I am targeted to change youth's mind set towards positivity.

I am targeted to change youth's mind set towards positivity.
I am targeted to change youth's mind set towards positivity

Monday 11 September 2017

KUWA MAKINI NA WATU HAWA. NI HATARI

Masikio yako yachuje kila unaloambiwa kabla ya kuchukua hatua.

Leo ni siku ya kutafakari baadhi ya aina ya watu ambao tunatakiwa kuwa nao makini sana hasa wale wenye nafasi ya kuweza kubadilisha mawazo yako. Kuna kundi la watu huenda wapo kwako kama marafiki maalumu sana kama ambavyo kilatini wanaitwa familiaritas au confidential friendship kwa kingereza. Hawa ukiwashirikisha mipango yako, na ikatokea wakakupatia marekebisho au mapendekezo lazima kuna uwezekano wa zaidi ya 70% kuyakubali.

Sasa nikupe orodha ya baadhi ya watu ambao inabidi unatakiwa kujua hawafai kuwaamini na wanaweza kukupeleka porini na kukwamisha mipango yako:

01.  Mtu anayeona yeye ni bora kuliko wengine wote:
Hapa lazima tuwekane sawa tafadhari. Point hii hailengi kumfanya mtu ajione dhaifu, la hasha!. Hapa nalenga mtu ambaye katika mazungumzo yake yote hufanya marejeo ya udhaifu wa wengine ukilinganisha na uimara wake. Mfano ukiona mtu kwenye mazunumzo yake kauli kama ‘Usinifananishe mimi na fulani, mimi nina uwezo zaidi/ unapoteza muda kuwa na fulani, mimi ndio ninauwezo wa kukuhudumia/ umempendea nini yule? Ona mimi nina x,y,z ambazo yule hana uwezo wa kuwa nazo/ Mimi ni mzuri sana, siendani na wewe, au unaniona kama fulani, mimi ni msomi kuliko fulani, mimi nina akili kuliko fulani’ hazikosekani basi ujue mtu huyu kuna uwezekano mkubwa wa kukupoteza au kutokuwa na mchango chanya kwenye ushauri wake, na pia wengi ni waongo.

02.Mtu anayejihami bila sababu (Defensive people).
 Hii ni aina ya watu ambao wao huwa wanajitanguliza kuona wapo sahihi kabla hujaanza kuhoji utendaji wao. Kwa mfano ukiona mtu unamwambia; ‘hapo umekosea’ halafu yeye anajibu ; ‘unadhani nilifanya makusudi? Sasa unadhani kwa mazingira haya ningefanyeje? Hata ungekuwa wewe ungefanya hivihivi’. Mtu kama huyu kufanya marakebisho baada ya kukosea huwa ni mgumu sana. Unatakiwa kuwa naye makini sana, na kama ni mwanafamilia (mke/mume) itakuwa vyema ukimtambua kwenye kipengere hiki, vinginevyo unaweza kuwa unaumia moyo kila siku na wakati mwingine kukosa amani ndani ya moyo wako.

03.Mtu anayelazimisha wote kuamini njia yake ya mafanikio ndio pekee ya kufuata
Hapa ndio kwenye shida zaidi, na watoto wadogo ndio walio kwenye hatari kubwa sana ya kuambukizwa huu ugonjwa. Kwa mfano, wapo watu ambao wamefanikiwa nje ya mfumo wa taaluma, sio kwasababu waliamua tu kuelekea huko, bali kuna mazingira yaliwatoa kwenye taaluma na kujikuta wanafanikiwa kutumia vipaji binafsi au kusaidiwa na watu wa karibu walio na msingi bora kwa kifedha. Watu wa aina hii baadhi yao hujikuta wanawaweka njiapanda walio kwenye taaluma kwa kuwaambia kuwa wanapoteza muda huko na hawatafanikiwa, na afadhari wajiunge nao nje ya mfumo wa taaluma kitu ambacho ni hatari sana kwa maana sio kila mtu anaweza kufanya kila kitu katika mazingira yote. Wapo pia ambao kwasababu wamefanikiwa kwa njia ya taaluma, basi wanawavuruga vichwa wale wanaopambana nje ya taaluma na kujikuta hawaweki bidii huko waliko. Huu ni upotoshaji, acha kila mtu afuate njia ambayo Mungu amempangia, kikubwa iwe sahihi na yenye kukubalika. Watie moyo watu kule waliko, sio lazima wote uwalazimishe kufanya kama wewe, na mambo yakiwachachia huko, utaanza kuwacheka tena kwa kuwaambia wanazembea au hawakusikilizi vizuri.
Kazi kwako, utamsikiliza yupi na uache yupi
.
04. Mtu anayesifia uovu kama njia ya kawaida ya maisha.
Vijana wengi tupo kwenye huu mtego wa kushawishiana. Kwa mfano mtu anajisifia uhodari wake wa kuwa na mahusiano holela kwa siri, udanganyifu, wizi, matusi, kutoheshimu wazazi au walezi, unyanyasaji katika mahusiano au katika mazingira yoyote. Ukiona katika mazungumzo yake mtu haoni aibu kujisifia katika mambo haya huyo ni hatari katika mustakabali na ustawi wa jamii yoyote ile, na haaminiki kwa lolote kwa maana dhamiri yake imesheheni dumuzi na uso usio na huruma kwa wanaoteseka kwa matokeo ya maamuzi yake.

05. Mtu asiye na ratiba. 
Hora argentum’; ni msemo wa kilatini unaofanana na ule wa kiingereza ‘time is money’ ikiwa na maana muda ni pesa/mali. Mtu ambaye hana mpango mkakati wa kuhakikisha anafanya jambo fulani kwa muda fulani mambo yake kamwe hayawezi kwenda. Ukiona mtu yupo tayari kwenda mahali popote anapoambiwa aende kwa muda wowote huyo hana ratiba , hafahamu namna ya kufanya kwanza jambo la kwanza. Yaani kuna watu rafiki yake akimwambia waende mjini anakubali bila kuhoji anaenda kufanya nini na je lilikuwa kwenye ratiba yake? Wakiwa njiani akipigiwa simu na  rafiki yake mwingine kuwa waende porini anakubali, hehhh, jamani, yani ikifika jioni yuko hoi na hakuna hata moja la kujivunia alilofanya katika ratiba yake. Kiukweli mtu asiyejari muda mimi huwa hazipandi kabisa. Lazima tufahamu kuwa muda ni rasilimali ya kipekee ambayo ni kama haionekani (invisible resource) lakini ikipotea hairudi tena, hivyo mtu asiye na ratiba unatakiwa kuwa naye makini sana ili usije ungana naye kuelekea shimoni.

06. Mtu asiyetaka kurekebishwa/asiyefundishika.
 Hili ni kundi jingine ambalo unatakiwa kuwa nalo makini sana. Baadhi ya watu wakisikia maonyo, wao hukimbilia kusema ‘hili halinihusu’ , yani kila kitu kinachomgusa yeye anaona kina wahusu watu fulani na sio yeye. Na hata ukigundua ana udhaifu fulani na ukaanza kumuelekeza, anaona kama unamtuhumu na anaanza kukwepa na kuhakikisha hauendelei kuongea, hasa mambo yanayoonekana kuwa binafsi kama mahusiano, lakini ukweli ni kwamba siyo ya binafsi kwa maana madhara yake huenda hadi kwa jamii iayokuzunguka kwa namna moja ua nyingine hata kama sio moja kwa moja.


07. Mtu mwenye mafungamano na ushirikina.
Nikisema hivi mtu anadhani namzungumzia mshirikina wa moja kwa moja. Hapana, huko ni mbali sana, mimi nazungumzia mtu wa kawaida ambaye muda mwingi anawaza kulogwalogwa tu, story zake ni za wahirikina tu, anataka aishi kama jiwe, yaani hata akipata kakipele tu kutokana na baridi, basi anakosa usingizi na kusema kuna mtu amemloga. Anajichagulia mfumo wa uuguaji, yani anampangia Mungu kuwa anataka asiugue ghafla, maana ikitokea tu hivyo kwake yeye tuhuma zake ni kwa wachawi tu, anajisahau kuwa mwili ni kama maua ya miti, hata upepo ukipuliza, lazima utayumba kidogo. Watu wa aina hii mfumo wao wa kufanya maamuzi ni mbovu, kiufupi hata aina ya ushauri wanaotoa huwa sio wa kujiamini na wameweka rehani amani yao kwa mambo yanayofikirika ambayo hawana uhakika nayo. Epuka kuwarithisha watoto hofu ya aina hii kwa maana inawafanya hata wao kuwa washirikina indirectly. Kuna wakati hata madhehebu ya dini hunasa kwenye huu mtego kwa kwa kuwajaza hofu ya kuwaza mapichapicha yasiyo na mashiko kwa mfumo huu.


Kwa leo niishie na hizo tabia chache angalau tupate nafasi ya kutafakari. Kitu cha msingi ni kuwa makini sana unapokuwa karibu na watu wenye tabia hizo, na ikumbukwe wengi hujiona kama wapo sahihi na busara kubwa sana inahitajika wakati wa kuwaelekeza ili wabadilike au hata kupunguza madhara yake kwao binafsi au watu wanaowazunguka. Kama ukiwa na swali au maoni unakaribishwa hapo chini kwa sehemu ya comment. Tafakari njema!

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Phone: 0763 639 101/ 0679 639 101

Asante kwa kusoma blog yangu.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

16 comments: