Mwanaume anayejitambua haoni shida kuomba msamaha |
Salamu. Leo nataka nizungmze na wanaume wenzangu. Hivi
karibuni niliandika tafakari fupi juu ya mapishi na wanawake. Japo sikuweka
huku kwenye blog, kule kule kwenye facebook, instagram na watsup kila mtu
alitoa mtazamo wake, hasa watsup uliibuka mjadala mkali kwenye baadhi ya
makundi ambako nilishirikisha. Na kiukweli lengo langu halikuwa kumaanisha kuwa
mapishi ni ndoa, bali ndoa ni composite function ambayo ndani yake kuna vitu
vingi sana, na lengo ni kuweka vitu vingine vyote sawa (keeping other factors
constant /CETERIS PERIBUS) na kuangalia athali za mke ambaye hapendi au ni
mvivu kupika.
Wakati wa kuchangia mada hiyo, wapo waliosema mbona
umewazungumzia wasichana pekee? Nikaahidi kuja na ugonjwa unaowasumbua wanaume
wengi kama compensation, kwa maana lengo ni kujenga na sio kushushua au
kuhukumu. Sasa nizungumze juu ya suala la wanaume kuona ugumu kuomba msamaha kwa
wanawake pale wanapowakosea. Ni ukweli usiopingika wanaume wengi hudhani wao
kuomba msamaha kwa wanawake ni kujishushia hadhi au kuonesha udhaifu. Wengi
hujitutumua na kuishia kusema ‘POTEZEA TU,
au VUNGA, au YAISHE au KAUSHA’. Sasa sijui nini kinakaushwa hapa, ni
mishikaki au chipsi? Sijuwi mimi.
Kwa haraka mtu anaweza kudhani hii ni kwenye ndoa tu, lakini
hata kwa vijana ambao hawajaoa, inaweza kutokea mkakwaruzana au kukwazana na
msichana yoyote mnayesoma naye au rafiki wa kawaida ambapo wanaume wengi hupata
ukakasi kutamka neno ‘nisamehe dada
yangu, nisamehe rafiki yangu’. Huu ni ujinga, na ujasiri wa hasara kwa
maana haijaandikwa kuwa wanawake tu ndio watakuwa wanakosea. Ni vyema wanaume
kujifunza kuomba msamaha pale unapomkosea mwanamke yoyote ili isikupe shida
hata ukiingia kwenye ndoa na kufanya kosa fulani kwa mkeo, kisha kuanza kuona
ukakasi kuomba msamaha. Ukiulizwa kitu ambacho unajua kabisa umefanya kosa,
unaanza kujitutumua kuonesha hasira na kutengeneza mazingira kuwa kwa wanaume
ni kawaida kufanya hicho kitu, hapana, hiyo sio kweli.
Kuomba msamaha hakukupunguzii kitu. Kwani hujuwi kuwa umekosa ? |
Kwa mwanaume kuomba msamaha kwa mwanamke hakupunguzi uanaume
wako wala kukudisqualify kutoka kwenye nafasi uliyopo, bali ni tendo la
kijasiri na ukomavu kifikra , kimtazamo na maamuzi. Ile amani anayopata
mwanamke baada ya kuombwa msamaha ni baraka kwako. Halafu masikini ya Mungu
wanawake hata hawaoni kazi kusamehe, hasa ukionesha kweli umeelewa kosa. Mara
nyingi kwasababu ya kujiona dhaifu hujikuta wanasamehe hata bila kuombwa msamaha,
sawa hili ni zuri sana kuwa nalo hata kwa wanaume, lakini wakiombwa
msamaha inakuwa jema zaidi.
Hata huko kwenye ndoa mara nyingi baadhi ya dada zetu
walioingia huko wanatushirikisha, utasikia ‘Weee
baba fulani hata akirudi usiku usijaribu kuuliza, atakuwashia moto hadi ujikute
wewe ndio unaomba msamaha kwa kumuuliza, amesema wanaume huwa hawaulizwi’,
mhhh, hii sio sifa njema, sasa kama mnajiita nyie ni mwili mmoja, halafu
unasema usiulizwe, basi na wewe usimuulize kitu. Ni kweli mwanaume ni kichwa
cha nyumba na hilo ni agizo la Mungu mwenyewe, sawa lakini ukimkosea mkeo au
mwanamke yoyote ufahamu kuna ubinadamu, na nafsi yake inafukuta na kujikuta anawaza
mambo mengi ya ajabuajabu ambayo angekufanyia
kama angekuwa na huo uwezo.
Ushauri wangu kwa wanaume wote tujifunze kuomba msamaha kwa
jinsia zote, na sio kwa mwanaume mwenzako tu kisa umeona ana minguvu kuliko
wewe kwamba akiamua anaweza kukugeuzia betri na umeme ukashindwa kuwaka? Mhhh,
hapana. Kama ambavyo inakukereketa mtu aliyekukosea asipoomba msamaha, ndivyo
ilivyo kwa wanawake ukiwakosea na ukatia mgomo kuomba msamaha eti unaogopa
kujishushia heshima, nani kakudanganya? Wewe omba tu msamaha kwa unyenyekevu
wote, utajiongezea heshima kwake na kujitofautisha na wengine wanaochukulia
kila kitu generally bila kuwa na unique behaviours.
Mwingine akijipapatua weee anaamua kuandika kaujumbe kamsamaha na kuweka mezani. Teh,teh, sawa ni jambo jema, lakini jifunze kutamka kwa kinywa chako then suppliment na hayo maandishi mazuri. |
Kwa upande wangu sioni shida kuomba msamaha endapo nitagundua
nimemmkosea mtu wa jinsia yoyote kwa maana hainipunguzii kitu chochote zaidi ya
kuniongezea tu reputability na kutowaza kuwa hivi ananifikiriaje nilipofanya
kosa au kumkwaza bila kuomba msamaha. Wafundisheni watoto wakiume kujua umhimu
wa kuomba msamaha kwa vinywa vyao kwa jinsia zote pale wanapofanya makosa kama
ilivyo kwa watoto wa kike. Hapo tutakuwa tunajenga jamii inayojielewa na
kuifanya jamii kukalika na kuwa na mapatano pasi na kuwa na ubabe na
unyanyasaji kwa watu fulani. Mtu anayeomba msamaha akikosa yupo kwenye nafasi
nzuri ya kushirikishwa mambo mengi mazuri kwa maana anazungukwa na watu wasio
na kinyongo. Usiombe mwanamke akuchukie kisawasawa kisa ulimkwaza na kugoma
kuomba msamaha weeee, huwa wanachefuka hao balaa tupu. Tuwapunguzie mizigo ya
kuwaza mengi, tuwaombe msamaha kila tuwakoseapo. OMBA MSAMAHA KILA UKIFANYA
KOSA BILA KUJALI NI KUBWA AU DOGO. Tafakari njema.
Eng Nguki Herman. M
No comments:
Post a Comment