Tuwafundishe watoto kusamehe, lakini tusiwape hofu. |
Katika maisha ya ukuaji kuna vitu
sio rahisi sana kuvisahau hata kama havina tija sana. Moja ya vitu ambayo
nilikuwa naogopa sana ni kupigana. Sasa kuna jamaa mmoja wakati niko shule ya
msingi alikuwa hakai mbali sana na nyumbani alifanikiwa kufahamu kuwa nina huo
woga. Na kwa sababu hata familia yao ilikuwa juu kimaisha alikuwa na ujasiri wa
ziada, na kama hiyo haitoshi alikuwa kanizidi madarasa kama matatu hivi
(tulikuwa tunasoma shule moja ya msingi huko Idodi-Kitanewa) na umri kanizidi.
Lakini hivi vyote sio kisingizio
kwa maana mbinu za kupigana zipo nyingi tu hata kama mtu kakuzidi nguvu, kwani
kwenye Biblia Daudi alifanyeje kumpiga Goliath? Ndivyo ilivyo ndugu yangu. Sasa huyu jamaa alikuwa akijisikia
tu ananipiga, dah, ukizingatia hali yetu ya maisha ya nyumbani, nikawa najiona
dhaifu sana kumfanya chochote huyu jamaa, tena mimi nilikuwa naishi na bibi yangu
tu nyumbani.
Basi kila nikipigwa na yule
jamaa, nikawa naenda kusema kwa bibi ili aliruhusu namimi nimgoliatishe huyu
jamaa ambaye alitumia udhaifu wangu kunigeuza mimi ngoma yake ya mazoezi. Ajabu
bibi alikuwa ananizuia na anaishia tu kusema ‘wewe muache tu , nitaenda
kuwaambia wazazi wake wamuonye asirudie hiyo tabia’. Nikawa nayaelewa yale maneno, japo huyu jamaa aliendelea na tabia
yake ya kunipiga akijisikia hasa mkienda kucheza mpira maeneo ya wazi au
tukienda mtoni huko kuogelea kipindi cha maji mengi na kuchoma viazi (
vimbwegea).
Mnyonge ukibahatika kupokonyoka hapo, ni kutimua mbio hadi mafichoni huko. |
Kiukweli pamoja na kwamba huyu
jamaa alikuwa amenizidi mabavu kwa mfumo fulani, lakini laiti bibi angeniruhusu
tu nijitutumue nitakavyoweza, hakika ningetafuta cha kufanya kama alivyofanya
mwenzangu Daudi wa kwenye Biblia, hata kutumia mawe tu au manati (Kwa maana
nilikuwa nayo na kokoto za kutosha muda wote). Ile hali ilikuwa inanichefua
sana na kujikuta wakati fulani nawaka hasira na kuona kama bibi pia anaiogopa
ile familia kwa maana mama yake mdogo yule jamaa ndio alikuwa balozi wa mtaa. Dah, lakini kulikuwa na fundisho kubwa
sana kwa bibi kunizuia kumrudi yule jamaa, maana alikuwa ananiambia sentensi
moja tu ya kihehe; ‘umtesa neke twangule nongwa’, akimaanisha utamuumiza na mwisho wa siku tutazua kesi.
Yule mbabe wangu alikuwa na kaka
yake, ambaye kiukweli alikuwa mpole sana, japo alionekana na nguvu sana lakini
hakuwa mgomvi kabisaa. Na wakati fulani betri zikigeukiana kwa huyu mbabe
wangu, yule kaka yake alikuwa anananisaidia angalau nipate upenyo wa kufanya
mazoezi ya kukimbia hadi nyumbani. Aisee, usiombe kuishi maisha ya unyonge na
kujiona huwezi kufanya kitu. Kama ni mtoto ni afadhari sana uwe na akili za
darasani, angalau unakuwa na watu wa kukuogopa kwenye kipengere hicho, hasa
wale ambao ikitolewa kazi wanakuja uwashushie vitu, wenyewe wanasema ‘unawasovia’
hata kama hakuna hesabu humo. Hawa watakutetea siku ukibanwa na waonezi wako,
na wakati mwingine unawashitakia ili wakawapige mkwala waonezi wako.
ZAMU YA MBABE KUKUMBANA NA DHAHAMA
Siku moja ilikuwa sikukuu, kama
sijasahau sana ilikuwa kati ya Pasaka au Krismasi. Sasa pale kwao wakaweka
mziki na watoto tukawa tunaserebuka pale. Nilikuwa nacheza kwa tahadhari sana
maana nipo nyumbani kwa mbabe wangu, na likitokea la kutokea yule jamaa atakuja
tu hata kunikanyaga kama kifaranga, wahehe tunaita kiswiya.
Ilikuwa siku ya kufurahi sana kucheza mziki,lakini kuna jamaa alikuwa ananinyima amani. |
Wakati mambo yanaendelea ikatokea
ugomvi kati ya yule mbabe wangu na kaka yake. Weee nikajivuta pembeni kabisa
mnyonge mimi. Katika purukushani yule mkubwa akamtwanga kichwa cha mdomoni yule
mbabe wangu na kufanikiwa kumng’oa jino la mbele, kisha nayeye kuumia kwenye paji
la uso kwa kuchimbwa na jino. Dah, kwakuwa yule mbabe wangu ana asili ya
ukorofi, watu waliokuwepo walimuacha pembeni hapo akilia na kuugulia maumivu,
kisha wakachemsha maji haraka na kuanza kumkanda-kanda huyu kaka mtu aliyeumia
paji la uso.
Kwakweli nilikuwa namuonea huruma
pia yule kaka mtu, na sikumuonea huruma kabisa yule mbabe wangu ambaye
alijipatia mwanya wa lazima siku ile baada ya kung’oka jino kwa kupigwa kichwa
na kaka yake. Ni kwasababu niliwaza kuwa huenda huku kuumia kutampa kipindi cha
mpito cha kuugulia maumivu hivyo kutopata muda wa kuninyanyasa au kukwaruzana
naye. Maisha yaliendelea ambapo baada ya
muda fulani kupita yule jamaa aliendelea tu na ukorofi wake na bado bibi aliendelea
kunisisitiza nimsamehe tu na kuna wakati kweli bibi alikwenda kuwaambia wazazi
wake juu ya tabia ya kijana wao ya kuninyanyasa, ambapo wazazi wake walimkemea
na kumuonya aache hiyo tabia. Yule kaka yake nilimuamini sana na kuona ni
mtetezi wangu.
MBABE WA MBABE WANGU AKAJA KUZUA YAKE
Maisha yaliendelea na walimaliza
shule wale ndugu wawili kwakuwa walikuwa darasa moja, kisha yule mkubwa kufanikiwa
kujiunga na sekondari.
Tarehe 15/06/2005 ilikuwa siku ya
gulio (mnada) kule kijijini kwetu. Hiyo siku nilikuwa na hela yangu elfu kumi
(10,000/=). Ilikuwa ni pesa yangu kabisa kutokana na kazi fulani niliyofanya,
ambapo nilitumia elfu moja kununua kitu fulani na ikabaki eflu tisa. Sasa
katika uhifadhi wa ile elfu tisa na utoto kuchangia, ile hela iliyobaki
waliniibia yote. Nililia sana, kwa maana ile hela ilikuwa kubwa sana kwangu.
Basi nikawasimulia baadhi ya rafiki zangu juu ya ule mkasa nilioupata. Sasa
yule kaka wa mbabe wangu ambaye nilikuwa namuamini sana nayeye alipata hizi
habari kuwa nimeibiwa hela elfu tisa.
Katika hali ya kustaajabu na
isiyo ya kawaida huyu jamaa niliyemuamini sana baada ya kupata zile taarifa
alikwenda kwa wazazi wangu na kuongea uongo wa kiwango cha lami na unaofanana
na uuaji kabisa. Alisema, nanukuu: ‘Herman alikuwa na hela leo na amechezea
kamali za mnadani. Mimi nilikuwa naye wakati anaenda kucheza. Nilimkatalia sana
kuwa hao watakutapeli hao, yeye akawa mbishi, nikamvuta mkono tuondoke pale,
lakini yeye aling’aang’ania kucheza hadi hela ikaisha. Nyie subirieni tu
atakuja huku analia hapa’
Duh, aisee, ukweli ni kwamba ile
siku hatukuonana kabisa yule jamaa hata ile kawaida tu kusalimiana, lakini
alikwenda kuupika uongo huo ambao kiukweli, dah inauma sana. Muda ukawadia wa
mimi kurudi nyumbani, kama alivyosema yule jamaa, nilirudi navuja chozi na hela
sina. Mama alikaa kimya ili anisikilize kwanza nini kimenikuta huko.
Nikamuelekeza kuwa nimeibiwa na sijuwi nini kimetokea, mama akanipa pole,
lakini akasema ‘mbona fulani kasema umecheza kamali na alikuzuia lakini wewe ukawa
mbishi?’ Mh, jamani, mbona mimi hata sijaonana naye leo? Akanieleza
maelezo yote aliyosema yule jamaa, kuna kitu kilinikaba shingoni kwa hasira kwa
maana nilijikuta najiuliza, :
- Alikuwa analenga nini kuongea uongo huu kwa wazazi wangu?
- Je hii hela ingekuwa sio yangu na nimetumwa na wazazi kununua kitu fulani kwaajili ya familia angeniweka katika mazingira gani?
- Je hii hela ingekuwa ya mtu hata asiye ndugu yangu labda aliniagiza nikamnunulie kitu fulani huko gulioni na akapelekewa uongo huu uliosukwa kwa ustadi mkubwa, angejisikiaje?
Nafsi yangu ilichafuka sana
ghafla na nilijikuta kwa mara ya kwanza namchukia sana kwa maana alifanya jambo
ambalo sikutegemea. Hasira zilinizidi na kujikuta nalia sana na wakati huo mama
alinituliza na kuniambia nimsamehe tu, na nijifunze kuelewa kuwa wapo watu wa
aina hiyo na nimapungufu yao, japo mtu unayewasikiliza kama ukichukua mamuzi ya
haraka, unaweza kusababisha madhara makubwa kwa taarifa za uongo na badaye
kujikuta unajutia maisha yako yote. Nikajikuta hata msaada wake kipindi ambacho
nilikuwa naonewa na mdogo wake nausahau kabisa, kwa maana kafanya jambo la
kuogofya kwa mdomo wake.
Sijawahi kumuuliza hata siku moja,
na tangu ile siku tumeonana kama mara mbili au tatu pekee hasa baada ya yeye
kuwa shule ya bweni na mimi kuhamia Iringa mjini mwezi wa nane 2005,na kuanza sekondari 2006.
Tangu kipindi hicho nilikaa kwa muda na baadaye kuwasamehe wote wawili japo kipindi
cha nyuma bado kuna roho ilikuwa inanituma nimtafute ili aniambie nini
kilimtuma kuupika uongo ule. Wote kwa sasa wanaishi maeneo tofauti tofauti na
familia zao.
HITIMISHO
Ndugu zangu, hakuna mtu mkamilifu
hapa duniani, sote ni dhaifu. Kitu cha msingi ni kutouendekeza huo udhaifu wako
(kilema cha dhambi) ambao unaweza kuwa na madhara makubwa sana kwako binafsi,
familia au watu wanaokuzunguka. Mfano ni mimi mtu niliyemuamini kupita kiasi
akaja kudhihirisha udhaifu wake kwa namna tofauti, lakini hii haiondoi ukweli
kuwa kuna mambo mazuri aliyofanya ikiwemo kunitetea kipindi cha nyuma. Hata
yule mbabe wangu, lazima tu kuna eneo fulani anafanya vizuri hata kama mimi
sikuona binafsi, huenda ni kwa mwingine. Kitu cha msingi ni kusaidiana,
kurekebishana, na wewe unayeonywa kubali kubadilika kwa maana hujuwi lini
utakutna na lipi. EPUKA UONGO NA UGOMVI KWA MAANA UNAWEZA
KUSABABISHA KIFO CHA MWILI AU NAFSI KATIKA MAZINGIRA MADOGO SANA.
Naitwa Nguki, sijawahi kumpiga
mtu zaidi ya mimi kupigwa mara kadhaa wakati niko shule ya msingi. Baada ya
hapo (kuanzia sekodari) kwakweli ni mkwara tu wa maneno umenisaidia kuepuka
mapigano , kutotilia maanane maneno chonganishi yenye uchochezi wa kupigana pia
kuomba msamaha hata kama sijakosa mimi ili yaishe na kuepusha mapigano. Kiufupi
sipendi hata kuona tu watu wanapigana na sina huo mpango kwakweli.
Eng Nguki Herman. M
Life is really something amazing
ReplyDeleteSure bro. It's a certain kind of schooling out of classes
DeleteDah bro fundisho kubwa sana, Pamoja br
ReplyDeleteTuko pamoja @Martin
Delete