa UCHAWI wako.(Ufunuo 18:23)
|
Bado kuna kundi kubwa la Wakristo ambao hawataki kuachana na imani za kishirina moja kwa moja. Anamuamini Mungu bado kwa kujifichaficha anaamini juu ya nguzu za ushirikina na kutafuta njia za kujikinga nje ya Mungu |
Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya,
uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, UCHAWI, uadui, ugomvi, wivu,
hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na
hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba
watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.(Galatia 5:19-21)
Mungu
ametuuumba tutawale wanyama na mimea na
tuvitumie vitufae. Kwa taarifa yako afya ndio mtaji mkubwa kuliko chochote.
Kutumia miti, mbegu matunda mbogamboga kwaajili ya kujitubu sio dhambi. Kama
hutaki kukubali hilo basi hata ukienda hospitali na daktari akikuambia ‘uwe
unakula angalau machungwa mawili kwa siku maana yaasaidia moja, mbili tatu’
usikikubali kwa maana nao pia utakuwa ushirikina, unataka hadi chungwa
waligeuze kiwe kidonge kinachoitwa chungwaolokwini ndio utakubali.
Jambo la ajabu kwa sasa ni hofu iliyotawala kwa wakristu kwa
kuogopa habari za kufikirika kuhusu ushirikina na kupandikiza mbegu za hofu kwa
watoto na kujikuta wakiabudu watu badala ya Mungu. Ni kawaida sana siku hizi
kusikia Mkristu ambaye anaumwa kidogo tu na Malaria au magonjwa yakimazingira
au kutokana na uzembe wake kufanya mazoezi au kuishi mazingira machafu, lakini
utamsikia nimerogwa, ni majini haya, oohhh ni wachawi hawa washindwe kwa jina
la Yesu. Heh, jamani mbona ni kituko hiki.
Kuna waraka fulani nilisoma
mtu fulani amewaandikia waumini wa dhehebu lake kuwa ‘Kwenda hospitali au kutumia dawa
za asili vyote ni dhambi kwa maana Mungu anaponya na kwenda hospitali au
kutumia dawa ni kuona kama Mungu hawezi’. Sasa huyu ana utofauti gani
na wapiga lamli? Kwa maana imani yake imekaa kimazingaombwe na upotoshaji, kama
wale waliowahi kusema wanataka kwenda Iraq bila viza wala paspoti, Mungu
atafanya muujiza wa kuwatoa uwanja wa ndege hadi huko waende wakahubiri.
Ni kweli Mungu anaponya, lakini daktari anatibu na ndio maana
tunasali kwaajili ya madaktari wetu na wauguzi wawe na moyo wa huruma na kutoa
huduma safi kwa wagojwa, tena tunamuomba Mungu azibariki dawa ili ziwafae
wagonjwa wetu kwa maana hata kama dawa ni sahihi, Mungu akiamua kuchuka uhai
wake hakuna njia ya kuzuia hilo.
ANGALIZO: Kama mtu atakuambia haya majani ya mti ni dawa ya
kidonda, ukisagasaga na kupaka unapona, lakini uende ukasagie na jiwe
lililookotwa njia panda ya kwenda makaburini, au wakati wa kupaka kiuno kiwe
kimeelekea linakozamia jua,, ooohhh uwe hujasalimiana na mtu yoyote, sijuwi
nini na nini,,,,,,,,,, hapana huo ni ushirikina na uchawi kwa maana kuna
mafungamano na nguvu za giza na sayansi pori ambayo imejificha na haielezeki
vizuri.
Lakini mtu anakuambia pale nje kwenu kuna muarobaini au mlonge na
unatibu kitu fulani, nenda kachume majani au mbegu, changanya na kitunguu
swaumu kidogo na tangawizi na asali kwa mbali halafu unywe bila masharti
yoyote, hivi hapa ushirikina uko wapi???. Tuko busy kuwadidimiza watu kimtazamo
na kuwavuruga uwezo wao wa kufikiria kisa tuataka kuwakusanya na kuwafanya
mtaji. Huo ni ushetani, tusiitumie Biblia kupotosha watu. Najua hofu ya watu
wengi ni kwamba ‘Kama napewa dawa na mtu fulani, je najua ameinenea maneno gani
huko wakati wa kuichimba au kuichuma?’ . Sawa hiyo ni tafakari nzuri, basi kama
hiyo ndio ishu tumia zile ambazo unajichimbia au kujichumia mwenyewe au mtu
unayemuamini.
Lakini kwanza tukubaliane
Mungu hawezi kumpa mtu kila kitu, hivyo hata utambuzi wa mti fulani unatibu
kitu fulani hajampa kila mtu, hivyo ni uamuzi wa huyo mtu kuwaambia wengine au
kuwachumia yeye mwenyewe. Kama ambavyo
leo unaamini (huenda ni kinyume kwako) kwamba ukisaga tangawizi ukachanganya na
asali inatibu kifua, hasa kwa watoto, ujue ilianza kwa mtu mmoja kutambua naye
akawaambia wengine. Nikukumbushe tu, Warumi
14:14 inasema ‘Najua, tena
nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa
asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile
ni najisi.’ Hivyo ukiamini pia ukisema nikila chungwa nitatoka vipele,
vitakutoka kweli kwa maana ndipo imani yako ilipolala.
|
Matibabu ya hospitali ni ya muhimu, sio ya kubeza hata kidogo. Ukisema unamuamini Mungu hivyo hata ukiumwa huendi hospitali kisa Mungu atafanya, basi unajitakia kufa, na utakufa ndio kwa ujinga wako huku unamsingizia Mungu |
*******************************************************************************************
Katika
kusoma kitabu kinachoitwa ‘Busara za
Mzee’ kilichoandikwa na Padre Titus Amigu amesema haya kwenye baadhi ya maeneo ya kitabu
chake;,
Hofu za
kishirikina zinatukwamisha waafrika wengi weusi kupiga hatua za maendeleo ya
kweli. Kuna wengine tunaamini sana katika ushirikina. Wengi tunataabika
kutafuta nguvu na uwezo wa kufanya maajabu huku wengine wakitafuta kinga dhidi
ya ushirikina, wengine tunaogopa laana, nasi tunataabika usiku kutaka kuivunja
ile tunayoiita miti ya familia. Wengine tunaogopa mizimu hivyo kujitaabishaa
kuitambikia ili kuituliza mizimu isije kutudhuru kwenye shughuli zetu za kila
siku.
Jiamini kama
mwana wa Mungu. Ondoa wasiwasi kwani wasiwasi ni chimbuko la magonjwa ya
kisaikomatiki. Mungu amekuumba kwa hiari yake mwenyewe naa ndipo Mungu mwenyewe
anakulinda mwili na roho. Ukijiamini katika ulinzi
wa Mungu unaaweza hata ukanywa sumu nayo isikudhuru.
Usilimbukie habari za majini, usije ukakubali usanii. Uwe mbishi
ukatafute uthibitisho wa ukweli wa vituko vya ajabu unavyosimuliwa.
Usichanganywe. Usikubali elimu yako izimwe hasa elimu ya afya na
elimu ya viumbe. Kuna matukio mengi unaweza kuyachambua kisayansi ukaona ukweli
au uongo wake. Elimu ya Baiolojia inaweza kukuelewesha mengi na ukapunguza
kustaajabu kusiko na sababu ama kudai kupungwa mapepo hata pasipo takiwa.
*******************************************************************************************
Wakristo tupone jamani na haya maigizo ya watu kutuchezea akili na
kujikuta nasisi tunawafundisha watoto uongo na ujinga. Makanisani siku hizi
kumekuwa na kazi mbili tu, kuwapa watu utajiri na kuwapa habari za vitisho vya
ushirikina. Hebu tuangalie maisha ya Yesu kwani alifanya mangapi? Suala la
kuutafuta uzima wa milele siku hizi kwa baadhi ya makanisa halizungumzwi tena,
wao ni kupokea miujiza ya majumba na magari, kuolewa na kuzaa basi. Sijasema
kwamba watu wateseke, hapana, lakini kuna mahala fulani tunachezewa akili.
Unafahamu kuwa kuna magonjwa ya zinaa kama Kisonono mgonjwa
asipotibiwa mapema huweza kuathiri hadi ubongo na mfumo wa fahamu kasha kumfanya
mtu awe kichaa? Bado mtu uko busy kudanganya watu kuwa eti umeongea na Mungu
kakwambia huyu mtu kalogwa na watu wanaomuonea wivu kwasababu ana akili sana na
darasani huko chuoni? Kuna utaofauti gani kati yaw ewe unayeongea haya na mpiga
ramli msituni huko? Huyu Mungu tunayemchezea hakika ni mvumilivu sana, maana
tumefanya machukizo mengi kwa mgongo wa
neno lake huku lengo likiwa kujistawisha sisi na familia zetu kwa kuwakandamiza
wenye matatizo na mahanagaiko ya dunia hii.
Mungu akusaidie, na ubadili
mtazamo wa kufikilia, acha kuwaza kulogwalogwa tu kila saa, matatizo
mengine unayachikonoa wewe mwenyewe, tena ukumbuke wewe sio chuma au jiwe,
chuma chenyewe hupata kutu, sembuse na wewe ambaye Biblia imesema kabisa kuwa
unafanana na maua a mti? Jamani, tusijitafutie shari kwa Mungu wetu ambaye sifa
yake ya kwanza ni huruma na kutukirimia neema zake ili tuweze kuwa salama na
kuitakatifuza dunia hii na kuhudumiana kama wana wa Baba mmoja.
Tumsifu Yesu Kristo.
Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
|
Asante kwa kutembelea blog yangu..Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi
kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata
mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya
kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa
chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira
tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com
|