I am targeted to change youth's mind set towards positivity.

I am targeted to change youth's mind set towards positivity.
I am targeted to change youth's mind set towards positivity

Thursday, 1 June 2017

USHIRIKINA-BAADHI YA WAKRISTO WANAUSUJUDIA

Chagua moja, usichanganye, usipotoshe. Mungu hana mshindani.

Ukiulizwa ushirikina ni nini labda utakuwa na tafsiri (definition) yako. Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi naweza kusema USHIRIKINA ni imani anayokuwa mtu kwa nguvu za giza ambayo huchagizwa kwa mafungamano na mizimu, wapiga ramli, tabiri chonganishi, uchawi, mazindiko na vyote vyenye undugu na hayo.

Naomba tuwekane sawa hapa, neno IMANI ZA KISHIRIKINA haliwahusu tu wanaofanya pekee, bali hata wanaosadiki, kutetemekea na kuyahusudu hayo ndio maana kuna neno IMANI. Kwa bahati mbaya baadhi ya Wakristu wanachanganya kati ya ushirikina na kutumia mitishamba kujitibu. Wapo wakristu wengi ambao wanajitokeza kifua mbele kusema Mungu anakataza kutumia miti, mbogamboga na matunda kujitibu kama havijatengenezwa katika maabara na kutolewa hospitali.

Hili ni tatizo kubwa la uelewa ambalo limewafanya baadhi ya watu hasa vijana kuwa limbukeni kwa kuaminishwa vitu vya kijinga kwa mgongo wa kuijua Biblia. Ni kweli Biblia imeutaja sana uchawi na ushirikina na imesem wazi kuwa vitu hivyo havina nguvu tena kwa wale wamuaminio Kristo.

Dawa zote tunazotumia malighafi zake ni miti, mbegu nakadharika, hivyo nitakubaliana na mtu anayepinga matumizi ya dawa za asili kwa sababu moja tu nayo ni uhakika wa vipimo kutokana na umri wa mgonjwa na ukubwa wa athari. Yaani zile 2x3, au 1x 4 ambazo huwa tunaziona zinaandikwa kwenye dawa za hospitali ni ngumu kuzifuata kwa dawa ya asili hivyo kuna uwezekano mkubwa waa kuzidisha kipimo (over dose), pia changamoto ya uhifadhi (storage) LAKINI SIO KWAMBA KUZITUMIA NI USHIRIKINA.
Dawa zote tunazotumia ni mazao ya miti, mbegu, matunda na mboga mboga. Tusiwadanganye watu kuwa kutumia miti kujitibu ni dhambi.

JE UCHAWI UPO?
Ndio, uchawi upo na ni dhambi, tena haujaanza leo, upo tangu enzi za agano la kale na ulishapigwa marufuku na Mungu. Tutazame mifano hii michache

Kwani kuasi ni kama dhambi ya UCHAWI, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.( 1 Samuel 15:23)

Lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kitimilifu, UCHAWI wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno.( Isaiah 47:9)

Nami nitakatilia mbali UCHAWI, usiwe mkononi mwako; wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana.( Micah 5:12)

Wala nuru ya taa haitamulika ndani yako tena kabisa; wala sauti ya bwana-arusi na bibi-arusi haitasikiwa ndani yako tena kabisa; maana hao wafanya biashara wako walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa UCHAWI wako.(Ufunuo 18:23)
Bado kuna kundi kubwa la Wakristo ambao hawataki kuachana na imani za kishirina moja kwa moja. Anamuamini Mungu bado kwa kujifichaficha anaamini juu ya nguzu za ushirikina na kutafuta njia za kujikinga nje ya Mungu


Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, UCHAWI, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.(Galatia 5:19-21)

Mungu ametuuumba tutawale  wanyama na mimea na tuvitumie vitufae. Kwa taarifa yako afya ndio mtaji mkubwa kuliko chochote. Kutumia miti, mbegu matunda mbogamboga kwaajili ya kujitubu sio dhambi. Kama hutaki kukubali hilo basi hata ukienda hospitali na daktari akikuambia ‘uwe unakula angalau machungwa mawili kwa siku maana yaasaidia moja, mbili tatu’ usikikubali kwa maana nao pia utakuwa ushirikina, unataka hadi chungwa waligeuze kiwe kidonge kinachoitwa chungwaolokwini ndio utakubali.

Jambo la ajabu kwa sasa ni hofu iliyotawala kwa wakristu kwa kuogopa habari za kufikirika kuhusu ushirikina na kupandikiza mbegu za hofu kwa watoto na kujikuta wakiabudu watu badala ya Mungu. Ni kawaida sana siku hizi kusikia Mkristu ambaye anaumwa kidogo tu na Malaria au magonjwa yakimazingira au kutokana na uzembe wake kufanya mazoezi au kuishi mazingira machafu, lakini utamsikia nimerogwa, ni majini haya, oohhh ni wachawi hawa washindwe kwa jina la Yesu. Heh, jamani mbona ni kituko hiki.

 Kuna waraka fulani nilisoma mtu fulani amewaandikia waumini wa dhehebu lake kuwa ‘Kwenda hospitali au kutumia dawa za asili vyote ni dhambi kwa maana Mungu anaponya na kwenda hospitali au kutumia dawa ni kuona kama Mungu hawezi’. Sasa huyu ana utofauti gani na wapiga lamli? Kwa maana imani yake imekaa kimazingaombwe na upotoshaji, kama wale waliowahi kusema wanataka kwenda Iraq bila viza wala paspoti, Mungu atafanya muujiza wa kuwatoa uwanja wa ndege hadi huko waende wakahubiri.

Ni kweli Mungu anaponya, lakini daktari anatibu na ndio maana tunasali kwaajili ya madaktari wetu na wauguzi wawe na moyo wa huruma na kutoa huduma safi kwa wagojwa, tena tunamuomba Mungu azibariki dawa ili ziwafae wagonjwa wetu kwa maana hata kama dawa ni sahihi, Mungu akiamua kuchuka uhai wake hakuna njia ya kuzuia hilo.

ANGALIZO: Kama mtu atakuambia haya majani ya mti ni dawa ya kidonda, ukisagasaga na kupaka unapona, lakini uende ukasagie na jiwe lililookotwa njia panda ya kwenda makaburini, au wakati wa kupaka kiuno kiwe kimeelekea linakozamia jua,, ooohhh uwe hujasalimiana na mtu yoyote, sijuwi nini na nini,,,,,,,,,, hapana huo ni ushirikina na uchawi kwa maana kuna mafungamano na nguvu za giza na sayansi pori ambayo imejificha na haielezeki vizuri.

Lakini mtu anakuambia pale nje kwenu kuna muarobaini au mlonge na unatibu kitu fulani, nenda kachume majani au mbegu, changanya na kitunguu swaumu kidogo na tangawizi na asali kwa mbali halafu unywe bila masharti yoyote, hivi hapa ushirikina uko wapi???. Tuko busy kuwadidimiza watu kimtazamo na kuwavuruga uwezo wao wa kufikiria kisa tuataka kuwakusanya na kuwafanya mtaji. Huo ni ushetani, tusiitumie Biblia kupotosha watu. Najua hofu ya watu wengi ni kwamba ‘Kama napewa dawa na mtu fulani, je najua ameinenea maneno gani huko wakati wa kuichimba au kuichuma?’ . Sawa hiyo ni tafakari nzuri, basi kama hiyo ndio ishu tumia zile ambazo unajichimbia au kujichumia mwenyewe au mtu unayemuamini.

 Lakini kwanza tukubaliane Mungu hawezi kumpa mtu kila kitu, hivyo hata utambuzi wa mti fulani unatibu kitu fulani hajampa kila mtu, hivyo ni uamuzi wa huyo mtu kuwaambia wengine au kuwachumia  yeye mwenyewe. Kama ambavyo leo unaamini (huenda ni kinyume kwako) kwamba ukisaga tangawizi ukachanganya na asali inatibu kifua, hasa kwa watoto, ujue ilianza kwa mtu mmoja kutambua naye akawaambia wengine. Nikukumbushe tu, Warumi 14:14 inasema Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi.’ Hivyo ukiamini  pia ukisema nikila chungwa nitatoka vipele, vitakutoka kweli kwa maana ndipo imani yako ilipolala.
Matibabu ya hospitali ni ya muhimu, sio ya kubeza hata kidogo. Ukisema unamuamini Mungu hivyo hata ukiumwa huendi hospitali kisa Mungu atafanya, basi unajitakia kufa, na utakufa ndio kwa ujinga wako huku unamsingizia Mungu


*******************************************************************************************

Katika kusoma kitabu kinachoitwa ‘Busara za Mzee’ kilichoandikwa na Padre Titus Amigu  amesema haya kwenye baadhi ya maeneo ya kitabu chake;,

Hofu za kishirikina zinatukwamisha waafrika wengi weusi kupiga hatua za maendeleo ya kweli. Kuna wengine tunaamini sana katika ushirikina. Wengi tunataabika kutafuta nguvu na uwezo wa kufanya maajabu huku wengine wakitafuta kinga dhidi ya ushirikina, wengine tunaogopa laana, nasi tunataabika usiku kutaka kuivunja ile tunayoiita miti ya familia. Wengine tunaogopa mizimu hivyo kujitaabishaa kuitambikia ili kuituliza mizimu isije kutudhuru kwenye shughuli zetu za kila siku.

Jiamini kama mwana wa Mungu. Ondoa wasiwasi kwani wasiwasi ni chimbuko la magonjwa ya kisaikomatiki. Mungu amekuumba kwa hiari yake mwenyewe naa ndipo Mungu mwenyewe anakulinda mwili na roho. Ukijiamini katika ulinzi wa Mungu unaaweza hata ukanywa sumu nayo isikudhuru.

Usilimbukie habari za majini, usije ukakubali usanii. Uwe mbishi ukatafute uthibitisho wa ukweli wa vituko vya ajabu unavyosimuliwa.

Usichanganywe. Usikubali elimu yako izimwe hasa elimu ya afya na elimu ya viumbe. Kuna matukio mengi unaweza kuyachambua kisayansi ukaona ukweli au uongo wake. Elimu ya Baiolojia inaweza kukuelewesha mengi na ukapunguza kustaajabu kusiko na sababu ama kudai kupungwa mapepo hata pasipo takiwa.
*******************************************************************************************
Wakristo tupone jamani na haya maigizo ya watu kutuchezea akili na kujikuta nasisi tunawafundisha watoto uongo na ujinga. Makanisani siku hizi kumekuwa na kazi mbili tu, kuwapa watu utajiri na kuwapa habari za vitisho vya ushirikina. Hebu tuangalie maisha ya Yesu kwani alifanya mangapi? Suala la kuutafuta uzima wa milele siku hizi kwa baadhi ya makanisa halizungumzwi tena, wao ni kupokea miujiza ya majumba na magari, kuolewa na kuzaa basi. Sijasema kwamba watu wateseke, hapana, lakini kuna mahala fulani tunachezewa akili.

Unafahamu kuwa kuna magonjwa ya zinaa kama Kisonono mgonjwa asipotibiwa mapema huweza kuathiri hadi ubongo na mfumo wa fahamu kasha kumfanya mtu awe kichaa? Bado mtu uko busy kudanganya watu kuwa eti umeongea na Mungu kakwambia huyu mtu kalogwa na watu wanaomuonea wivu kwasababu ana akili sana na darasani huko chuoni? Kuna utaofauti gani kati yaw ewe unayeongea haya na mpiga ramli msituni huko? Huyu Mungu tunayemchezea hakika ni mvumilivu sana, maana tumefanya machukizo  mengi kwa mgongo wa neno lake huku lengo likiwa kujistawisha sisi na familia zetu kwa kuwakandamiza wenye matatizo na mahanagaiko ya dunia hii.

Mungu akusaidie, na ubadili  mtazamo wa kufikilia, acha kuwaza kulogwalogwa tu kila saa, matatizo mengine unayachikonoa wewe mwenyewe, tena ukumbuke wewe sio chuma au jiwe, chuma chenyewe hupata kutu, sembuse na wewe ambaye Biblia imesema kabisa kuwa unafanana na maua a mti? Jamani, tusijitafutie shari kwa Mungu wetu ambaye sifa yake ya kwanza ni huruma na kutukirimia neema zake ili tuweze kuwa salama na kuitakatifuza dunia hii na kuhudumiana kama wana wa Baba mmoja.
Tumsifu Yesu Kristo.

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Asante kwa kutembelea blog yangu..Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

12 comments: