Wednesday, 28 June 2017

MWANAUME, KUMUOMBA MSAMAHA MWANAMKE NI HESHIMA.

Mwanaume anayejitambua haoni shida kuomba msamaha

Salamu. Leo nataka nizungmze na wanaume wenzangu. Hivi karibuni niliandika tafakari fupi juu ya mapishi na wanawake. Japo sikuweka huku kwenye blog, kule kule kwenye facebook, instagram na watsup kila mtu alitoa mtazamo wake, hasa watsup uliibuka mjadala mkali kwenye baadhi ya makundi ambako nilishirikisha. Na kiukweli lengo langu halikuwa kumaanisha kuwa mapishi ni ndoa, bali ndoa ni composite function ambayo ndani yake kuna vitu vingi sana, na lengo ni kuweka vitu vingine vyote sawa (keeping other factors constant /CETERIS PERIBUS) na kuangalia athali za mke ambaye hapendi au ni mvivu kupika.

Wakati wa kuchangia mada hiyo, wapo waliosema mbona umewazungumzia wasichana pekee? Nikaahidi kuja na ugonjwa unaowasumbua wanaume wengi kama compensation, kwa maana lengo ni kujenga na sio kushushua au kuhukumu. Sasa nizungumze juu ya suala la wanaume kuona ugumu kuomba msamaha kwa wanawake pale wanapowakosea. Ni ukweli usiopingika wanaume wengi hudhani wao kuomba msamaha kwa wanawake ni kujishushia hadhi au kuonesha udhaifu. Wengi hujitutumua na kuishia kusema ‘POTEZEA TU, au VUNGA, au YAISHE au KAUSHA’. Sasa sijui nini kinakaushwa hapa, ni mishikaki au chipsi? Sijuwi mimi.

Kwa haraka mtu anaweza kudhani hii ni kwenye ndoa tu, lakini hata kwa vijana ambao hawajaoa, inaweza kutokea mkakwaruzana au kukwazana na msichana yoyote mnayesoma naye au rafiki wa kawaida ambapo wanaume wengi hupata ukakasi kutamka neno ‘nisamehe dada yangu, nisamehe rafiki yangu’. Huu ni ujinga, na ujasiri wa hasara kwa maana haijaandikwa kuwa wanawake tu ndio watakuwa wanakosea. Ni vyema wanaume kujifunza kuomba msamaha pale unapomkosea mwanamke yoyote ili isikupe shida hata ukiingia kwenye ndoa na kufanya kosa fulani kwa mkeo, kisha kuanza kuona ukakasi kuomba msamaha. Ukiulizwa kitu ambacho unajua kabisa umefanya kosa, unaanza kujitutumua kuonesha hasira na kutengeneza mazingira kuwa kwa wanaume ni kawaida kufanya hicho kitu, hapana, hiyo sio kweli.
Kuomba msamaha hakukupunguzii kitu. Kwani hujuwi kuwa umekosa ?

Kwa mwanaume kuomba msamaha kwa mwanamke hakupunguzi uanaume wako wala kukudisqualify kutoka kwenye nafasi uliyopo, bali ni tendo la kijasiri na ukomavu kifikra , kimtazamo na maamuzi. Ile amani anayopata mwanamke baada ya kuombwa msamaha ni baraka kwako. Halafu masikini ya Mungu wanawake hata hawaoni kazi kusamehe, hasa ukionesha kweli umeelewa kosa. Mara nyingi kwasababu ya kujiona dhaifu hujikuta wanasamehe hata bila kuombwa msamaha, sawa hili ni zuri sana kuwa nalo hata kwa wanaume, lakini wakiombwa msamaha  inakuwa jema zaidi.

Hata huko kwenye ndoa mara nyingi baadhi ya dada zetu walioingia huko wanatushirikisha, utasikia ‘Weee baba fulani hata akirudi usiku usijaribu kuuliza, atakuwashia moto hadi ujikute wewe ndio unaomba msamaha kwa kumuuliza, amesema wanaume huwa hawaulizwi’, mhhh, hii sio sifa njema, sasa kama mnajiita nyie ni mwili mmoja, halafu unasema usiulizwe, basi na wewe usimuulize kitu. Ni kweli mwanaume ni kichwa cha nyumba na hilo ni agizo la Mungu mwenyewe, sawa lakini ukimkosea mkeo au mwanamke yoyote ufahamu kuna ubinadamu, na nafsi yake inafukuta na kujikuta anawaza  mambo mengi ya ajabuajabu ambayo angekufanyia kama angekuwa na huo uwezo.

Ushauri wangu kwa wanaume wote tujifunze kuomba msamaha kwa jinsia zote, na sio kwa mwanaume mwenzako tu kisa umeona ana minguvu kuliko wewe kwamba akiamua anaweza kukugeuzia betri na umeme ukashindwa kuwaka? Mhhh, hapana. Kama ambavyo inakukereketa mtu aliyekukosea asipoomba msamaha, ndivyo ilivyo kwa wanawake ukiwakosea na ukatia mgomo kuomba msamaha eti unaogopa kujishushia heshima, nani kakudanganya? Wewe omba tu msamaha kwa unyenyekevu wote, utajiongezea heshima kwake na kujitofautisha na wengine wanaochukulia kila kitu generally bila kuwa na unique behaviours.
Mwingine akijipapatua weee anaamua kuandika kaujumbe kamsamaha na kuweka mezani. Teh,teh, sawa ni jambo jema, lakini jifunze kutamka kwa kinywa chako then suppliment na hayo maandishi mazuri.

Kwa upande wangu sioni shida kuomba msamaha endapo nitagundua nimemmkosea mtu wa jinsia yoyote kwa maana hainipunguzii kitu chochote zaidi ya kuniongezea tu reputability na kutowaza kuwa hivi ananifikiriaje nilipofanya kosa au kumkwaza bila kuomba msamaha. Wafundisheni watoto wakiume kujua umhimu wa kuomba msamaha kwa vinywa vyao kwa jinsia zote pale wanapofanya makosa kama ilivyo kwa watoto wa kike. Hapo tutakuwa tunajenga jamii inayojielewa na kuifanya jamii kukalika na kuwa na mapatano pasi na kuwa na ubabe na unyanyasaji kwa watu fulani. Mtu anayeomba msamaha akikosa yupo kwenye nafasi nzuri ya kushirikishwa mambo mengi mazuri kwa maana anazungukwa na watu wasio na kinyongo. Usiombe mwanamke akuchukie kisawasawa kisa ulimkwaza na kugoma kuomba msamaha weeee, huwa wanachefuka hao balaa tupu. Tuwapunguzie mizigo ya kuwaza mengi, tuwaombe msamaha kila tuwakoseapo. OMBA MSAMAHA KILA UKIFANYA KOSA BILA KUJALI NI KUBWA AU DOGO. Tafakari njema.

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

Thursday, 1 June 2017

USHIRIKINA-BAADHI YA WAKRISTO WANAUSUJUDIA

Chagua moja, usichanganye, usipotoshe. Mungu hana mshindani.

Ukiulizwa ushirikina ni nini labda utakuwa na tafsiri (definition) yako. Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi naweza kusema USHIRIKINA ni imani anayokuwa mtu kwa nguvu za giza ambayo huchagizwa kwa mafungamano na mizimu, wapiga ramli, tabiri chonganishi, uchawi, mazindiko na vyote vyenye undugu na hayo.

Naomba tuwekane sawa hapa, neno IMANI ZA KISHIRIKINA haliwahusu tu wanaofanya pekee, bali hata wanaosadiki, kutetemekea na kuyahusudu hayo ndio maana kuna neno IMANI. Kwa bahati mbaya baadhi ya Wakristu wanachanganya kati ya ushirikina na kutumia mitishamba kujitibu. Wapo wakristu wengi ambao wanajitokeza kifua mbele kusema Mungu anakataza kutumia miti, mbogamboga na matunda kujitibu kama havijatengenezwa katika maabara na kutolewa hospitali.

Hili ni tatizo kubwa la uelewa ambalo limewafanya baadhi ya watu hasa vijana kuwa limbukeni kwa kuaminishwa vitu vya kijinga kwa mgongo wa kuijua Biblia. Ni kweli Biblia imeutaja sana uchawi na ushirikina na imesem wazi kuwa vitu hivyo havina nguvu tena kwa wale wamuaminio Kristo.

Dawa zote tunazotumia malighafi zake ni miti, mbegu nakadharika, hivyo nitakubaliana na mtu anayepinga matumizi ya dawa za asili kwa sababu moja tu nayo ni uhakika wa vipimo kutokana na umri wa mgonjwa na ukubwa wa athari. Yaani zile 2x3, au 1x 4 ambazo huwa tunaziona zinaandikwa kwenye dawa za hospitali ni ngumu kuzifuata kwa dawa ya asili hivyo kuna uwezekano mkubwa waa kuzidisha kipimo (over dose), pia changamoto ya uhifadhi (storage) LAKINI SIO KWAMBA KUZITUMIA NI USHIRIKINA.
Dawa zote tunazotumia ni mazao ya miti, mbegu, matunda na mboga mboga. Tusiwadanganye watu kuwa kutumia miti kujitibu ni dhambi.

JE UCHAWI UPO?
Ndio, uchawi upo na ni dhambi, tena haujaanza leo, upo tangu enzi za agano la kale na ulishapigwa marufuku na Mungu. Tutazame mifano hii michache

Kwani kuasi ni kama dhambi ya UCHAWI, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.( 1 Samuel 15:23)

Lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kitimilifu, UCHAWI wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno.( Isaiah 47:9)

Nami nitakatilia mbali UCHAWI, usiwe mkononi mwako; wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana.( Micah 5:12)

Wala nuru ya taa haitamulika ndani yako tena kabisa; wala sauti ya bwana-arusi na bibi-arusi haitasikiwa ndani yako tena kabisa; maana hao wafanya biashara wako walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa UCHAWI wako.(Ufunuo 18:23)
Bado kuna kundi kubwa la Wakristo ambao hawataki kuachana na imani za kishirina moja kwa moja. Anamuamini Mungu bado kwa kujifichaficha anaamini juu ya nguzu za ushirikina na kutafuta njia za kujikinga nje ya Mungu


Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, UCHAWI, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.(Galatia 5:19-21)

Mungu ametuuumba tutawale  wanyama na mimea na tuvitumie vitufae. Kwa taarifa yako afya ndio mtaji mkubwa kuliko chochote. Kutumia miti, mbegu matunda mbogamboga kwaajili ya kujitubu sio dhambi. Kama hutaki kukubali hilo basi hata ukienda hospitali na daktari akikuambia ‘uwe unakula angalau machungwa mawili kwa siku maana yaasaidia moja, mbili tatu’ usikikubali kwa maana nao pia utakuwa ushirikina, unataka hadi chungwa waligeuze kiwe kidonge kinachoitwa chungwaolokwini ndio utakubali.

Jambo la ajabu kwa sasa ni hofu iliyotawala kwa wakristu kwa kuogopa habari za kufikirika kuhusu ushirikina na kupandikiza mbegu za hofu kwa watoto na kujikuta wakiabudu watu badala ya Mungu. Ni kawaida sana siku hizi kusikia Mkristu ambaye anaumwa kidogo tu na Malaria au magonjwa yakimazingira au kutokana na uzembe wake kufanya mazoezi au kuishi mazingira machafu, lakini utamsikia nimerogwa, ni majini haya, oohhh ni wachawi hawa washindwe kwa jina la Yesu. Heh, jamani mbona ni kituko hiki.

 Kuna waraka fulani nilisoma mtu fulani amewaandikia waumini wa dhehebu lake kuwa ‘Kwenda hospitali au kutumia dawa za asili vyote ni dhambi kwa maana Mungu anaponya na kwenda hospitali au kutumia dawa ni kuona kama Mungu hawezi’. Sasa huyu ana utofauti gani na wapiga lamli? Kwa maana imani yake imekaa kimazingaombwe na upotoshaji, kama wale waliowahi kusema wanataka kwenda Iraq bila viza wala paspoti, Mungu atafanya muujiza wa kuwatoa uwanja wa ndege hadi huko waende wakahubiri.

Ni kweli Mungu anaponya, lakini daktari anatibu na ndio maana tunasali kwaajili ya madaktari wetu na wauguzi wawe na moyo wa huruma na kutoa huduma safi kwa wagojwa, tena tunamuomba Mungu azibariki dawa ili ziwafae wagonjwa wetu kwa maana hata kama dawa ni sahihi, Mungu akiamua kuchuka uhai wake hakuna njia ya kuzuia hilo.

ANGALIZO: Kama mtu atakuambia haya majani ya mti ni dawa ya kidonda, ukisagasaga na kupaka unapona, lakini uende ukasagie na jiwe lililookotwa njia panda ya kwenda makaburini, au wakati wa kupaka kiuno kiwe kimeelekea linakozamia jua,, ooohhh uwe hujasalimiana na mtu yoyote, sijuwi nini na nini,,,,,,,,,, hapana huo ni ushirikina na uchawi kwa maana kuna mafungamano na nguvu za giza na sayansi pori ambayo imejificha na haielezeki vizuri.

Lakini mtu anakuambia pale nje kwenu kuna muarobaini au mlonge na unatibu kitu fulani, nenda kachume majani au mbegu, changanya na kitunguu swaumu kidogo na tangawizi na asali kwa mbali halafu unywe bila masharti yoyote, hivi hapa ushirikina uko wapi???. Tuko busy kuwadidimiza watu kimtazamo na kuwavuruga uwezo wao wa kufikiria kisa tuataka kuwakusanya na kuwafanya mtaji. Huo ni ushetani, tusiitumie Biblia kupotosha watu. Najua hofu ya watu wengi ni kwamba ‘Kama napewa dawa na mtu fulani, je najua ameinenea maneno gani huko wakati wa kuichimba au kuichuma?’ . Sawa hiyo ni tafakari nzuri, basi kama hiyo ndio ishu tumia zile ambazo unajichimbia au kujichumia mwenyewe au mtu unayemuamini.

 Lakini kwanza tukubaliane Mungu hawezi kumpa mtu kila kitu, hivyo hata utambuzi wa mti fulani unatibu kitu fulani hajampa kila mtu, hivyo ni uamuzi wa huyo mtu kuwaambia wengine au kuwachumia  yeye mwenyewe. Kama ambavyo leo unaamini (huenda ni kinyume kwako) kwamba ukisaga tangawizi ukachanganya na asali inatibu kifua, hasa kwa watoto, ujue ilianza kwa mtu mmoja kutambua naye akawaambia wengine. Nikukumbushe tu, Warumi 14:14 inasema Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi.’ Hivyo ukiamini  pia ukisema nikila chungwa nitatoka vipele, vitakutoka kweli kwa maana ndipo imani yako ilipolala.
Matibabu ya hospitali ni ya muhimu, sio ya kubeza hata kidogo. Ukisema unamuamini Mungu hivyo hata ukiumwa huendi hospitali kisa Mungu atafanya, basi unajitakia kufa, na utakufa ndio kwa ujinga wako huku unamsingizia Mungu


*******************************************************************************************

Katika kusoma kitabu kinachoitwa ‘Busara za Mzee’ kilichoandikwa na Padre Titus Amigu  amesema haya kwenye baadhi ya maeneo ya kitabu chake;,

Hofu za kishirikina zinatukwamisha waafrika wengi weusi kupiga hatua za maendeleo ya kweli. Kuna wengine tunaamini sana katika ushirikina. Wengi tunataabika kutafuta nguvu na uwezo wa kufanya maajabu huku wengine wakitafuta kinga dhidi ya ushirikina, wengine tunaogopa laana, nasi tunataabika usiku kutaka kuivunja ile tunayoiita miti ya familia. Wengine tunaogopa mizimu hivyo kujitaabishaa kuitambikia ili kuituliza mizimu isije kutudhuru kwenye shughuli zetu za kila siku.

Jiamini kama mwana wa Mungu. Ondoa wasiwasi kwani wasiwasi ni chimbuko la magonjwa ya kisaikomatiki. Mungu amekuumba kwa hiari yake mwenyewe naa ndipo Mungu mwenyewe anakulinda mwili na roho. Ukijiamini katika ulinzi wa Mungu unaaweza hata ukanywa sumu nayo isikudhuru.

Usilimbukie habari za majini, usije ukakubali usanii. Uwe mbishi ukatafute uthibitisho wa ukweli wa vituko vya ajabu unavyosimuliwa.

Usichanganywe. Usikubali elimu yako izimwe hasa elimu ya afya na elimu ya viumbe. Kuna matukio mengi unaweza kuyachambua kisayansi ukaona ukweli au uongo wake. Elimu ya Baiolojia inaweza kukuelewesha mengi na ukapunguza kustaajabu kusiko na sababu ama kudai kupungwa mapepo hata pasipo takiwa.
*******************************************************************************************
Wakristo tupone jamani na haya maigizo ya watu kutuchezea akili na kujikuta nasisi tunawafundisha watoto uongo na ujinga. Makanisani siku hizi kumekuwa na kazi mbili tu, kuwapa watu utajiri na kuwapa habari za vitisho vya ushirikina. Hebu tuangalie maisha ya Yesu kwani alifanya mangapi? Suala la kuutafuta uzima wa milele siku hizi kwa baadhi ya makanisa halizungumzwi tena, wao ni kupokea miujiza ya majumba na magari, kuolewa na kuzaa basi. Sijasema kwamba watu wateseke, hapana, lakini kuna mahala fulani tunachezewa akili.

Unafahamu kuwa kuna magonjwa ya zinaa kama Kisonono mgonjwa asipotibiwa mapema huweza kuathiri hadi ubongo na mfumo wa fahamu kasha kumfanya mtu awe kichaa? Bado mtu uko busy kudanganya watu kuwa eti umeongea na Mungu kakwambia huyu mtu kalogwa na watu wanaomuonea wivu kwasababu ana akili sana na darasani huko chuoni? Kuna utaofauti gani kati yaw ewe unayeongea haya na mpiga ramli msituni huko? Huyu Mungu tunayemchezea hakika ni mvumilivu sana, maana tumefanya machukizo  mengi kwa mgongo wa neno lake huku lengo likiwa kujistawisha sisi na familia zetu kwa kuwakandamiza wenye matatizo na mahanagaiko ya dunia hii.

Mungu akusaidie, na ubadili  mtazamo wa kufikilia, acha kuwaza kulogwalogwa tu kila saa, matatizo mengine unayachikonoa wewe mwenyewe, tena ukumbuke wewe sio chuma au jiwe, chuma chenyewe hupata kutu, sembuse na wewe ambaye Biblia imesema kabisa kuwa unafanana na maua a mti? Jamani, tusijitafutie shari kwa Mungu wetu ambaye sifa yake ya kwanza ni huruma na kutukirimia neema zake ili tuweze kuwa salama na kuitakatifuza dunia hii na kuhudumiana kama wana wa Baba mmoja.
Tumsifu Yesu Kristo.

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Asante kwa kutembelea blog yangu..Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

Tuesday, 25 April 2017

UTASHI NA DHAMIRI VIMETEKWA

Ulizaliwa peke yako, utakufa peke yako. Tumia akili yako vizuri

Siku chache zilizopita niliandika mada ndogo yenye kichwa cha mada ‘KWANINI KUJAMIIANA NI HATARI KABLA YA NDOA.’Na kuiweka kwenye magroup ya watsup,facebook na instagram (@eng.ngukiwamalekela) ili kuona mitazamo ya watu hasa vijana juu ya hili. Kabla sijaeleza sarakasi za huko nitaomba kurudia hapa kile kipande kidogo nilichoandika.

Kujamiiana hakuna nafasi yoyote kuonesha mapenzi hata kama mpo katika mahusiano kwa muda mrefu au hata kama ndoa ipo karibu sana na ni wachumba rasmi. Bali:

  • Hupunguza mvuto wa msichana kwa mvulana
  • Humfanya msichana awe mtumwa kwa mvulana
  • Hofu ya mimba, magonjwa na kutojiamini
  • Mwanaume kutooana umhimu wa kufunga ndoa na msichana huyu kwa maana anampa unyumba ambao ndio kiini cha ndoa, kama ni ugali hata kwa mama yake upo tu.
  • Mgogoro wa nafsi na kukosa uhusiano na Mungu
  • Mwanamke kuishi kwa kujihami (defensive) kwa kuhisi yeye ni (supplier) mtoa ngono tu bali mtu wa kuolewa ni mwingine.
  • Kila baada ya ngono kwa mwanamke wimbo hubadilika kutoka ‘jitahidi tujitunze na tufikie malengo yetu ya ndoa’ na kuanza kuwa ‘ukinisaliti nitakuua wewe na kisichana chako au nitajiua, nimejitoa mwili wangu kwaajili yako, tafadhali nifichie aibu yangu huku mvulana yeye akijisifia kwa wenzake na kuwaeleza ulivyo mchakarikaji kumfurahisha kingono na unavyojibembeleza kwake ulivyo huna jeuri ya kumuacha.
  • Nakukumbusha tu kwamba madhara ya ngono kabla ya ndoa yapo tu hata kama mtaoana lakini yapo na wahusika hujitahidi kuyapotezea hasa kisaikolojia, kiroho na kijamii.
  • Labda niulize, hujawahi kuona mtu kapata sifuri kwenye mtihani wake wa mwisho, nabado utamsikia anasema ‘haijaniathiri kitu, na haya niliyapanga mwenyewe,watu kibao wamesoma lakini hawana lolote, nitatoka kivingine. Hivi ni kweli huyu mtu hajaumizwa na haya matokeo? Ukweli ni kwamba kaumia sana na hakuna namna ya kurudisha ule muda na rasilimali vilivyopotea, bali anajitahidi kupambana na dhamira yake kuuzima ukweli. Hata kwenye ngono ndivyo ilivyo.

Bora nusu shari kuliko shari kamili. Najua ni ngumu kumeza hasa kama uliaminishwa kuwa huwezi, lakini chukua hatua na ugeuke.
Mwisho wa nilichopost.

Sasa pamoja na baadhi ya watu kuukubali ukweli japo unauma, wapo waliosema yafuatayo ambayo niliyategemea na nilifurahi kwa maana walikuwa wazi:

  • Wapo waliosema hayo yalikuwa zamani sio kwa sasa
  • Wengine wakawasemea na wenzao kuwa ‘wewe humu umejiandikia mwenyewe peke yako wengine hatukubaliani na hilo’
  • Wengine wakasema ‘utaishije sasa bila kufanya ngono? Au unatakaa watu wafanye punyeto (masterbation)?
  • Wengine wakasema ‘siku hizi wanaume wanataka kujaribu kwanza (kutest) ndipo waoe. Ukijifanya kubania utaishia hivyo bila kuolewa. (Japo mwenye huo mtazamo ndio huishia kuwa kisima cha majaribio na kuolewa ni kwa wengine)
  • Wengine wakasema huwezi ishi katika mahusiano kama dada na kaka lazima mfanye tu.
  • Na wengine wakaweka maneno ya kuamsha hashiki kwa wenzao ili waamini kabisa kuwa haiwezekani hata kidogo kumudu mhemko wa mwili pale utakapohitaji kufanya ngono


Nilichojifunza ni kwamba wengi wa waliokuwa wanapinga kabisa ukweli huu wapo kundi la mwanafunzi niliyemtolea mfano kwenye post yangu hapo juu. Watu kukubali kuwa ‘ndio nimewahi kufanya lakini ni kwa makosa na iliniathiri na sitaki kurudia kosa au sitaki watoto wangu waje kuishi hivi’ wanadhani ni ushamba na kujidhalilisha. Watu wanapigia chapuo uongo ili tu ku draw tension ya wasio na msimamo.

Katika mada yangu sikulenga kuhukumu mtu ambaye amewahi kukosea bila kujari mara ngapi, hapana. Mungu wetu ni Mungu wa kutoa nafasi ya pili (second chance) kwa mtu aliyekosea. Naongea haya kwa maana wapo watu ambao tendo moja la ngono lilizalisha mimba, magonjwa ya ajabu yasiyona tiba, aibu na mvurugano mkubwa wa kifamilia na kuzalisha majuto ya daima.

 Lakini wapo ambao wamefanya mara nyingi nabado madhara yao pengine ni yandani zaidi na kwa nje mtu hajayaona. Hii haimaanishi wamefanya aina mbili tofauti za ngono, hapana bali ni Mungu tu anakuepushia na kukupa nafasi ya kubadilika akiamini kuna watu fulani wanakutegemea hivyo akiruhusu pigo hilo wengi watapata shida sana kwa kukosa huduma yako.

Mtu wa kundi hilo la pili ndiye kinara wa kupigia chapuo utekaji wa dhamiri za watu kwa kujigamba kuwa hawezi kuishi bila ngono kana kwamba anaviungo vya chuma ambavyo yuko makini kuweka oil na grease ili visipate kutu. Kama lilivyojanga la UKIMWI ni rahisi sana kulitaja ukiwa huna maambukizi. Hebu kutana na watu wanaoishi na maambukizi ya UKIMWI na uone mtazamo wao, wanatamani kupona, wakiambiwa nenda eneo fulani uatapona wanakwenda kwa gharama yoyote. Wakiambiwa ukila kitu fulani utapona, watakula hata kama hakina radha.

Ndivyo ilivyo hata kwa wanaopigia chapuo ngono kwa kutumia kondomu ni wale ambao hawana maambukizi. Kama huamini nenda kwa huyo mfanyangono mwenzako mwambie nimepima na kugundulika na maambukizi ya UKIMWI, lakini nimekuja na kondomu kwahiyo tutafanya ngono salama mpenzi wangu’, uone kama kuna sketi au suruali itashuka hapo, ng’oooo hata busu tu atakukatalia na tumbo kuanza kumuunguruma.

Nikukumbushe tu kuwa UKIMWI upo Tanzania tangu 1983, ni zaid ya miaka 33 iliyopita, na kizazi kinachojishughulisha sana na ngono ni vijana ambao wapo chini ya miaka 30 au juu kidogo, hivyo wengi wanaishi na maambukizi ya UKIMWI pengine kwa kuzaliwa nayo, hivyo unaweza kufanya ngono wote au mmoja akawa hajawahi kabisa kufanya ngono na afya yake ni nzuri kumbe ana maambukizi kutoka kwa wazazi wake na ni HIV carrier, hatumii ARV na CD4 zipo juu kama kawaida.

Lakini pia mahusiano ni kipindi cha kuchunguzana, hivyo mnaweza kwenda na badaye ukagundua tabia chafu ambayo haiwezi kuvumilika, utafanyaje? Tuchukulie mfano mahusiano yamepamba moto na mnafanya ngono then unagundua huyo mfanyangono mwenzako ni mshirikina aliyebobea na familia yao kila mtoto  wa kwanza huwa wanamtoa sadaka kwenye mizimu na matambiko huko, nayeye ni kiranja wa hiyo kazi, wakati huo mwanamke kashajazwa mimba, na mnasema tutaoana utafanyeje? Au unagundua mwenzako ni jambazi la kutupwa, kuua kwake ni kama kunywa mtindi, utafanyeje?

Asilimia kubwa ya mahusiano yanayohusisha ngono huishia kuoa/kuolewa na mtu ambaye humpendi kwa maana mvulana unaanza kumuonea huruma mtoto atakayezaliwa baada ya kumpa mimba msichana hivyo unaamua tu kumchukua kwa ushenga wa mtoto aliye tumboni. Hivyo upendo utakuwa kwa mtoto na sio mke napengine kuwachukia wote. Msichana naye anaona aibu kuwa na mtoto ambaye atalelewa na baba mwingine na hajuwi mtazamo wa watu kuona yuko vile napengine akaja kupata mume ambaye hataki mtoto wa kumkuta, hivyo anaamua kumbana huyu aliyempa mimba ili amuoe kwa lazima.
Umeyasikia mengi,  suala la upande utakaofuata ni juu yako. Mungu amekupa dhamira ikusaidie kukuonya. Chukua hatua binafsi



Katika wale waliokuwa wanacomment kuna mmoja aligusia suala la punyeto au masturbation naomba nilifafanulie madhara yake hapa:

Punyeto/Masterbation ni tabia ya baadhi ya wanaume kutumia mikono yao kusugua uume hadi kutoa mbegu za kiume na kujiridhisha wenyewe (emotional/sexual self-satisfaction).

Madhara yake ni:
  • Unavunja mishipa myembamba ambayo inasaidia resistance wakati wa haja ndogo, ule uthabiti wa uume kucontol mkojo unapungua hivyo ukienda kukojoa unakosa uwezo wa kuuzui hivyo utatoka kama bomba la maji hadi mwisho, na ukiendelea hadi ukubwani kwenye utu uzima basi mkojo ukikubana tu unajitokea wenyewe hapo ulipo kwa maana mawasiliano kati ya uume na kibofu yanakatika. Sasa kama utatembea na pampasi kama kichanga mimi sijuwi.
  • Ikumbukwe hili linahusisha ubongo pia, na ukifika muda wa kuwa ndani ya ndoa utakuwa unatoa mbegu ambazo hazijakomaa (pre mature ejaculation), ambao ni ugumba kwa mwanaume.
  • Mwanaume aliyezoea (addicted) kufanya punyeto hawezi kufurahia tendo la ndoa muda ukifika kwa maana joto linalotolewa na mkono ni kubwa kuliko linalotolewa na mwanamke, hivyo atamuacha mkewe na kuendelea na tabia yake.
  • Wengine wanapata madhara hadi nje kwa kupata vidonda na makovu (physical wounds and scars ).

UTAACHAJE
Kwanza kubali kuwa ulichokuwa unafanya kina madhara makubwa sana na ni hatari sana hivyo anza taratibu kupunguza na baadaye utaacha kabisa. Pata matibabu kama ulipata vidonda na waone washauri nasaha ili kuata counseling itakayokuimarisha ubongo wako na uanze safari mpya.

JE WASICHANA NAO WANAFANYA PUNYETO?
Ndio. Katika semina ambazo tumekuwa tukifanya na vijana mara nyingi hili limeibuka. Wapo baadhi ya wasichana kwa kuyaona mitandaoni au kudanganywa na watu wamekuwa wakitumia vifaa vyenye muundo wa uume ili kufanya ngono wenyewe kama ndizi, test tubes, tango, karoti nakadharika. 

Madhara ya vyote hivyo ni:
  • Kusababisha michubuko katika via vya uzazi ambapo hupelekea makovu ambayo yanaweza kuziba mirija ya uzazi au kusababisha kuota virusi vitakavyopelekea uambukizo wa kansa ya shingo ya kizazi (cervical cancer)
  • Kuwafukuza bacteria wazuri ambao wapo kwenye via vya uzazi kupambana na shambulio lolote la mangojwa fulani. Ikumbukwe kutokana na mifumo yetu ya uzazi kwa mwanaume hali ya ugonjwa fulani wa ngono dalili zikianza kuonekana nje, huenda ndani bado hali sio mbaya sana, lakini kwa mwanamke hali ikianza kuonekana nje ndani ujue hali ni tete zaidi.
  • Lakini pia vitu vyote hivyo vinaweza kukatikia na kubakia ndani, utavitoaje?

KWA WAVULANA NA WASICHANA:Aina zote za punyeto ni hatari, ushamba na ulimbukeni, acha kujaribujaribu kila usikiacho.

Natamani nieleweke lengo langu kuandika haya sio kuhukumu au kuonesha kuwa mtu aliyewahi kukosea ndio hafai, hapana. Lengo langu ni moja tu, kama mimi na wewe hatujawahi kukosea basi TUMSHUKURU MUNGU NA TUSIJARIBU KUKOSEA, TUITAWALE MIILI YETU NA KUPAMBANA NA VISHAWISHI HADI NDOA. Kama mimi na wewe tumewahi kukosea lakini Mungu katuacha hai, basi TUGEUKE NA TUSIRUDIE KOSA, TUTUMIE VYEMA NAFASI YA PILI TULIYOPEWA NA MUNGU ILI KUHAKIKISHA ANGALAU TUNAKUJA KUWA NA KITU CHA KUWAASHAURI WATOTO WETU. Ukigeuka Mungu anapunguza madhara (Spiritual and mental rejuvenation), utakuwa na amani na mfumo wa utendaji kazi wa nafsi yako unarekebika na kuwa mzuri, na Baraka za Mungu utaziona kwa macho yako.

‘Kama wewe unatabia fulani, basi usitudanganye kwamba wote wanatabia au mtazamo kama wako. Ulizaliwa peke yako na utakufa peke yako. Wote tutakufa, ishu ni nani kafa kivipi. Mungu ametuumbia dhamiri inayotuonya na kutukumbusha kugeuka, usikubali mtu aiteke dhamiri yako na kukuburuza na mtazamo wake hasi ambao hujuwi utakupekeka wapi. Uking’ang’ana na njia ya POTELEA MBALI, utatokea mtaa wa NINGEJUA’

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman

Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

Friday, 17 February 2017

HOMILIA HAITOSHI.

Ee Mungu tupe shauku ya kujifunza neno lako, ndilo taa ya miguu yetu.

Tumsifu Yesu Kristu. Shairi hili ni sehemu ya mahubiri na mafundisho yangu ya kila siku ambalo kwa neema ya Mungu lilichapishwa katika gazeti letu la kanisa Katoliki , gazeti la Kiongozi kwa matoleo mawili mfululizo yani toleo la  tarehe  8-14/5/2015   na toleo la   15-21/5/2015 .  Kama hukupata nafasi ya kupata nakala ya gazeti lile na kusoma basi ni wakati wako sasa kupata ujumbe uleule. Lipo pia shairi langu lililochapishwa katika gazeti la kimisionari la Enendeni ambalo hutolewa na Wamisionari wa Consolata , lakini maudhui yake yamepita (yalijikita kukemea tukio la muda mfupi) hivyo sitaliweka humu.

HOMILIA HAITOSHI, CHIMBA ZAIDI IMANI


01
Tumsifu Yesu Kristo, Enyi watoto wa Mungu,
Nawaletea kijito, cha umande na ukungu,
Sifanye moyo mzito, kukionja hiki chungu,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

02
 Marakadha husikia, Wakatoliki wavivu,
 Kitaka kufatilia, ni kauli ya kichovu,
 Kanisa lataka jua, liwalisheni kwa nguvu?
 Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

03
Kama hujanielewa, namaanisha usome,
Vitabu kede twapewa, kwanini usijitume?
Kama hautaki sawa, mimi ninakupa shime,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

04
Amigu na Kamugisha, na wengine waandishi,
 Vitabu vingi kutosha, kuvisoma ni mbishi,
 Ujue unachekesha, nafsiyo hushibishi,
 Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

05
Huenda hauna pesa, semina wahudhuria?
Muumba umemsusa, wadhani achekelea?
Baraka unazikosa, na kwake hutaingia,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

06
Misa unahudhuria, sawa hiyo njema sana,
Vipi kwenye jumuia, mbona unakwepa bwana?
 Hebu acha kusinzia, uyasahau ya jana,
 Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.
07
Katekisimu wajua, mafundisho imejaa,
 Ukurasa kifungua, hutaacha kurudia,
 Changanya na biblia, roho itashiba pia,
  Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

08
Imani sio kikombe, Useme umeoteshwa,
Ni wamuumba ujumbe, nafsiyo kushibishwa,
Hivyo lazima uchimbe, pasipo kubabaishwa,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

09
Huenda nakuchefua, Tulia utaelewa,
Lengo hapa ni kukua, Imani kuielewa,
Sasa ukinishushua, utashindwa kutambua,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

10
Muda wa kazi unao, sawa wataka riziki,
Basi acha singizio, sala haziepukiki,
Nong’oneza jiranio, Shetani mtoe nduki,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

11
Wajua watakatifu, Yasome maisha yao,
Tena haitakukifu, watakuombea hao,
Uchambuzi akinifu, Utakupandisha huo,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

12
Theresia dada yangu, Angelina mama pia,
Na wote rafiki zangu, mimi nawakumbushia,
Upendo tu ndio rungu, shetani mkung’utia
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

13
Huyu atajiuliza, kwani kusali lazima?
Namimi nakuuliza, Ni wamhimu uzima?
Hapo ukijiongeza, jibu unalitazama,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

14
Imani sio pambio, la kujua siku moja,
Tena si ya kivamio, Eti ni mtu wa hoja,
Machweo hata mawio, nidhamu  ndonambamoja,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

15
Kwaleta afya kusali, pole kama hutambui,
Novena na taamuli, hapo ndio silegei,
Fikara pia Rozali, ni Zaidi ya mayai.
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

16
Mimi ninakukumbusha, Tena mimi sio kitu,
Ukiona nakuchosha, ndo udhaifu wa mtu,
Jitahidi hakikisha, kusali unathubutu,,
Homilia haitoshi,Chimba Zaidi imani.

17
Kanisa letu tajiri, kwa vipawa vya kutosha,
Walimu na wahubiri, hima watuhamasisha,
Ila tu ni ujeuri, tamaa watukatisha,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

18
Nguki naishia hapa, kazi kwako kuyashika,
Sidhani ‘metoka kapa,  kwa machache niloshuka,
Kusali acha kukwepa, Baraka zipate shuka,
HOMILIA HAITOSHI,CHIMBA ZAIDI IMANI.
 Namini umepata chochote kwa kupitia shairi hili. Ubarikiwe sana.
Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Thank you for visiting my blog. Click ‘ view the web version’  to see other topics OR SEE THE  LIST ON THE FOOTER BLOCK which have been categorized by months posted.  You are welcome also for Professional information about Agriculture, water resources, soil and environmental conservation visit www.wadcotanzania.blogspot.com  .Eng Nguki