Suala la kupenda ni suala
mtambuka ambalo wakati fulani watu hutumia nguvu nyingi kujitahidi kutetea
mantiki yake na kujikuta wanaishia kuongea uongo au kuharibu uhalisia. Kwa kawaida
mtu akiulizwa sababu za kumpenda mtu fulani, anaweza kutoa majibu haya au yenye
mlengo huu:
- Kwasababu nayeye ananipenda
- Kwasababu ni mzuri (mrembo/ handsome)
- Kwasababu amewahi kunisaidia nilipokuwa na shida
- Kwasababu anaonekana atakuja kuwa baba/mama bora wa familia
- Kwasababu ana akili sana darasani
- Kwasababu anaonekana mpambanaji sana na anajituma
- Kwasababu ana pesa nyingi sana, nikiwa naye siwezi pata shida
- Kwasababu ni mpole na sio mlevi
- Na mengine mengi
Sawa lakini yote hayo huenda
ukawa ni ushawishi wa kupenda, lakini sio sababu ya kupenda. Kuna utofauti kati
ya sababu ya kufanya kitu na ushawishi wa kufanya kitu. Sababu ni hamu na
muwako wa ndani wa kufanya kitu, kumbe ushawishi ni kitu ambacho kinakufanya
uamini kuwa utakuwa salama baada ya kufanya hicho kitu.
Mfano rahisi. Tamaa ni sababu ya kufanya ngono, lakini matumizi ya kondomu ni kishawishi
cha kufanya ngono. Nadhani hapo umeelewa utofauti kati ya haya maneno mawili
Upendo ni lazima uwafaidie wote , na sio wa kibinafsi |
Sasa sababu mbili kuu za kupenda
ni hizi hapa:
- Ni hitaji la kila kiumbe hai
- Ni amri
KUPENDA KAMA HITAJI
Hili lipo wazi kabisa, hakuna mtu asiyetaka kupendwa. Ndio
hata mimi najisikia raha sana ninapogundua mtu fulani ananipenda. Kuanzia
wazazi wangu, walezi wangu, wanafamilia, walimu na marafiki wa jinsia na kada
zote. Kupendwa kunaleta msisimko wa aina yake na kukufanya uone uko ‘PROTECTED AND SECURED’ kwa sala za wanaokupenda na unaamini muda
wowote ukiwashirikisha jambo wataitikia kwa muitikio chanya (positive response).
Ni wazi mtu kama hakupendi hawezi kukuombea kwa Mungu mafanikio au hata afya
njema. Fuaraha yake ni kuona unaishi kwa wasiwasi, mateso na maumivu au hata
kutoweka kabisa.
Hili halipo tu kwa binadamu, hata mifugo yako nyumbani,
ikigundua unaipenda na kuihudumia, utaona kabisa inaonesha ishara ya
kukufurahia na kila mara urudipo nyumbani lazima irukeruke miguuni pako. Najaribu
kuwaza hata miti na maua ya nyumbani ambayo kila siku unayatunza, kuyamwagilia
na kuyawekea mbolea, laiti yangekuwa na mdomo yangezungumza na kukubali (appreciate)
upendo unaoonesha kwayo.
Ukifahamu hilo ndivyo inavyokuwa
upande wa pili, kama unafurahia kupendwa basi na wewe kuwapenda wengine ni
lazima, kwa maana wanahitaji hilo, na ni la kudumu. Watu wanapata vidonda vya tumbo, presha na
msongo wa mawazo na wengine afya zao kuzorota mara wakigundua hawapendwi au
kutothaminika na watu walio karibuu nao. Ulishajiuliza siku mtu wako wa karibu
akikutamkia ‘SIKUPENDI WEWE, YANI NATAMANI KAMA NISINGEIONA HIYO SURA YAKO’
utajisikiaje? Wakati fulani sio lazima mtu atamke, lakini mambo yake tu yanatoa
picha kuwa hampendi mtu fulani.
Na wapo wengine wako katikati (neutral),
yani yeye anajipenda yeye mwenyewe tu, mweee jamani, sasa si uende baharini
huko utafute kisiwa ukae huko peke yako? Kama unaona hilo ni gumu, tafsiri yake
ni kwamba tunahitajiana na kutegemeana. Unapotembea tu huko nje na kuona watu
wamefurahi, hawana huzuni, hiyo ni dawa pia na fundisho kuwa huwezi
kujifurahisha mwenyewe, ili mtu ucheke, lazima uchekeshwe na mtu mwingine, kama
sio mko uso kwa uso basi hata kwa message tu mnazochati. Kwa lugha rahisi
tujifunze kuwapenda watu pasi na kujali matabaka ya aina fulani
Angalizo: Kwakuwa kupendwa ni
hitaji, wapo wanaotumia mgongo wa uhitaji huo na kupeleka kwa watu upendo nusu
kilo, mateso na maumivu kilo hamsini.
Hiyo ni dhambi kwa maana mpokeaji alijiandaa kuwa aliyemuendea ni mtu mwema
anayefahamu kuwa kupenda na kupendwa ni lazima kati ya mtu na mtu au jamii na
jamii.
Ni rahisi kutamka neno NAKUPENDA, lakini ukweli tunao wenyewe mioyoni |
KUPENDA KAMA AMRI
Upendo ni amri ya Mungu.
Nimejaribu kufuatilia mawaidha ya dini zote, mathalani Wakristu na Waislamu,
wote wameagizwa kupenda, na kwamba kama wasipowapenda binadamu wenzao basi na Mungu
hatawapenda wao. Ahaaaaa, kumbe kama hujui kupenda basi huwezi kuambatana na baraka
za Mungu. Upendo hauhitaji pesa au mazingira maalumu au kuwekewa mikakati kama
bajeti ya kujenga reli ya standard gauge, la hasha! Ukitambua tu kuwa ni amri
ya Mungu , basi ni kujifunza tu kuwa ni sehemu ya maisha yako.
Upendo unaozungumzwa hapa hauna
masharti, vionjo tatanishi na vitenzi vichokozi vyenye mlengo wa kumuinua
shetani. Kwani hujawahi kuona mtu anasema ‘nilimuua mume wangu ili niishi kwa amani na
mtu NINAYEMPENDA’, Sasa huo ni upendo? Hapana, ni ushetani kwa maana
huyu wasasa akibadilika kidogo tu na akaja anayejali zaidi, basi atamuua na
huyu ili afurahie na huyo mwingine. Hivyo ndugu zangu ni bora tukafahamu jambo
hili kinagaubaga ili tusichanganye mambo na kudhani kupenda ni hiari, hapana. KUPENDA
NI LAZIMA, lakini KUHUSIANA NI HIARI YA MTU. Kumpenda mtu sio lazima
muhusiane, au kuzoeana bila mipaka, hapana, tupendane, tushirikiane, lakini
mipaka na heshima iwepo ili kulinda utu wa mtu, misingi ya kijinsia, utamaduni
na uhuru wa kuamua juu ya msatakabali wa maisha ya baadaye ya mtu binafsi. Kama una swali, hoja au maoni, kuwa huru hapo chini eneo la comments. NAWAPENDA WOTE
Eng Nguki Herman. M