Friday, 17 February 2017

HOMILIA HAITOSHI.

Ee Mungu tupe shauku ya kujifunza neno lako, ndilo taa ya miguu yetu.

Tumsifu Yesu Kristu. Shairi hili ni sehemu ya mahubiri na mafundisho yangu ya kila siku ambalo kwa neema ya Mungu lilichapishwa katika gazeti letu la kanisa Katoliki , gazeti la Kiongozi kwa matoleo mawili mfululizo yani toleo la  tarehe  8-14/5/2015   na toleo la   15-21/5/2015 .  Kama hukupata nafasi ya kupata nakala ya gazeti lile na kusoma basi ni wakati wako sasa kupata ujumbe uleule. Lipo pia shairi langu lililochapishwa katika gazeti la kimisionari la Enendeni ambalo hutolewa na Wamisionari wa Consolata , lakini maudhui yake yamepita (yalijikita kukemea tukio la muda mfupi) hivyo sitaliweka humu.

HOMILIA HAITOSHI, CHIMBA ZAIDI IMANI


01
Tumsifu Yesu Kristo, Enyi watoto wa Mungu,
Nawaletea kijito, cha umande na ukungu,
Sifanye moyo mzito, kukionja hiki chungu,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

02
 Marakadha husikia, Wakatoliki wavivu,
 Kitaka kufatilia, ni kauli ya kichovu,
 Kanisa lataka jua, liwalisheni kwa nguvu?
 Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

03
Kama hujanielewa, namaanisha usome,
Vitabu kede twapewa, kwanini usijitume?
Kama hautaki sawa, mimi ninakupa shime,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

04
Amigu na Kamugisha, na wengine waandishi,
 Vitabu vingi kutosha, kuvisoma ni mbishi,
 Ujue unachekesha, nafsiyo hushibishi,
 Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

05
Huenda hauna pesa, semina wahudhuria?
Muumba umemsusa, wadhani achekelea?
Baraka unazikosa, na kwake hutaingia,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

06
Misa unahudhuria, sawa hiyo njema sana,
Vipi kwenye jumuia, mbona unakwepa bwana?
 Hebu acha kusinzia, uyasahau ya jana,
 Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.
07
Katekisimu wajua, mafundisho imejaa,
 Ukurasa kifungua, hutaacha kurudia,
 Changanya na biblia, roho itashiba pia,
  Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

08
Imani sio kikombe, Useme umeoteshwa,
Ni wamuumba ujumbe, nafsiyo kushibishwa,
Hivyo lazima uchimbe, pasipo kubabaishwa,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

09
Huenda nakuchefua, Tulia utaelewa,
Lengo hapa ni kukua, Imani kuielewa,
Sasa ukinishushua, utashindwa kutambua,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

10
Muda wa kazi unao, sawa wataka riziki,
Basi acha singizio, sala haziepukiki,
Nong’oneza jiranio, Shetani mtoe nduki,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

11
Wajua watakatifu, Yasome maisha yao,
Tena haitakukifu, watakuombea hao,
Uchambuzi akinifu, Utakupandisha huo,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

12
Theresia dada yangu, Angelina mama pia,
Na wote rafiki zangu, mimi nawakumbushia,
Upendo tu ndio rungu, shetani mkung’utia
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

13
Huyu atajiuliza, kwani kusali lazima?
Namimi nakuuliza, Ni wamhimu uzima?
Hapo ukijiongeza, jibu unalitazama,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

14
Imani sio pambio, la kujua siku moja,
Tena si ya kivamio, Eti ni mtu wa hoja,
Machweo hata mawio, nidhamu  ndonambamoja,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

15
Kwaleta afya kusali, pole kama hutambui,
Novena na taamuli, hapo ndio silegei,
Fikara pia Rozali, ni Zaidi ya mayai.
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

16
Mimi ninakukumbusha, Tena mimi sio kitu,
Ukiona nakuchosha, ndo udhaifu wa mtu,
Jitahidi hakikisha, kusali unathubutu,,
Homilia haitoshi,Chimba Zaidi imani.

17
Kanisa letu tajiri, kwa vipawa vya kutosha,
Walimu na wahubiri, hima watuhamasisha,
Ila tu ni ujeuri, tamaa watukatisha,
Homilia haitoshi, Chimba Zaidi imani.

18
Nguki naishia hapa, kazi kwako kuyashika,
Sidhani ‘metoka kapa,  kwa machache niloshuka,
Kusali acha kukwepa, Baraka zipate shuka,
HOMILIA HAITOSHI,CHIMBA ZAIDI IMANI.
 Namini umepata chochote kwa kupitia shairi hili. Ubarikiwe sana.
Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Thank you for visiting my blog. Click ‘ view the web version’  to see other topics OR SEE THE  LIST ON THE FOOTER BLOCK which have been categorized by months posted.  You are welcome also for Professional information about Agriculture, water resources, soil and environmental conservation visit www.wadcotanzania.blogspot.com  .Eng Nguki  


Wednesday, 25 January 2017

JUMUIYA-Stress Free Zone

Hofu na mashaka yote, hutoweka kwa kushiriki Jumuiya

Tumsifu Yesu Kristu na heri ya mwaka mpya. Ninakupa salamu za mwaka mpya kwakuwa tangu mwaka huu uanze sijaandika mada hata moja humu na hii ndiyo mada inayofungua mlango wa mada moto moto kwa mwaka  2017. 

Tukiwa tunaendelea kumshukuru Mungu kwa uzima pamoja na changamoto kadha wa kadha ikiwemo uhaba wa mvua na mengineyo leo nataka nikupakulie kidogo juu ya mada muhimu sana inayokumbushia umuhimu wa jumuiya ndogo ndogo. hasa zinazoundwa na wanafunzi. 

Katika miaka yangu minne nikisoma chuo kikuu SUA-Morogoro 2012-2016 nimeyaona na kujifunza yafuatayo kutoka katika jumuiya ya wanafunzi wakatoliki (Tanzania Movement of Catholic Students-TMCS)

  • Jumuiya ndio mahali pekee unapoingia ukiwa mgonjwa na kutoka mzima. Ndio vijana tunaumwa sana tu sio kidogo. Tunaumwa mawazo yakumiliki vitu tusivyo na uwezo navyo, tunaumwa ulevi, tunaumwa fitina, tunaumwatamaa za mwili, tunaumwa wivu, tunaumwa kukosa huruma nakadharika. Katika kushiriki jumuiya utakutana na watu wenye vipawa vya kuhubiri, vipawa vya kushauri, vipawa vya kufariji ambao hao wote humfanya aliyehudhuria kutoka akiwa mtu mwingine kabisa huku akiwa na moyo uliotakata na matarajio mema yanayoshikika.
  • Jumuiya ndio mahali pekee ambapo utatua mizigo yako ya msongo wa mawazo. Chuo/Shule ni ngumu sana (huenda ilikuwa hivyo kwangu pekee) kiasi kwamba kuna wakati unatamani kumuazima mwenzako kichwa chako ili upumzike kidogo kuwaza. Unaweza kuamka asubuhi na kugundua hujamaliza kazi inayotakiwa kukusanywa leo, wakati huo huo kesho kuna test na inabidi ufanye marudio ya notes nyingi sana, kama hiyo haitoshi leo siku nzima kuna vipindi, (saa moja asubuhi hadi saa moja na nusu usiku) na ni masomo ambayo ukikosa kipindi kimoja basi huko mbele ya safari utaona vumbi tu, Kwa njia hii inafika jioni umejaa msongo wa mawazo, hapo bado hujapigiwa simu nyumbani huko kuna matatizo nakadharika.                                                                                                                         Ukienda kusali na wenzako katika jumuiya lazima utaokota kitu hata kimoja cha kukufaa. Mungu ana watu wake wataalamu wa ucheshi na kukufanya ufurahi huku ukibarikiwa kwa sala za jioni, nyimbo na tafakari ya neno la Mungu. Nkuhakikishia ukiondoka hapo na kwenda kushika madaftari yako unakuwa na nguvu mpya (you gain new momentum). Iwe kwenda kusoma kwenye kundi au peke yako, utaona kuna wepesi wa hali ya juu baada ya kutoka sala.
Tukifurahi na kuimba kwenye jumuiya. Baada ya hapo vichwa vyetu viko safi kuyakabili masomo. Kuna wepei fulani Mungu anajaza ndani yetu.

  • Jumuiya ndio kituo cha afya ambako chanjo dhidi ya magonjwa sugu ya uchonganishi, majivuno, wizi , dhambi zote na vilema vyake hutolewa. Ni kweli kwamba kuhudhuria jumuiya huku ukiendelea kufanya mambo mabaya haina maana. Lakini ni ukweli wa  mchana kwamba mtu anayeshiriki jumuiya anaenda kukutana na neno la Mungu ambalo ni moto wa kuteketeza dhambi na vilema vyake. Mahubiri yanachoma na kufukunyua ndani ya uvungu wa moyo wa kila asikiaye hasa linapozungumzwa jambo ambalo ni kilema chako. Kama kweli dhamiri yako ipo hai, utaumia moyoni, utafanya kitubio na kuweka mikakati ya kuto kukosea tena. Hii ni chanjo kwa waliokuwa hawajafanya kosa fulani na ni dawa kwa aliyekuwa tayari muhanga wa kilema hicho.
  • Jumuiya ndipo mahali pekee ambapo unakwenda kupata walezi watakaokubeba ukipata changamoto nzito isiyobebeka na marafiki wengine. Natambua kila mtu ana rafiki au marafiki anaowaita wakushibana,  lakini kuna wakati betri zinaweza kugeukiana, umeme unazima kila kona, ndipo utajua kuwa ni wakushibana au wa kunjaana. Kwa mtu ambaye anashiriki na wenzake kusali katika jumuiya, anatengeneza mtandao wa watu sahihi ambao watatumia mbinu zote kuhakikisha anapata msaada. Nikiwa chuoni nimeona wanafunzi wakipata matatizo makubwa ambayo hata wazazi hawawezi kutatua kwa haraka,  lakini jumuiya imekuwa ikijitoa binafsi au kushirikisha wanajumuiya na kutoa msaada wa haraka kwa njia ya huduma na ufariji.
  • Jumuiya ndipo mahali wanakopikwa wazazi bora, wachakarikaji, wapambanaji na watakaowajibika katika familia zao . Hakika hili halihitaji ubishi. Matharani katika jumuiya kumekuwa na semina za WAWATA, mafungo, huduma katika vituo vya watoto yatima, wazee na wasiojiweza na mengi ynayofanana na hayo. Hii ni tabia njema na ishara ya kujiandaa kuyabeba majukumu ya familia na jamii ambayo inatarajia makubwa sana kutoka kwako. Mambo mengi sana hata mimi binafsi niliyachukua moja kwa moja na yanatakiwa kufanyiwa utekelezaji bila ubishi kama kweli nataka kuwa baba bora wa familia. Mzazi asiye na huruma kwa wahitaji, kuwafundisha watoto kujitoa, kufariji, tabia njema na matendo ya huruma huyo sio mkristu, bali ni wakala wa shetani. Labda unaweza kusema mbona wapo wakristu ambao bado wanatabia chafu na malezi ya vumbi kwa familia zao? Ngugu yangu hayo ni mapungufu ya mtu binafsi kutokana na malezi yaliyomkuza na watu wanaomzunguka, lakini sio ishara ya Ukristo.
  • Jumuiya ni mahali pa kukata kiu ya mafundisho ya kikristu na kukufanya uwe mwalimu hodari wa familia na jamii. Hebu tafakari zile misa za katikati ya juma, novena za Roho Mtakatifu, novena kwa Mt Rita wa Kashia, semina za wanajumuiya, mapadre, watawa, yale  mafungo ya Fransalian mara mbili kila muhula (kwa wanafunzi wa SUA), Joint Prayers, hija kwa kila mwaka wa masomo, jamani Mungu akupe nini mkristu wewe mwanafunzi? Hii kwangu ni chakula bora tena mlo kamili. Tatizo ni uvivu tu wakupuuza haya mambo na kujifanya tumetingwa na mambo mengine (busy) kumbe tunajikosesha mambo muhimu kwa roho zetu  amnbayo ni chakula cha roho zetu hivyo  unakufa kwa utapiamlo huku chakula bora kipo mezani, na kimeandaliwa na mama yako mzazi ambaye ni mpishi hodari mwenye viwango vya aina yake. 
Mungu anajidhihirisha kwa watu kupitia upendo wa jumuiya, chamsingi usimuumize mtu au usitende dhambi.

Baada ya masomo, tafakari ya neno la Mungu tunapata nafasi ya kushiriki matukio ya kupongezana na ucheshi kama jumuiya. Tukitoka hapo mambo yanaingia vizuri kichwani

Kutembelea vituo vya wahitaji ni kujifunza malezi katika jumuiya. Shiriki na wenzako. (Mgolole sister's orphanage centre, Mehayo centre, Fungafunga, Amani centre etc )

  • Jumuiya ni mahali pa kutengeneza mtandao mkubwa wa mawasiliano ya kijamii, kibiashara  ndani na nje ya nchi. Katika kusali kwenye jumuiya watu wamepata watu waliowapa taarifa za kibiashara maeneo mbali mbali, wengine wameunda umoja na kufanya uzalishaji wa pamoja, wengine wameoana (iwe kwa makusudi ya Mungu na sio kulazimisha). Kila mkoa utakaoenda unajikuta kuna mtu anakufahamu kwasababu mlikuwa mnasali pamoja. Kwa hili hata mimi ni shahidi, nimepata mambo mengi sana kupitia ndugu zangu katika Kristu ambao nilikutana nao katika kusali jumuiya. Uitegemee kmengine yote ya jumuiya kana kwamba wewe ndio mmiliki wa chombo hiki (Active participation). 

Mungu akutie nguvu, neema na baraka zake zisikupungukie, na uwe na wakati mwema. Karibu kwenye mtiririko wa mada motomoto kwa mwaka huu mpya 2017, usisitete kuuliza chochote au kuchangia kwa comment, email au simu. Tumsifu Yesu Kristu

'JUMUIYA NDOGONDOGO ZA KIKRISTU, ROHO MOJA, MOYO MMOJA KATIKA KRISTU!

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman

Thank you for visiting my blog. Click ‘ view the web version’  to see other topics on list ( in case you don't), which have been categorized by months posted. Eg to see the topics posted last month meaning last year, just click 2016 then after reading resent posts at the footer select the term order posts to see other topics, do the same until you are done for all posts from October 2016. You are welcome. Also for Professional information about Agriculture, water resources, soil and environmental conservation visit www.wadcotanzania.blogspot.com  Eng Nguki  



Saturday, 3 December 2016

TUNASHANGAA YAMEOTAJE, NA TUMEYAPANDA WENYEWE

Kila  mtu amejeruhiwa/kuathiriwa na janga la UKIMWI kwa namna fulani.

Habari. Bila shaka unafahamu tarehe 1 Desemba ya kila  mwaka ni siku ya UKIMWI duniani. kabla sijaanza kuzungumzia lengo langu hasa kukihusu kichwa cha mada yangu, basi pitia takwimu hizi hapa chini juu ya hali ya UKIMWI Tanzania Bara zilizotolewa Dec 1 2016 na TACAIDS kupitia viongozi mbalimbali na vyombo vya habari:

Takwimu
Maelezo
5.3%
 Maambukizi ya UKIMWI kwa Tanzania bara. Sawa na watanzania 5 kati ya kila watanzania 100
6.2%
 Wastani wa wanawake walioathirika na maambuziki ya UKIMWI.  Sawa na wanawake 6 kati ya kila wanawake 100
3.8%
Wastani wa wanaume walioathirika na maambuziki ya UKIMWI. Sawa na wanaume 4 kati ya kila wanaume 100
10.6%
Vijana kati ya umri wa miaka 15-24 wanamambukizi ya UKIMWI, sawa na vijana 11 kati ya kila vijana 100

Ikumbukwe takwimu hizi ni kwa wale ambao wamepimwa iwe ni upimaji wa hiari wa kawaida, kabla ya kufunga ndoa, wakati wa uchangiaji damu au wakati wa ujauzito. Utakubaliana na mimi kuwa kuna kundi kubwa sana la waathirika hasa maeneo ya vijijini ambako watu wanapata maambukizi ya ukimwi lakini hawana elimu juu ya utambuzi wa afya na wengine huishia kudhani wamelogwa na kujikuta wanafakamia miti shamba au kwenda kwa waganga wa kienyeji kupiga lamri nakadharika. Kwa lugha rahisi mimi naamini hali ya maambukizi ni  mbaya zaidi ya inavyodhaniwa kwa takwimu.

NANI MCHAWI?
Sio mimi ni wewe. Hapana ni wewe sio mimi

Sisi wenyewe na serikali yetu. Ndio ni sisi wenyewe tunajiloga na kuitmbukiza jamii yetu katika shimo la huzuni na giza totoro inayoumiza na kuangamiza kizazi hiki na kijacho. Kundi kubwa la watu wanapigia debe maisha ya kufanya ngono kama ni utaratibu wa kawaida wa maisha ya watu hasa vijana. Watu wenye ushawishi mkubwa wamefumba mdomo kuongea ukweli na hali halisi ya mambo kwenye visababishi vya kuenea kwa UKIMWI, na badala yake wamejikita zaidi kutoa matamko ya kulalamika matokeo yake na kuomba, kutafuta na kutumia fedha nyingi kushughulikia matokeo ya UKIMWI.

Kwa macho yangu nimeshuhudia shirika fulani linatembelea mashuleni na makundi ya vijana wa kucheza ngoma za burudani, mashindano ya kucheza na kimba kisha kutoa zawadi za mabox ya kondom kwa vijana hao. Kama hiyo haitoshi, pembeni waliweka banda na kuwaalika vijana wa kike kwa wakiume waende ili wakafundishwe namna ya kufanya ngono kwa kondom, tena taasisi ya kielimu. Na nilishuhudia vijana wasio na mpango mkakati wa maisha yao wakimiminika kwenda huko, halafu bila aibu tunashangaa kwanini maambukizi yanapanda?. Kisingizio cha kondomu kimetumika sana kukoleza moto wa ngono kwa vijana, na asilimia kubwa ya vijana wamenasa kwa mtego huo na bado wakayabeba maambukizi. Kondom hazijafika leo, zipo kabla ya UKIMWI na bado maambukizi yanazidi kupanda,  bado hatufungui macho na kuelewa kuw tunawekeza kwenye mradi usiozalisha. 
Muda wa kunyoosheana vidole haupo. Tumia akili yako kuweka malengo ya kujitoa kwenye ngono. Mungu atakuepusha tu. Ni kweli na hakika. Jionee huruma wewe ,kizazi chako na cha wengine.

Kupitia takwimu hizo hapo juu unaona vijana ambao tunawaita 'sexually active group' ndio vinara wa maambukizi. Maambukizi hayo yanachochewa na wao wenyewe pia mabinti kufanya ngono na watu wazima ambao wanamaambukizi ya UKIMWI na hutumia fedha zao kama ulimbo wa kuwanasa wasichana wadogo.

KWANINI WANAWAKE WANAONGOZA KWA MAAMBUKIZI ?

Katika vitu vya kuchekesha na kuudhi ni uchambuzi wa watu tena wasomi juu ya swali hili, 'kwanini wanawake wanaongoza kwa maambukizi ya UKIMWI'. Nasema inachekesha kwakuwa hakuna hata mmoja niliyemsikia akigusia chimbuko na mzizi wa tatizo hili,bali wote waling'ang'ana kwenye matokeo, isipokuwa baadhi ya viongozi wa dini walisema ukweli. Nilikuwa nawafuatilia kwa karibu sana. Wengi walitumia kigezo cha unyanyasaji wa kijinsia, ubakaji, umasikini nakadharika, vitu ambavyo vinachangia kwa kiai kidogo sana.

 Inachekesha zaidi kwakuwa sikusikia hata mmoja akihoji kwanini kwenye nyimbo na miziki wanaume wanavaa suti na kupendeza  lakini wasichana wanavaa nguo za ndani pekee na visidiria  na kuachia maungo yao nje? Hakuna aliyesema kwanini wanawake wa sasa hawaoni thamani tena ya miili yao na kutembea uchi barabarani huko na kuamsha hashiki za wanaume pia kutoa mafunzo ya udadisi waa ngono kwa watoto wadogo? Nyie mnojiita watetezi wa haki za ujinsia hasa haki za mwanamke na unyanyasaji, hapa huwa mnavaa miwani ya tinted sio? Ukweli ni kwamba tabia ya wasichana na wanawake kujianika miili yao na kuona wao ni bidhaa inayohitajika sana kwa wanaume (highly demanded commodity) kumefanya wanaume wengi kuwa na mahusiano na wanawake zaidi ya mmoja. Ni wanawake wachache sana wenye mahusiano na wanaume zaidi ya mmoja, lakini wanaume wengi wamejilundikia wanawake kwakuwa wanawake wenyewe (sio wote) waamekuwa mawakala kamili wa kusajili wanaume kwa mavazi yao na kushindwa kusema HAPANA kwa ngono. Hivyo mwanaume mmoja anayeishi na maambukizi ya UKIMWI ni rahisi kusambaza kwa wanawake wengi zaidi kuliko uwezekano wa mwanamke mmoja anayeishi na maambukizi kusambaza kwa wanaume wengi zaidi. Hii inatokana na sababu za kimaumbile pia, ukichanaganya na maelezo yangu hapo juu basi unapata HADITHI NJOO ,UTAMU KOLEA.
Wanawake ni waleta uhai mpya. Ni wasaidizi kamili wa Mungu kuleta watu duniani huku. Tabia ya kujitoa ufahamu na kujidharirisha kunafanya hata watoto walio matumboni kuanza kulia kwa hofu kwakuwa wamebebwa na wazazi maharamia wasiojali utu na kujisitiri kwa heshima. BADILIKA LEO

Kwa mtindo huu, suala la UKIMWI litabaki kuwa miradi ya watu ya kujitengenezea fedha, na kufurahia maambukizi kupanda kwakuwa bila UKIMWI na wao watakosa kazi. Ni bora tukaongozwa kwa busara binafsi, na kujifunga mkanda, yani KUSEMA HAPANA KWA TABIA YA NGONO NA TABIA AMBATANISHI. Nikisema haya kwa mtu ambaye anjiona amekubuhu kwenye tabia hii, huenda anashangaa na kuona naandika nadharia, lakini huu ni ukweli ambao huenda ukawa ni mgumu kuumeza lakini hamna namna, utabaki kuwa ukweli. Kwani ukisema HAPANA KWA NGONO unatoka vidonda sehemu fulani ya mwili? Mwanamke ukiamua kusema hapana, mwanaume hana jipya. Hisia za wanaume huwa zinapanda haraka, na ukisema hapana na kuondoka, huwa zinashuka haraka pia na ufahamu kurejea kama ilivyo sufuria iliyotolewa kwenye jiko la moto. Wakati wanawake hisia zao hupanda taratibu (hasa pale unapompa nafasi mwanaume ya kujieleza na kujiweka karibu na wewe), kisha mkifika juu, huwa zinabaki juu hukohuko kwa muda mrefu kama chungu kilichotolewa kwenye jiko la moto. Ndipo hapo utasikia mara wanaume baba yao mmoja, oh, nataka mtoto  tu, lakini sitaki kuolewa,, sitakuja kumwamini mwanaume yoyote, kwa maana wote ni waongo, oh,,,,,, ah,,,,, nakadharika. Kuongezeka kwa watoto wa je ya ndoa au wasio na mlezi ya moja kwa moja kutoka kwa baba zao, kunatoa picha halisi ya hili jambo. Wazazi wengi au hawataki au hawawezi kuzungumza ukweli na mabinti zao, na wakijitahidi sana wanaishia tu kusema UWE MAKINI, AU TUMIA AKILI. Maneno ambayo hayaakisi kabisa kuwa mzazi unataka binti yako au kijana wa kiume aepukane na janga hili la UKIMWI.

Ukweli ni kwamba mimi ni mmoja kati ya watu ambao hawashangai kabisaaaaaaaaaaaaaa juu ya idadi ya wanawake wenye maambukizi ya UKIMWI kuwa kubwa kuliko wanaume, kwasababu wao ndio huchochea hurka ya wanaume kuwapapalikia. Kwa sentensi hiyo sijasema wanaume hatuna makosa, hapana, nasi pia tunatakiwa kupambana na udhaifu wa miili yetu, kujifunza kuuthibiti mwili kwa maana ni ukweli wa mchana kuwa changamoto ni nyingi, kichwa kinavurugika unapoona miili ya wanawake waziwazi, lakini jikubali, badili mazingira, mshirikishe Mungu, sema HAPANA PIA KWA VISHAWISHI, usitumie pesa zako ili kukoleza mapambano na mikikimikiki ya ngono. Kama umeoa basi ridhika na mke wako kwa maana ndiye Mungu aliyekupangia. Kma hujaoa basi timiza malengo yako na baadaye fanya uchaguzi sahihi.

Sitaki kusema imani za dini zinasemaje juu ya hili, lakini nijuavyo mimi HAKUNA DINI HATA MOJA INAYOSHABIKA NGON KABLA NA NJE YA NDOA. KUSUBILI INAWEZEKANA, SEMA HAPANA KWA NGONO ILI KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA UKIMWI NA KUEPUSHA MATUMIZI YA FEDHA NYINGI AMBAZO ZIMEKUWA ZIKIELEKEA HUKO. Kumbuka kwa Tanzania kuanzai DEC 1, 2016 serikali imezindua Bodi ya udhamini wa mfuko wa UKIMWI ambako mabilioni ya fedha yanakusanywa kutoka vyanzo vya ndani ili kushughulikia mambo ya UKIMWI na kupunguza utegemezi kwa wahisani wa nje ambao vigezo vyao hubadilika mara kwa mara..
Nikutakie tafakari njema na tufanye maamuzi ya busara ili kuzikomboa familia zetu. Mungu akubariki.

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
UCE Tanzania-Volunteer
03 Dec 2016
Thank you for visiting my blog. Click home/ view the web version to see other topics on list ( in case you don't), which have been categorized by months posted. Eg to see the topics posted last month, just click November.  The same for October. You are welcome. Also for Professional information about Agriculture, water resources, soil and environmental conservation visit www.wadcotanzania.blogspot.com  Eng Nguki  

Ili ufanye vizuri unahitaji juhudi, ili ufanye vizuri  zaidi unamuhitaji Mungu.Hauwezi kufeli darasani kwasababu unatoa sehemu ya muda wako kufanya kazi za Mungu. Usikate tamaa., angalia unakosea wapi na urekebishe. Huenda ukapitia Chamgamoto kidogo na ukaanza kumlaumu Mungu au mtu fulani, hapana, utapita tu, kaza mwendo. 25 Nov 2016-SUA

Wednesday, 23 November 2016

SIO RAHISI HATA KIDOGO.

Mungu yuko upande wetu. Tujibidiishe kusali na kufanya kazi.

Tumsifu Yesu Kristu.
Namshukuru Mungu paoja nanyi kwa neema ambazo anatujalia kila siku ingawa hatustahili. Maovu yetu mara kadhaa yametutenga mbali na Mungu na kutusogeza kubaya ambako haukuwa mpango wa Mungu Zaburi  103:12 Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi
Ni kweli, tumefanya maovu na lazima tukiri wazi kwa vinywa vyetu
Zaburi 106:6 Tumetenda dhambi pamoja na baba zetu, Tumetenda maovu, tumefanya ubaya.
Isaiah 59:12 Maana makosa yetu yamezidi kuwa mengi mbele zako, na dhambi zetu zashuhudia juu yetu; maana makosa yetu tunayo pamoja nasi, na maovu yetu tumeyajua;
Jeremiah 14:20 Ee Bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi..
Mara nyingi nikiwa nasoma chuoni, wakija wanafunzi ambao walishamaliza walikuwa wanatutia moyo kwa kutuambia shule sio ngumu mtafaulu tu. Ni kweli nen hili ni muhimu na la faraja kwa wanafunzi wanaoendelea. Mimi pia nimemaliza hapa chuoni, lakini niwaambie tu bila kuumauma maneno, shule ni ngumu, ten asana tu Ndio shule sio rahisi hata kidogo. Kwa sentensi hii sina maana kwamba huwezi kumaliza au kufaulu vizuri, bali juhudi za makusudi na kujitoa sadaka ya muda lazima viwepo kwa nguvu zote.

NINI KINAFANYA CHUO/SHULE WAKATI FULANI KUWA NGUMU KUPITA KAWAIDA
Kwa ambao wamewahi kutumia computer:, ikitokea unahamisha vitu vingi  kutoka kwenye flash disk kwenda kwenye computer au kinyume chake, utaona computer inaandika two days left , ikimaanisha hiyo kazi ya kuhamisha mafaili yako itachukua siku mbili, baada ya dakika kama tatu, utaona inakambia bado siku moja, baada tena ya dakika chache inakuambia bado msaa sita, tena baada ya muda mfupi inakwambia bado nakika kadhaa, badaye sekunde na ile kazi inakwisha ndani  ya robo saa tuamaa na kuongeza juhudi hifanya iishe mapema na kwa ufanisi. Hivyo kama mtu sio mvumilivu na anasafari baada ya lisaa limoja, akiona ile 2 days left, basi anaahirisha na kuona itamchelewesha. .Kwa tafsiri rahisi ni wamba kazi yoyote mwanzo huonekana kubwa na nzito sana , na ndiyo ilivyo, lakini kutokata  Zipo sababu nyingi sana. Pamoja na changamoto ya uwezo binafsi wa mwanafunzi kitaaluma, ulevi, msongo wa mawazo na majukumu yanaayozidi uwezo, naomba nizitaje sababu kongwe mbili ambazo ni UVIVU NA NGONO.


UVIVU: Mithali 19:15 Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa.
Sina sababu ya kuanza kudadavua uvivu ni nini. Kwa kifupi ni hali ya mtu kukwea kutimiza wajibu wake kwa makusudi. Mvivu hufurahia matokeo mazuri pasi na kuangalia mchakato ulioleta matokeo hayo. Uvivu upo kwenye vitu vingi sana. Huenda ni katika kusoma, au katika kusali. Mtu mvivu kusali hupima nguvu za Mungu kwa vitu vichache alivyovichagua yeye. Kwa mfano akiwa hahudhurii jumuiya, bali misa anaenda na mambo yake ynamuendea vizuri, basi anaridhika na kujiambia kuwa Mungu katosheka na donoadonoa yake kwenye mikusanyiko ya sala, hivyo wale ammbao wanaenda jumuiya na kufanya kazi kadha wa kadha za kanisa, nabado mambo yao ni magumu, anadhani hawapo sawa kiimani au wanakosea mahala fulani.

Wito wangu kwenu ni kusali misa na sala za jumiya kila siku kwa maana hujuwi lini litazungumzwa lipi ambalo litakufaa wewe wapi hasa baada ya maisha ya shule. Epuka kufanya substitution ya muda wa Mungu  na vitu vingine kama chakula, stress nakadhalika.

Mifano yenye undugu na uvivu hatari:
  • Kama ni muda wa kuanza kipindi cha dini, na wewe ndio upo kwenye foleni ya chakula na roho haikuumi kabisa, ujue kuna changamoto.
  • Kama akikukwaza mtu fulani hasa yule ambaye unadhani ndio muhimu kuliko kitu chochote, basi unafunga vyote including mambo ya Mungu, except chakula tu, ujue kuna changamoto.
  • Kama uko addicted  na kitu fulani mbacho ndio starehe yako eg mpira, movie etc na kama ndio unatazama muda wa kipindi cha dini na kuona bora uendelee kutazama, ujue kuna shida somewhere.
  • Hata kama umetoka kipindi cha mwisho darasani saa 1:20 au hata saa 1:30 jioni na kuna nafsi inakuambia ‘umechelewa sana, dakika 15 hazitoshi kwenda hadi dini, bora tu utembee taratibu, ukale upumzike’ , hiyo faraja siyo ya Kimungu.
  • Au ukisikia wimbo wa Roho Mtakatifu unaimbwa, basi unajiambia ‘nimeshachelewa, hakuna sababu ya kwenda sahizi, nitaenda tu kesho’ hapo ni tatizo, ni uvivu huo.
  • Mtu mvivu anateemea mijiza tu bila imani na mapendo, anawaza habari za kuambiwa ;POKEA MUUJIZA WAKO, WALE KUKU WAKO WATAANZA KUZALIANA KWA FUJO HADI BANDA LISITOSHE, Unajibu Aminaaaaa , wakati kuku wenyewe unawapa chakula mara moja kwa wiki, kila siku wanaumwa new castle . Hapo hata akisema KUKU WAKO WATAANZA KUTAGA MAYAI MATATU KWA SIKU ,’ Na wewe unajibu Aminaaaa. Huo ni uvivu wa kufikilia.
  • Ref, : Baba na mama walikuwa na ugomvi kwenye familia, na wakaenda kwa mtu anajiita nabii na mtumishi wa Mungu. Lengo wapokee muujiza wao wa shetani anayesumbua familia yao. Jamaa akawaambia kuwa Roho wa Bwana anamshuhudia kuwa mama ni mshirikina, kumbe mama hata hana lolote masikini,familia ikaanza kuvurugika hadi walipoenda kwa padre kusuluhisha. Tena baba ni msomi mweye PhD , nikawa najiuliza hii sio academic PhD, labda ni  PH ya soil inayokaribia acidity. Yote haya ni matokeo ya uvivu wa kufikilia na kutaka matokeo ambayo hujayatolea jasho kutafuta.
Tufunguemioyo yetu na kumtukuza Mungu kwa kazi zetu na vipawa alivyotujalia Mungu wetu


NGONO: Ni kujamiana nje ya utaratibu (kabla na nje ya ndoa). Kujamiiana ndani ya ndoa huitwa TENDO LA NDOA. Ni takatifu, halali na linatamkika kirahisi. Pia matokeo yake ni furaha kwa kila mtu, lakini matokeo ya ngono hayapokeleki hata kama mtu ni tajiri na ana kila kitu.
 Katika mazingira ya chuo, mihemko ya kuhusiana kwa pupa ni major consumer wa kuwapoteza utashi watu.  (Watched Hot Friday Movie)

Ninapozungumzia ngono ninalenga michakato yote yennye mlengo huo na mawakala wake. Mifano:
·         Mara ngapi umevaa mavazi ya makwazo na kuwavuta watu kingono. Kwa maana mwingine unaweza kumuamsha hashiki mtu na akaona wwewe hauingiliki, hivyo anagain momentum ya kwenda kumshawishi mwingine aweze kutimiza uovu wake huo.
·         Mara ngapi umekuwa kinara wa kuahidi tu watu kwamba utaolewa/kuwoa? O level, A level, JKT, wiki la registration, unayesali naye, classmate, mnayesoma naye elective course, halafu unaota eti hawana effect, subiri tu utaelewa siku moja.

·         Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kabla hata test one hujafanya, hiyo UE ndio hata hujui inafananaje, but tayari umesema kuna mtu yupo hoi hajiwezi juu yako. Hapo inatoa picha ya moja kwa moja what is your primary goal. Sijasema kwamba mahusiano mabaya, hapaa, lakini yanahitaji kujipanga, utulivu wa nafsi na mwili yaliyopita kwenye MVUTO, MAWASILIANO na baadaye MAHUSIANO.

·         Mara ngapi umejithaminisha sura yako na kujiona wewe ni bora sana hivyo hakuna atakayekupa shida kwenye mahusiano kutokana na uzuri wako hasa kwa wasichana  (kioo hakidanganyi). Lakini ukweli ni kwamba wewe huwajui wanaume, bali unawajua wavulana tu. The sme kwa wavulana, mostly tunawajua wasichana ambao bado wako kwenye makuzi, na tunajidanganya kuwa ni wanawake.

·         Msichana, once you put your skirt off, everything is off. Ni rahisi sana, mtu akikuona na utulivu ukampotea , akija anaongea hadi anatetemeka , msichana na wewe ndio unaona unamkomeshaaaaa kwa uzuri wako kumbe mwenzako pale akili zake za kawaida hazipo, in such akianza kukusogolea towards your direction, huruma inakuingia, akisema mguu pande, unajibu mguu sawa. Baada ya kukufahamu, Yeye mweyewe tena anakuambia, nyuma geuka, mbele tembea, Kiruuuuuu, unaanza kulalamika mbona harudi, kwani aliona nini that day? Jibu ni kwamba hakuona kitu, coz angekiona kitu angekirudia tena kwa mara nyingine..

JE TUSIINGIE KATIKA MAHUSIANO?
Tuingie tu, lakini uwe kweli ni muda sahihi, mmejiandaa vya kutosha na uhakika wa kupropagate, hii inahusisha mtazamo wa kiimani na kirasilimali. Kumbuka hii ni tofauti na urafiki, kwa maana urafiki hautafutwi na hauna limitation, bali mahusiano hutafutwa na yana limitation. Lakini pia jifunze kuweka mahusiano bila ngono. Tawala mwili wako, vaa mavazi ya staha, jikubali kuwa wewe ni binadamu uliye kamili.

Katika mazingira fulani roomates wana attribute watu tuingie kwenye mahusiano kutokana na huduma ambazo wanazipata kwa hao wanaowaita wapenzi wao, wakati sio wapenzi bali ni wafanya ngono wenzao, eg wakiugua etc. Au simu zao wakiongea na kubembelezana usiku, masikinini wewe tumbo linakuunguruma na kuona kama Mungu kakusahau. Hivi umekosa vipimo vya kupma kazi za Mungu?

KAMA ANALAZIMISHA NGONO, NITAKATAAJE WAKATI NAMPENDA?
Sio kweli, huo ni unafiki. Upendo hauunganishwi na ngono, kuna kitu kimukuscorpion na unajifanya huoni huo uchfu na shimo ambalo mnajichimbia wote wawili hasa msichana.
Tukiambie kizazi chote ukweli kwamba ngono ni adui anayetutenga na MUNGU.
  • ·    Kwanza mwambie wewe sio chombo cha starehe, hivyo mkataba wa ngono unauvunja rasmi.
  • ·    Akiendelea kulazimisha mwambie haupo tayari kuendelea na hayo mahusiano.
  • ·    Punguza mawasiliano na badaye acha kabisa.
  • ·   Utaumia kidogo kwa kipindi cha mwanzo na baada ya muda fulani utagain momentum ya amani. Bora maumivu kidogo ya sasa kuliko maumivu ya kudumu badaye.
  • ·   Usikubali tena kukutana naye sehemu za faragha , anaweza  kukudhuru kwa namna yoyote endapo utakataa kutimiza matakwa yake. Mkikutana msalimie kama kaka/dada.
  • ·    Acha kukurupukia mahusiano mapya mapema, tuliza kichwa fanya mambo ya msingi sana hasa sala na shule. 


VIPI JUU YA UHAKIKA WA MTARAJIWA WANGU KUWA ANAJITUNZA HUKO ALIKO?
Haikuhusu. Wewe heshimu mwili wako, wekeza kwenye sala, Mungu atakulindia huyo ambaye humjuwi, kwa maana kujiliinda kwako ni sala pia. Once ukimpata mkakati wa kwanza wa kuuweka ni kuweka mkataba kuwa NGONO NI ADUI WA MAHUSIANO . Na utamjua siku ya ndoa,  na ukisema basi wewe unaanza taratibu majaribio ya mwili wako kisa una uhakika utamkuta used, basi wewe hautofautiani na wapiga lamli ambao wapo very detailed kuongea mambo ambayo hawawezi kuprove. Hii ni kwasabau hata mchumba wako aliyekutolea posa na mahari anaweza kufa siku moja kabla ya ndoa, na asikuoe, wala hawawezi kusema marehemu kaacha mjane mmoja ambaye alitakiwa kumuoa kesho.

Kwa hayo machache niwatakie kila la heri katika masomo yenu, na Mungu awasaidie sana, nasi tunawaombea san ili mpate wepesi katika masomo yenu. KARIBUNI KWENYE MAHAFALI KESHOKUTWA 25/11. Tumsifu Yesu Kristo. ( 23/11/2016- TMCS SUA NEW HOSTELS)

Eng Herman Nguki wa Malekela (Bsc Irrigation & Water Resources Engineering  2012-16- SUA)
  Email  ngukiherman@ymail.com instagram:@eng.ngukiwamalekela

Tembelea www.ngukiherman.blogspot.com mara kwa mara kujisomea mada mbali mbali za vijana, mahusiano na kanisa. Karibu ujifunze.
Thank you for visiting my blog. Click home/ view the web version to see other topics on list ( in case you don't), which have been categorized by months posted. Eg to see the topics posted on October , just click October. You are welcome. Also for Professional information about Agriculture, water resources, soil and environmental conservation visit www.wadcotanzania.blogspot.com  Eng Nguki  

Saturday, 12 November 2016

REJESHA TABASAMU LAO, KRISMAS HII

Wahitaji wanakutegemea wewe, jifunze kuhudumia makundi maalumu

Nakumbuka wakati niko mdogo, tena nikiishi katika familia ya kipato cha chini sana, bibi alijitahidi sana wakati wa sikukuu hasa Krismas na Pasaka angalau kupika wali ili majirani wenye uwezo watakavyoanza kunukisha vyakwao basi nisijisikie vibaya, au kuingia kwenye mtego wa kuchoropokea huko, si unajua tena utoto. Lakini ni ukweli usiopingika kwamba pale unapokuwa na uduni fulani au kuishi maisha magumu unaishi kwa hofu na kuona watu wote hawakupendi (defensiveness). Ikitokea mtu fulani kajitolea kukusaidia nawewe ufurahi angalau siku maalumu kama sikukuu, hakika unatenga muda wa ziada kusali kwaajili yake ili afanikiwe zaidi.
Logo ya Jumuiya ya Sant' Egidio

CHRISTMAS LUNCH NI NINI?
Chama cha kitume cha Sant' Egidio kilicho chini ya Kanisa Katoliki kinawaita waliobarikiwa kuwa na uwezo kidogo kuliko wenzao ili kujitoa kuwasaidia wahitaji. Ninapozungumzia uwezo sijasema pesa pekee, bali hata kusali kwaajili ya wengine, kujitolea muda kwaajili ya kuwasaidia wengine kwa huduma, faraja na sala. Miongoni mwa misingi au nguzo ya jumuiya hii ni sala na huduma. Kwenye kipengele cha huduma hii inahusisha kwenda kuwatazama wagonjwa majumbani au hospitalini, kuwatazama wafungwa na wakimbizi. Unaenda kusali nao na kama una zawadi yoyote bila kujali ni ndogo kiasi gani, kwa maana Mungu aliyekuwezesha kuvipata anajua vyema kuliko wanadamu wanaokutazama kwa nje. 

Kwaajili hiyo chama hiki cha kitume huandaa chakula cha mchana kila tarehe 25 Desemba na kuwalisha makundi ya wahitaji mahali pale walipo, kuwapa zawadi na kufurahi pamoja nao. Makundi haya huhusisha watoto ytima, wazee, walemavu na watindiwa ubongo. Mfano kwa chuo kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) wao huwakusanya wahitaji kutoka nyumba ya wazee na wasiojiweza Fungafunga, vituo vya watoto wenye ulemavu wa mwili na akili Mehayo na Amani, Kituo cha watoto cha Rosalia wa Sowano nakadhalika.
Ninaposema wahitaji wote ieleweke ni WOTE bila kujali dini wanazotoka wala kituo kiianzishwa na watu gani.



Upendo wa Mungu hudhihirika katika nyuso za wahitaji pale wanapokumbatiwa na kuambiwa wanapendwa na wana nafasi ya kuendelea kuishi. Ikumbukwe huduma ya namna hii sio ya kikundi fulani pekee, hapana watu wa dini zote wapo walemavu na wahitaji. vivyo hivyo suala la kujitoa kwa wahitaji halina mipaka.
 Kama unapata shida sana kuelewa suala la Christmas Lunch , tumia simu yako au Computer yako nenda kwenye google na undike CHRISTMAS LUNCH OF SANT' EGIDIO , utaletewa video na maelezo ya jinsi tukio hili linavyofanyika nzhi mbalimbali duniani kwa maana sio Tanzania pekee, na utagundua unachelewa tu kuungana na kundi kubwa la watu linalojichotea neema kwa Mungu kila uchwao kwa kuwasaidia wahitaji.
Wengine hawana miguu wala mikono, hivyo wewe ndio wakuwachukulia chakula na kuwalisha kama ambavyo hapa dada Dorice Stanford anavyofanya katika Christmas Lunch ya jumuiya ya Sua
Viongozi wa jumuiya za wanafunzi wakatoliki vyoni TMCS na jumuiya ya Sant' Egidio wanahangaika kila kona kutafuta michango kila kona ili kuwezesha utoaji wa chakula hiki cha mchana anagalau kila mhitaji apate sahani moja ya chakula siku ya Christmas. Wapo wachache, na hawawezi kufika kila mahali kuhamasisha, ikumbukwe ni wanafunzi na wanabanwa na ratiba za chuo, lakini  uwe mwanafunzi au sio mwanafunzi unaweza kuchangia leo hata kuwalisha wahitaji wawili tu siku hiyo kwa njia rahisi nitakayokwambia leo humu.
Sio Tanzania tu hata Burundi, Malawi na nchi nyinginezo wanajitolea kufanya huduma hii, hata wewe waweza ifanya kama sehemu ya kumshukuru Mungu. Anza leo.
Jumuiya inajitahidi kupandikiza moyo huu wa huruma kuanzia kwa vijana wadogo kabisa ili wakue huku wakitambua kuwa wajibu wa kusaidia wahitaji ni wa lazima kwa kila ambaye Mungu kamuweka hai. Hii itapunguza unyanyasaji na pengo kati ya walio nacho na wasio nacho. Hebu fikiria wewe binafsi ikitokea kuna sherehe fulani muhimu, ukajiandaa vizuri sana na kusafisha viatu vyako kisha kuviweka nje vikauke vizuri. Dakika chache kabla ya shamrashamra kuanza unagundua viatu vyaki nje vimeibwa na hauna viatu vingine, hivyo utalazimika kuvaa malapa au ubaki ndani umejifungia kwa maana wenzako wote wameulamba vizuri nje huko. Yote tisa, la kumi anatokea mtu anaviatu jozi mbili au tatu, na unamuangalia kwa jicho la huruma lakini hakuelewi, unamwambia shida yako, lakini anakuambia hivi vingine atavivaa wiki ijayo hivyo hawezi kumgawia mtu. Sijuwi utawaza nini au utajisikiaje
Uwe sauti yao. Uwezo unao. kidogo ulichonacho gawana na wahitaji.
JE UNGEPENDA KUUNGANA NA MAMIA YA WATU KUCHANGIA CHRISTMAS LUNCH YA MWAKA 2016?

Nirahisi sana. Mchango wako wa kiasi chochote utakaotoa utafanya mambo yafuatayo:

  1. Usafiri kwenda na kurudi kuwachukua wahitaji kutoka katika vituo vyao na kuwaleta eneo moja. Hawa ni wazee, watoto na walemavu kutoka Fungafunga, Mehayo, Amani Center na Kihonda.
  2. Mapambo ya ukumbi.
  3. Chakula na vinywaji kwa wahitaji tajwa hapo juu.
  4.  Zawadi kwa wahitaji ambapo baada ya chakula kila kituo hupewa zawadi kama unga, mchele,  mafuta, maharage na vifaa vya shule kwa watoto wanaosoma.
KUCHANGIA----Tumia mawasiliano hayo hapo juu kuchangia. Kumbuka kuwasiliana na viongozi hao mara baada ya kuchangia hasa kwa walio mbali. Kwa wale walio karibu, kuna wanafunzi wachache wanatembea na fomu za kuchangisha huduma hii, tafadhari changia kwa kadiri Mungu alivyokuwezesha. Pia jitolee sadaka ya muda kufanya usafi, maandalizi na kwenda ukumbini siku hiyo 25/12 mara baada ya misa ili usaidie kuwahudumia wahitaji wakati wa chakula. wahitaji ni wengi hivyo watu wa kuwasaidia pia wanatakiwa kuwa wengi. Waweza wasiliana hata na mimi nitakupa maelezo zaidi na kukuunganisha nao.
Mungu wa mbinguni anatambua uwezo wako kuwa ni mdogo, na anakuhitaji ujitoe kwa pale utakapoweza. Jitoe tafadhari. Nakutakia tafakari njema kwa hayo machache niliyokushirikisha, naamini utaungana nami kuhakikisha hili linawezekana. Waweza kumhudumia hata mzee au mlemavu mmoja tu au familia fulani isiyojiweza hapo karibu na kwenu. Sasa usikubali shetani akupige mtama ukaanza kusingizia eti hakuna wahitaji karibu na kwenu, hapo utakuwa unamtukuza ibilisi ambaye ni baba wa uongo.
Uwezo unao, fanya mabadiliko kwa jamii inayokuzunguka, iaminishe kuwa maisha mazuri ni yakujitoa kwa wahitaji ambao watasali kwaajili yako na Mungu atakufungulia milango ya baraka zake. Sant' Egidio huwa hatuhitimu, ni huduma hadi siku ya kufa kwako, ukiishiwa vinavyoshikika, hudumia kwa sala na faraja, utabarikiwa.
Thank you for visiting my blog. Click home/ view the web version to see other topics on list ( in case you don't), which have been categorized by months posted. You are welcome. Also for Professional information about Agriculture, water resources,soil and environmental conservation visit www.wadcotanzania.blogspot.com  
Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman