Bikira Maria mama wa Mungu, Utuombee |
Tumsifu Yesu
Kristu/Bwana Yesu asifiwe/Shaloom.
Nakusalimu ndugu yangu katika Kristu Yesu mwana wa Mungu ambaye kupitia
yeye tumekuwa wamoja kwa namna fulani. Naomba kukuondoa hofu kama utakuwa ni
mmoja kati ya waliokwanzika na kichwa cha somo hili, kwa maana utakuwa
umejikwaza mwenyewe kwa kujikataa au kuenda kinyume na ukweli. Kuwa mpole na
usome taratibu maelezo yangu , na kama una hoja au kitu cha kupinga basi utatiririka
hapo chini kwenye eneo la ku-comment, namimi bila hiyana nitakuja kukuweka
sawa.
KWANI BIKIRA
MARIA NI NANI?
Biblia takatifu
imedadavua na kukakavua kinagaubaga juu ya mama Maria, fungua kwa muda wako Injili ya Luka kuanzia sura ya
kwanza aya ya 26 na kuendelea. Kwa kifupi Bikira Maria ni mwanamke safi, aliyeteuliwa
na Mungu ili kupitisha nafsi yake ya pili (Yesu Mwokozi), yani kuwa mzazi wa
Yesu Kristu Mungu kweli na mtu kweli. Alijazwa neema, kutunzwa na kulindwa ili abaki
bila doa hata kumbeba mkombozi tumboni mwake.
Kama hiyo haitoshi, hakuishia kumzaa tu mtoto Yesu na kumuacha
akapambane na hali yake, NOOOOOOO, aliendelea kumlinda, kumtunza (kumbuka pale
walipokuwa wanamtafuta roho juujuu Luka 2:43-52), usisahau pale walipomkimbiza
mtoto kwenda Misri ili asiuawe na Herode
(Mathayo 2:12-21) mara anaambiwa maneno ya kumchoma moyo juu ya huyu mtoto
(Luka 2:35) bado akaendelea naye hata katika safari ya mateso hadi msalabani
(Yohana 19:26-27)
Mafundisho
makuu manne (DOGMA) kuhusu Mama Maria
- Maria Mama wa Mungu
- Maria Bikira Daima
- Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
- Maria Mpalizwa Mbinguni
Wapo baadhi ya
watu bila aibu mbele za Mungu wanasema kwao Maria sio kitu, wao wanamuangalia
Kristu pekee kwa maana hakukuwa na ulazima wa Mungu kumtumia Maria na angeweza
kumtumia hata mwanamke yoyote. Hivyo Maria alishamaliza kazi yake na hana
umhimu wowote kwao. Hii ni kufuru mbele za Mungu ambaye ndiye aliyemtakatifuza
huyu mama ili awe chombo kitakatifu kilichombeba mkombozi. Tatizo ni mafundisho
yaliyokaa kimfumo wa kuoteshwa na vionjo vyenye ukakasi na kuwarithisha watoto
uvuguvugu kisa tu hutaki kutafakari.
Maswali
machache ya kujiuliza
- Kama unaamini kuwa Yesu Kristu ni Mungu kweli, nafsi ya pili ya Mungu Baba aliyeshikamana pamoja na Roho Mtakatifu bila kutengana, mbona unapata kigugumizi kusema Maria ni Mama wa Mungu (Yesu)?
- Kama Maria alishamaliza kazi yake ya kumzaa Yesu,na sasa hana umhimu wowote, basi na Yesu alishamaliza kazi yake na sasa hana umhimu wowote?
- Kama hakukukuwa na upekee wa Maria na Mungu angeweza kumtumia mwanamke yoyote, kumbe pia hapakuwa na ulazima wa Mungu kumtumia Yesu kutukomboa na angemtumia mtu yoyote?
Najaribu kuwaza
kwa sauti hasa ninapoona wengi wakifanya mrejeo kwa wateule wengi wa zamani
katika Biblia kama Musa, Elia, Daudi na wengine, lakini likija suala la Bikira
Maria mhhhh, hapo wanaona mapichapicha. Wengi ukiwadodosa wanajing’atang’ata tu
na kuishia kusema yeye anaangalia wokovu tu ulioletwa na Yesu, hataki kujua
kuwa huyu Yesu hadi kutujia kuna watu ambao Mungu aliamua kushirikiana nao
kujimwilisha (incarnation) ili tumuone na kumpokea katika umbo la kibinadamu.
Kazi ya Bikira Maria ilitabiriwa tangu agano la kale huko Isaya 7:14 na kuelezewa matokeo yake katika agano
jipya.
Angalau siku
hizi kuna baadhi ya watu wa madhehebu yasiyo ya Kikatoliki wameanza kustuka na
kujua kuwa walikuwa wanafanya makosa kutomheshimu mama wa Mkombozi wao hivyo
kwa mbaliiiii wameanza kumtaja taja na kumheshimu, japo kwasababu ya kukosa
msaada wa mafundisho au kuogopa wachungaji wao, basi wanashindwa kupata mang’amuzi
ya hali ya juu na kujizolea neema kutokana na maombezi ya Mama huyu kwa mwanaye
Yesu. Wapo ambao taratibu wameanza kusali Sala ya Salamu Maria na hata Rozali
japo wanakuwa waoga kutokana na upande waliopo kutopigia chapuo sala hizi zenye
nguvu ya kimungu ndani yake. Yeye mwenyewe kasema 'vizazi vyote tutamuita mbarikiwa' (Luka 1:48), sasa asijejua hili ni kizazi cha sayari gani?
Bikira Maria, Mama wa Amani, Utuombee |
KUABUDU Vs
KUHESHIMU.
Anayepaswa
kuabudiwa ni mmoja tu (Kumbukumbu la Torati 5:7), naye ni Mungu muumba mbingu na
nchi. Kuna watu pia wanapata ukakasi na kuwalishaa watoto wao matango poli kwa
kusema wakatoliki wanamuabudu Bikira Maria, la hasha! Sio kweli, wao wanamuheshimu
tu, tena heshima hiyo hatujakurupuka tu kumpa, bali ni Mungu kwanza ndiye
aliyemuheshimu na kumkinga na doa la aina yoyote ili afanyike chombo cha kubeba
nafsi yake kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Sasa jamani kama Mungu mwenyewe
kamheshimu na kumpandisha hivi, sisi ni akina nani hata tumdharau? Ndio maana
nimesema mtu asiyetambua nafasi ya Bikira Maria katika kuletwa kwa ukombozi
huyo sio Mkristo bali anaigiza kuwa Mkristo.
Bikira Maria
ameshatokea mara kadhaa duniani hapa na ushahidi wa wazi kabisa upo. Maeneo
kama Fatima, Lurdi Ufaransa, Kibeho Rwanda n.k yanatoa fundisho kwa dunia juu
ya kumheshimu huyu mama. Hakuna mtu aliyewahi kupinga matokeo haya kwa maana ni
matokeo ya wazi kabisa ambapo ni Mungu yule yule aliyemteua awe mama wa mwokozi
anathibitisha kuwa uteule wake u hai hata leo huko mbinguni na duniani.
Bikira Maria ,kikao cha hekima, Utuombee |
Kama unavyopata
ujasiri wa kumwambia binadamu mwenzako akuombee kwa Mungu, sasa nakushauri
utumie nafasi hii adimu kumwambia Mama Bikira Maria ambaye yuko Mbinguni uso
kwa uso na Mungu akuombee kwa Mungu na mwanaye Yesu Kristu naye atafanya hivyo.
Wewe omba kwa imani na matokeo utayaona.
TUOMBE:
Ee Mungu mwema,
Baba wa Mataifa yote, kwa wema wako uliamua kumteua Mama Bikira Maria awe mama
wa Mkombozi wetu Yesu Kristu, tunakuomba uturehemu na kutusamehe pale
tunapokengeuka na kudharau heshima hiyo kubwa uliyompa mama huyu. Tena tunaomba
msamaha na kwa mwanaye Yesu Kristu ambaye kabla ya kushuka duniani alikuwa
kashikamana nawe kama nafsi yako, hivyo alishiriki kumteua mama Bikira Maria
ili atusamehe na kutustahilisha baraka zako. Tena tunaomba msamaha na kwa Roho
Mtakatifu ambaye mara kadhaa tumejigamba kujazwa naye kumbe ni vionjo vya
kibinadamu na viini macho, na ndani mwetu tumejaa maasi hata kumdharau mama wa
mkombozi. Nawe Maria Mtakatifu mama wa Mungu, utuombee kwa Mungu ili sala zetu
ambazo mara kadhaa zinakwamishwa na maovu yetu ziweze kupokelewa, nasi kwa
unyenyekevu tunaahidi kukuheshimu na kuthamini kazi yako ya kushirikiana na
Mungu kutuletea Yesu, Bwana na Mwokozi wetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu
Kristu, anayeishi na kutawala pamoja na
Baba, Mungu daima na milele. Amina
Eng Nguki Herman. M
No comments:
Post a Comment