I am targeted to change youth's mind set towards positivity.

I am targeted to change youth's mind set towards positivity.
I am targeted to change youth's mind set towards positivity

Sunday 3 December 2017

NIMEMPA MIMBA, WAZAZI WAKE WANATAKA NDOA NDANI YA WIKI MOJA,

Kama maandishi hayasomeki kwa mobile version, shusha mwishoni utakuta "View web version" click hapo.

Natambua fika hatari ya kujamiiana kabla ya ndoa na matokeo yake. Moja wapo ni mimba, na ikumbukwe hapa tatizo sio mimba bali ni mfumo wa kuipata/kusababisha na uwezo wa kuhudumia mimba yenyewe na mtoto atakayezaliwa. Hili nalitambua vizuri sana na nimekuwa nikiliongea na kuliandika kila uchwao, sio kwa kuhukumu hapana, hii ni kwasababu kuzaliwa ndani ya ndoa au nje ya ndoa hakufanyi azaliwe kiumbe tofauti, japo kuna hatari ya myumbo katika malezi na kumkosesha mtoto baadhi ya haki fulani za msingi au kukosa uhuru.

Katika hali isiyo ya kawaida nilijikuta nimempata msichana fulani na kufanya naye ngono, na kumpa mimba siku hiyo hiyo. Mimi  sikutambua kuwa nimempa mimba na yeye alisema kuwa hawezi kupata mimba. Basi baada ya muda fulani wazazi wake waliniita na kuniambia nimempa mimba mtoto wao na wanachotaka ni ndoa kabla mtoto hajazaliwa kwa maana hawataki mjukuu wa nje ya ndoa. Na ikiwezekana nimuoe ndani ya wiki moja.

Mungu wangu weee, presha ilinipanda, viungo vyote viliishiwa nguvu, nikawaza na kuwazua nitaishije na kumlea huyu binti, tena sina kazi na akaunti yangu benki inapumulia mashine hata elfu kumi hakuna. Nikawaza juu ya makazi na kugundua nina chumba kimoja tu nacho wanakaa wadogo zangu wawili wanaosoma tena ninawahudumia mimi mwenyewe na hawana sehemu ya kwenda. Rafiki yangu mmoja akaniambia ‘Nguki hapa komaa tu mzee baba, ndani ya wiki hii oa tu’.
Ukweli nilikuwa na hamu sana ya kuitwa baba, eh, niwe na mtoto. Lakini sasa njia niliyotumia ndiyo inayonipa majuto. Nikawa nawaza juu ya rafiki zangu na watu wa karibu, wataelewaje kuona ndoa imeibuka kama uyoga hakuna cha kuvalishana pete wala send off wala nini? Huku wazazi wa yule binti ndio kwanza hawataki kusikia chochote. Basi nikajikaza kisabuni hadi kwa baba yangu mlezi, akasema ‘hiyo changamoto umeizalisha mwenyewe na hakuna kukwepa. Mimi nitakuongezea hela kidogo kwaajili ya hizo harakati zako, kama utaongezea kwenye harusi sawa, kama ni kwemnye maisha utajua mwenyewe’ 


Kuna wakati mambo yanakaba hadi unajionea aibu wewe mwenyewe.


Kichwa kiliniuma sana, hadi nikahisi yule msichana ananidanganya. Nikampigia simu ili aje niliangalie tumbo vizuri kama linaonekana kuongezeka ukubwa. Alikuja na kunikuta nipo na rafiki zangu nimejiinamia kwa mawazo. Akafika pale akiwa ameniletea na mikate, nikamuaangalia kichovu na kumuuliza kama yuko serious kweli nilimpa mimba kwa tendo lile moja au ananipima tu akilia, akanisogelea kwa karibu, mamamamamamama weeeeeee, katumbo kamejaa mwanawane, yani hakuna ubishi. Akanishika kichwa changul kwa tabasamu na kuniambia kingereza ‘Nguki, do you think I am lying to you? This pregnancy is yours’. (Akiwa na maana nisidhani anadanganya, hiyo mimba ni yangu). Aliongea kwa kujiamini, bila wasiwasi huku akinishika kidevu changu kilichokauka kama mti mkavu kwa presha tangu nizipate hizi habari.

Kwakweli sijawahi pata maumivu ya kichwa na mawazo makali kama haya, nilitazama juu na kuona kama Mungu kaniacha, jeuri yangu ya kuwashauri vijana wenzangu ikayeyuka ghafla, nikiangalia wazazi wangu hawana uwezo wa kujitwisha hii changamoto. Nikajiuliza, nini kinafuata bado sikupata jibu. Nilijikuta nalowa jasho mchana na usiku sipati cha kufanya na wiki moja niliyopewa na wazazi wake yule binti niliye mtumbilize ndio hiyoooo inaisha.

Rafiki yangu akaniambia niende kwa wazazi wa yule binti kuwaambia nimeshindwa kutekeleza masharti yao na kama kuna lolote wanataka kufanya juu yangu kwakweli wafanye tu, maana sioni cha kufanya juu wala chini, zaidi najikuta nakonda tu ndani ya wiki moja. Basi yule jamaa yangu akanipakia kwenye pikipiki yake, haooooo hadi nyumbani kwa wazazi wa yule binti..
Kichwa kinazungukaaa kama mpira, lakini hakuna pa kutokea!


Tulimkuta mama yake akiwa nje, alipotuona tu, akamuita mumewe aliyekuwa ndani. La haulaaaaa, yule mzee alipotoka alinikata jicho hilo kwa muda katika tano bila kuongea chochote! Ohh Mungu wangu weeee, hofu ikanitanda, huku navuja jasho nikadondoka chini kama fulushi puuuuuu!, Wakati nahangaika kusimama  kwa kuishika mikono ya yule rafiki yangu, nikagundua nimeshikilia neti na nilikuwa nimezinduka kutoka kwenye ndoto yangu! Loooh, nilikuwa navuja jasho, nikainuka na kukaa, nikajikuta natamka kwa nguvu ‘Mungu, nini lakini jamani’. Asikwambie mtu, sijawahi ota ndoto yenye kashkash kama hii ya usiku wa kuamkia 25/11/2017. 
Nilipoamka nikawa nawaza hivi hizi presha ni katika ndoto, je ingekuwa live?


Narudia tatizo sio mimba bali mfumo. Aisee hizi presha sizitaki kabisaa,hii ni ndoto lakini imenipa picha nzima ya hali ambayo nitakutana nayo endapo nitajitoa ufahamu. Nakushauri na wewe kijana mwenzangu amini katika subira na jiwekee tu malengo, haya yote uyafaidi ndani ya ndoa. Narudia tena hapa hatunyoosheani vidole au kuhukumu, hapana, bali kama umewahi kukosea, basi fanya ukarabati mkubwa (Major rehabilitation) wa nafsi ili usikosee tena na kujiwekea nafasi nzuri ya kuwa mlezi bora wa familia.KUSUBIRI INAWEZEKANA, ANZA SASA.


Kitabu changu Kipya


Katika kujifunza pia nakukaribisha uniunge mkono kwa kununua kitabu nilichokiandika (DHAMIRI NA UTASHI VIMETEKWA) ambacho ndani nimeeleza mambo mengi yahusuyo mahusiano, upendo, subira, kuweka malengo, na malezi. Nimekielekeza kwa vijana, lakini pia wazazi na walezi kitawafaa sana ili kuongea na watoto/vijana wao. Ili kukipata waweza nitafuta kwa namba zangu hapo chini. Lakini pia kinapatikana  Dar es Salaam (Doloka Investment Company Ltd Millenium Towers Makumbusho-0655 266 993 na Pia Kijichi-0686 971 623), Morogoro kinapatikana chuoni Sua (nipigie nikuunganishe na wanaokiuza), Kinapatikana pia Fransalian Bookshop-Kola Morogoro na Iringa ofisi za UCE Tanzania, Kihesa-Kichangani.Karibu sana ujifunze.

Eng Herman Nguki
Email:ngukiherman@ymail.com
Instagram: eng.ngukiwamalekela

Phone #: 0763 639 101/ 0679 639 101
Asante kwa kusoma katika blog hii.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com




Monday 18 September 2017

BANDO LA MUNGU HALICHACHI.


Upendo wa Mungu hauna kipimo

Tumsifu Yesu Kristu/Bwana aifiwe/Shalom. Leo tutatafakari sehemu ndogo ya maandiko matakatifu kutoka kitabu cha nabii Isaya ambapo tutaona ukuu wa maneno yenye pumzi ya Mungu hivyo kujenga hoja ya ‘Bando la Mungu kuwa la kudumu, yaani halichachi.’

Tunasoma Isaya 43:1-5
1 Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu.
 2 Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.
 3 Maana mimi ni Bwana, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako.
 4 Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.
 5 Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi.

NOTE: Aliyekuhuluku=Aliyekuumba

Kuna uwezekano mkubwa baada ya kusoma sehemu hiyo ndogo ya maandiko matakatifu, kuna ujumbe fulani mfano wa mwale wa mwanga unapita kwa haraka kichwani mwako. Sasa mimi nitapita na baadhi ya dondoo na kuzipa maelezo kidogo lengo likiwa ni kushirikishana ukuu wa Mungu.
Mungu ni Upendo


  • Usiogope, maana nimekukomboa. Kuna wakati fulani nikawa najiuliza, mbona haijaandikwa usiogope maana NITAKUKOMBOA, bali NIMEKUKOMBOA? Herufi ‘ME’ ni wakati uliopita mtimilifu (past participle), sasa inakuwaje tumeambiwa tusiogope kama suala la ukombozi lilishafanyika? Yani mwanafunzi anakuwaje na hofu wakati kashakabidhiwa mkononi majibu ya mtihanai wake na amefaulu?. Kilichopo hapa ni kwamba bado kuna kundi kubwa la watu (huenda nikawa mmoja wapo) ambao zawadi ya ukombozi iko mikononi mwao, lakini bado wamejawa na hofu na kutumia nguvu nyingi sana kushughulikia mambo madogo na ya kawaida kana kwamba kuna mtu fulani kashikilia maisha yao zaidi ya Mungu. Kumbe Mungu mwenyewe kwa kinywa cha nabii Isaya anatuambia leo tutupilie mbali hiyo hofu na kujivunia ukombozi ambao kwa hiyari yake ameamua kutuzawadia.
  •  Nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Mtu akikuita kwa jina lako ina maana anakufahamu vizuri. Hata wanyama tu wa kufugwa, ukiwaita kwa majina wanakuwa na amani kuwa wewe ndio mchungaji wao na watakuja miguuni pako na kunyenyekea, japo hawana utashi. Nabii Isaya anatukumbusha kuwa Mungu hajaishia kutuita majina tu, bali anatusisitiza kuwa sisi ni mali yake kwa maana hata mpita njia anaweza kukuita jina lako. Kuna wakati tu kwa makusudi tunaziba masikio na kutosikia atuitapo. Kila mara inawezekana dhamira yako ikawa inakutuma kufanya jambo fulani au kukuonya kutofanya jambo fulani lakini  ukatumia nguvu nyingi kupambana na kujikuta hauitii, ina maana unajitengenezea ukuta kati yako na Mungu. Mara nyingi dhamiri huwa ipo sahihi na ndio maana kama mwili unakusukuma kufanya jambo lisilo jema , dhamiri hai hupingana na wewe kwa kuleta ugumu (resistance) katika mjongeo utakaokupeleka huko.
  • Maji mengi na mito havitakugharikisha, moto hautakuteketeza. Katika sehemu hii ya maandiko, majina moto na maji vimetumika kuwakilisha matatizo, mahangaiko na changamoto za kila siku. Kumbuka Biblia haijasema kuwa hautakumbana na huo moto au maji, bali imesema utakumbana navyo lakini havitakudhuru. Kwa lugha rahisi ni kwamba matatizo, changamoto na magumu tutaendelea kukutana nayo lakini hayataweza kutukengeusha na kututoa kwenye msitari wa imani. Yote hayo ni kutokana na upendo wa Mungu usio na kikomo kwetu, hivyo kama shukurani kwa Mungu tuzishinde changamoto kwa kuonesha ustahimilivu na ukomavu wa imani ili Mungu kwayo ajitwalie utukufu.
Mungu anatutetea dhidi ya maovu ili matendo yetu yazidi kuangaza

  • Ulikuwa wa thamani na kuheshimiwa machoni pangu, nimekupenda. Kumbe kupendwa ni zao la kuthaminiwa. Mtu hawezi kukupenda kama hajuwi thamani yako, ‘Value brings love’. Ndivyo ilivyo kwa Mungu, ametupandisha hivi hata kutuita wa thamani na heshima machoni pake, naam ndipo haswaaa anasisitiza kuwa ametupenda. Upendo wa Mungu hauna kipimo kwetu, na ndio maana kuna wakati huwa natafakari ingelikuwa ukifanya kosa na kurudia basi Mungu anachukua roho yako, je ingekuwa ni miaka mingapi tangu nizikwe? Jiulize pia wewe mwenzangu binafsi. Hakika ni wa huruma sana, sawasawa na neno lake katika Zaburi 130:3 Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?
  • Nitatoa watu kwaajili yako na kabila za watu kwaajili yako. Ndio, hili liko wazi na shuhuda kwa watu wengi nikiwemo mimi nisiyestahili. Kuna wakati fulani mambo yanakaba kila upande, inafika kipindi unauona mwisho wako uleeee unakaribia. Ghafla bin vuu anatokea mtu, watu au familia fulani inakuokoa kwenye changamoto au tatizo lako, mwisho wasiku unajiuliza hivi walikuwepo wahitaji wangapi ambao yamewakaba zaidi yangu? Imekuwaje iwe kwangu? Huyu ndio Mungu tunayemuabudu, Mungu wa surprise, Mungu wa kuinua watu pale usipotarajia ili uyaone matendo yake makuu na kushuhudia ukuu wa jina lake. Katika hili, nakukumbusha kuwatembelea wahitaji wa aina zote na kufanya lile uwezalo kwaajili yao.
  •  Usiogope kwa maana mimi ni pamoja nawe. Hapa ndipo penye uhakika wa kuendelea kumuamini na kutembea kifua mbele huku taa yetu ikiwa ni Msalaba wake (Marko 8:34). Ndio kasema mwenyewe kuwa hofu tuididimize huko shimoni, nasi tuwe na uhakika wa uwepo wake kutupigania. Sasa kama baba yako ameshasema ‘usiogope nitakupa unachotaka’, hivi unaanzaje kutapatapa huko kusikojulikana? Tulia ujichotee neema bwerere kutoka kwa mchungaji wako ambaye anakujua kwa jina na sikuzote anapita kwenye mlango wa boma lako.
Usiogope, Mungu yupo kwaajili yako


Hakika bando la Mungu halichachi, tena kwa upekee wake halina kiwango, wewe ni kupiga tu kwa maana umechorwa kwenye viganja vya mikono yake, anajua hofu zako na kila kitu. Basi Mungu awe nasi tunapotafakari matendo yake makuu na ya kuogofya, huku tukijibidiisha kutenda mema kwa wenzetu, unyenyekevu na utii ni baba wa yote. Kama ukiwa na nyongeza au swali unakaribishwa kupitia sehemu ya ku-comment hapo chini, au hata kwa mitandao mingine ya kijamii utakakokuta link ya mada hii. Neema ya Mungu Baba, na upendo wa Yesu Kristu na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nasi sote, sasa na hata milele. Tumsifu Yesu Kristu

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela

Phone: 0763 639 101/ 0679 639 101
Asante kwa kusoma katika blog hii.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

Monday 11 September 2017

KUWA MAKINI NA WATU HAWA. NI HATARI

Masikio yako yachuje kila unaloambiwa kabla ya kuchukua hatua.

Leo ni siku ya kutafakari baadhi ya aina ya watu ambao tunatakiwa kuwa nao makini sana hasa wale wenye nafasi ya kuweza kubadilisha mawazo yako. Kuna kundi la watu huenda wapo kwako kama marafiki maalumu sana kama ambavyo kilatini wanaitwa familiaritas au confidential friendship kwa kingereza. Hawa ukiwashirikisha mipango yako, na ikatokea wakakupatia marekebisho au mapendekezo lazima kuna uwezekano wa zaidi ya 70% kuyakubali.

Sasa nikupe orodha ya baadhi ya watu ambao inabidi unatakiwa kujua hawafai kuwaamini na wanaweza kukupeleka porini na kukwamisha mipango yako:

01.  Mtu anayeona yeye ni bora kuliko wengine wote:
Hapa lazima tuwekane sawa tafadhari. Point hii hailengi kumfanya mtu ajione dhaifu, la hasha!. Hapa nalenga mtu ambaye katika mazungumzo yake yote hufanya marejeo ya udhaifu wa wengine ukilinganisha na uimara wake. Mfano ukiona mtu kwenye mazunumzo yake kauli kama ‘Usinifananishe mimi na fulani, mimi nina uwezo zaidi/ unapoteza muda kuwa na fulani, mimi ndio ninauwezo wa kukuhudumia/ umempendea nini yule? Ona mimi nina x,y,z ambazo yule hana uwezo wa kuwa nazo/ Mimi ni mzuri sana, siendani na wewe, au unaniona kama fulani, mimi ni msomi kuliko fulani, mimi nina akili kuliko fulani’ hazikosekani basi ujue mtu huyu kuna uwezekano mkubwa wa kukupoteza au kutokuwa na mchango chanya kwenye ushauri wake, na pia wengi ni waongo.

02.Mtu anayejihami bila sababu (Defensive people).
 Hii ni aina ya watu ambao wao huwa wanajitanguliza kuona wapo sahihi kabla hujaanza kuhoji utendaji wao. Kwa mfano ukiona mtu unamwambia; ‘hapo umekosea’ halafu yeye anajibu ; ‘unadhani nilifanya makusudi? Sasa unadhani kwa mazingira haya ningefanyeje? Hata ungekuwa wewe ungefanya hivihivi’. Mtu kama huyu kufanya marakebisho baada ya kukosea huwa ni mgumu sana. Unatakiwa kuwa naye makini sana, na kama ni mwanafamilia (mke/mume) itakuwa vyema ukimtambua kwenye kipengere hiki, vinginevyo unaweza kuwa unaumia moyo kila siku na wakati mwingine kukosa amani ndani ya moyo wako.

03.Mtu anayelazimisha wote kuamini njia yake ya mafanikio ndio pekee ya kufuata
Hapa ndio kwenye shida zaidi, na watoto wadogo ndio walio kwenye hatari kubwa sana ya kuambukizwa huu ugonjwa. Kwa mfano, wapo watu ambao wamefanikiwa nje ya mfumo wa taaluma, sio kwasababu waliamua tu kuelekea huko, bali kuna mazingira yaliwatoa kwenye taaluma na kujikuta wanafanikiwa kutumia vipaji binafsi au kusaidiwa na watu wa karibu walio na msingi bora kwa kifedha. Watu wa aina hii baadhi yao hujikuta wanawaweka njiapanda walio kwenye taaluma kwa kuwaambia kuwa wanapoteza muda huko na hawatafanikiwa, na afadhari wajiunge nao nje ya mfumo wa taaluma kitu ambacho ni hatari sana kwa maana sio kila mtu anaweza kufanya kila kitu katika mazingira yote. Wapo pia ambao kwasababu wamefanikiwa kwa njia ya taaluma, basi wanawavuruga vichwa wale wanaopambana nje ya taaluma na kujikuta hawaweki bidii huko waliko. Huu ni upotoshaji, acha kila mtu afuate njia ambayo Mungu amempangia, kikubwa iwe sahihi na yenye kukubalika. Watie moyo watu kule waliko, sio lazima wote uwalazimishe kufanya kama wewe, na mambo yakiwachachia huko, utaanza kuwacheka tena kwa kuwaambia wanazembea au hawakusikilizi vizuri.
Kazi kwako, utamsikiliza yupi na uache yupi
.
04. Mtu anayesifia uovu kama njia ya kawaida ya maisha.
Vijana wengi tupo kwenye huu mtego wa kushawishiana. Kwa mfano mtu anajisifia uhodari wake wa kuwa na mahusiano holela kwa siri, udanganyifu, wizi, matusi, kutoheshimu wazazi au walezi, unyanyasaji katika mahusiano au katika mazingira yoyote. Ukiona katika mazungumzo yake mtu haoni aibu kujisifia katika mambo haya huyo ni hatari katika mustakabali na ustawi wa jamii yoyote ile, na haaminiki kwa lolote kwa maana dhamiri yake imesheheni dumuzi na uso usio na huruma kwa wanaoteseka kwa matokeo ya maamuzi yake.

05. Mtu asiye na ratiba. 
Hora argentum’; ni msemo wa kilatini unaofanana na ule wa kiingereza ‘time is money’ ikiwa na maana muda ni pesa/mali. Mtu ambaye hana mpango mkakati wa kuhakikisha anafanya jambo fulani kwa muda fulani mambo yake kamwe hayawezi kwenda. Ukiona mtu yupo tayari kwenda mahali popote anapoambiwa aende kwa muda wowote huyo hana ratiba , hafahamu namna ya kufanya kwanza jambo la kwanza. Yaani kuna watu rafiki yake akimwambia waende mjini anakubali bila kuhoji anaenda kufanya nini na je lilikuwa kwenye ratiba yake? Wakiwa njiani akipigiwa simu na  rafiki yake mwingine kuwa waende porini anakubali, hehhh, jamani, yani ikifika jioni yuko hoi na hakuna hata moja la kujivunia alilofanya katika ratiba yake. Kiukweli mtu asiyejari muda mimi huwa hazipandi kabisa. Lazima tufahamu kuwa muda ni rasilimali ya kipekee ambayo ni kama haionekani (invisible resource) lakini ikipotea hairudi tena, hivyo mtu asiye na ratiba unatakiwa kuwa naye makini sana ili usije ungana naye kuelekea shimoni.

06. Mtu asiyetaka kurekebishwa/asiyefundishika.
 Hili ni kundi jingine ambalo unatakiwa kuwa nalo makini sana. Baadhi ya watu wakisikia maonyo, wao hukimbilia kusema ‘hili halinihusu’ , yani kila kitu kinachomgusa yeye anaona kina wahusu watu fulani na sio yeye. Na hata ukigundua ana udhaifu fulani na ukaanza kumuelekeza, anaona kama unamtuhumu na anaanza kukwepa na kuhakikisha hauendelei kuongea, hasa mambo yanayoonekana kuwa binafsi kama mahusiano, lakini ukweli ni kwamba siyo ya binafsi kwa maana madhara yake huenda hadi kwa jamii iayokuzunguka kwa namna moja ua nyingine hata kama sio moja kwa moja.


07. Mtu mwenye mafungamano na ushirikina.
Nikisema hivi mtu anadhani namzungumzia mshirikina wa moja kwa moja. Hapana, huko ni mbali sana, mimi nazungumzia mtu wa kawaida ambaye muda mwingi anawaza kulogwalogwa tu, story zake ni za wahirikina tu, anataka aishi kama jiwe, yaani hata akipata kakipele tu kutokana na baridi, basi anakosa usingizi na kusema kuna mtu amemloga. Anajichagulia mfumo wa uuguaji, yani anampangia Mungu kuwa anataka asiugue ghafla, maana ikitokea tu hivyo kwake yeye tuhuma zake ni kwa wachawi tu, anajisahau kuwa mwili ni kama maua ya miti, hata upepo ukipuliza, lazima utayumba kidogo. Watu wa aina hii mfumo wao wa kufanya maamuzi ni mbovu, kiufupi hata aina ya ushauri wanaotoa huwa sio wa kujiamini na wameweka rehani amani yao kwa mambo yanayofikirika ambayo hawana uhakika nayo. Epuka kuwarithisha watoto hofu ya aina hii kwa maana inawafanya hata wao kuwa washirikina indirectly. Kuna wakati hata madhehebu ya dini hunasa kwenye huu mtego kwa kwa kuwajaza hofu ya kuwaza mapichapicha yasiyo na mashiko kwa mfumo huu.


Kwa leo niishie na hizo tabia chache angalau tupate nafasi ya kutafakari. Kitu cha msingi ni kuwa makini sana unapokuwa karibu na watu wenye tabia hizo, na ikumbukwe wengi hujiona kama wapo sahihi na busara kubwa sana inahitajika wakati wa kuwaelekeza ili wabadilike au hata kupunguza madhara yake kwao binafsi au watu wanaowazunguka. Kama ukiwa na swali au maoni unakaribishwa hapo chini kwa sehemu ya comment. Tafakari njema!

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Phone: 0763 639 101/ 0679 639 101

Asante kwa kusoma blog yangu.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

Sunday 20 August 2017

SABABU KUU MBILI ZA KUPENDA

Busara inatakiwa sana kuelewa mantiki ya upendo kwa mtu

Suala la kupenda ni suala mtambuka ambalo wakati fulani watu hutumia nguvu nyingi kujitahidi kutetea mantiki yake na kujikuta wanaishia kuongea uongo au kuharibu uhalisia. Kwa kawaida mtu akiulizwa sababu za kumpenda mtu fulani, anaweza kutoa majibu haya au yenye mlengo huu:

  • Kwasababu nayeye ananipenda
  • Kwasababu ni mzuri (mrembo/ handsome)
  • Kwasababu amewahi kunisaidia nilipokuwa na shida
  • Kwasababu anaonekana atakuja kuwa baba/mama bora wa familia
  • Kwasababu ana akili sana darasani
  • Kwasababu anaonekana mpambanaji sana na anajituma
  • Kwasababu ana pesa nyingi sana, nikiwa naye siwezi pata shida
  • Kwasababu ni mpole na sio mlevi
  • Na mengine mengi


Sawa lakini yote hayo huenda ukawa ni ushawishi wa kupenda, lakini sio sababu ya kupenda. Kuna utofauti kati ya sababu ya kufanya kitu na ushawishi wa kufanya kitu. Sababu ni hamu na muwako wa ndani wa kufanya kitu, kumbe ushawishi ni kitu ambacho kinakufanya uamini kuwa utakuwa salama baada ya kufanya hicho kitu.
Mfano rahisi. Tamaa ni sababu ya kufanya ngono, lakini matumizi ya kondomu ni kishawishi cha kufanya ngono. Nadhani hapo umeelewa utofauti kati ya haya maneno mawili
Upendo ni lazima uwafaidie wote , na sio wa kibinafsi


Sasa sababu mbili kuu za kupenda ni hizi hapa:
  1. Ni hitaji la kila kiumbe hai
  2. Ni amri


KUPENDA KAMA HITAJI
Hili lipo wazi  kabisa, hakuna mtu asiyetaka kupendwa. Ndio hata mimi najisikia raha sana ninapogundua mtu fulani ananipenda. Kuanzia wazazi wangu, walezi wangu, wanafamilia, walimu na marafiki wa jinsia na kada zote. Kupendwa kunaleta msisimko wa aina yake na kukufanya uone uko ‘PROTECTED AND SECURED’  kwa sala za wanaokupenda na unaamini muda wowote ukiwashirikisha jambo wataitikia kwa muitikio chanya (positive response). Ni wazi mtu kama hakupendi hawezi kukuombea kwa Mungu mafanikio au hata afya njema. Fuaraha yake ni kuona unaishi kwa wasiwasi, mateso na maumivu au hata kutoweka kabisa. 

Hili halipo tu kwa binadamu, hata mifugo yako nyumbani, ikigundua unaipenda na kuihudumia, utaona kabisa inaonesha ishara ya kukufurahia na kila mara urudipo nyumbani lazima irukeruke miguuni pako. Najaribu kuwaza hata miti na maua ya nyumbani ambayo kila siku unayatunza, kuyamwagilia na kuyawekea mbolea, laiti yangekuwa na mdomo yangezungumza na kukubali (appreciate) upendo unaoonesha kwayo.
Ukifahamu hilo ndivyo inavyokuwa upande wa pili, kama unafurahia kupendwa basi na wewe kuwapenda wengine ni lazima, kwa maana wanahitaji hilo, na ni la kudumu.  Watu wanapata vidonda vya tumbo, presha na msongo wa mawazo na wengine afya zao kuzorota mara wakigundua hawapendwi au kutothaminika na watu walio karibuu nao. Ulishajiuliza siku mtu wako wa karibu akikutamkia ‘SIKUPENDI WEWE, YANI NATAMANI KAMA NISINGEIONA HIYO SURA YAKO’ utajisikiaje? Wakati fulani sio lazima mtu atamke, lakini mambo yake tu yanatoa picha kuwa hampendi mtu fulani.


Na wapo wengine wako katikati (neutral), yani yeye anajipenda yeye mwenyewe tu, mweee jamani, sasa si uende baharini huko utafute kisiwa ukae huko peke yako? Kama unaona hilo ni gumu, tafsiri yake ni kwamba tunahitajiana na kutegemeana. Unapotembea tu huko nje na kuona watu wamefurahi, hawana huzuni, hiyo ni dawa pia na fundisho kuwa huwezi kujifurahisha mwenyewe, ili mtu ucheke, lazima uchekeshwe na mtu mwingine, kama sio mko uso kwa uso basi hata kwa message tu mnazochati. Kwa lugha rahisi tujifunze kuwapenda watu pasi na kujali matabaka ya aina fulani

Angalizo: Kwakuwa kupendwa ni hitaji, wapo wanaotumia mgongo wa uhitaji huo na kupeleka kwa watu upendo nusu kilo,  mateso na maumivu kilo hamsini. Hiyo ni dhambi kwa maana mpokeaji alijiandaa kuwa aliyemuendea ni mtu mwema anayefahamu kuwa kupenda na kupendwa ni lazima kati ya mtu na mtu au jamii na jamii.
Ni rahisi kutamka neno NAKUPENDA, lakini ukweli tunao wenyewe mioyoni


KUPENDA KAMA AMRI
Upendo ni amri ya Mungu. Nimejaribu kufuatilia mawaidha ya dini zote, mathalani Wakristu na Waislamu, wote wameagizwa kupenda, na kwamba kama wasipowapenda binadamu wenzao basi na Mungu hatawapenda wao. Ahaaaaa, kumbe kama hujui kupenda basi huwezi kuambatana na baraka za Mungu. Upendo hauhitaji pesa au mazingira maalumu au kuwekewa mikakati kama bajeti ya kujenga reli ya standard gauge, la hasha! Ukitambua tu kuwa ni amri ya Mungu , basi ni kujifunza tu kuwa ni sehemu ya maisha yako.


Upendo unaozungumzwa hapa hauna masharti, vionjo tatanishi na vitenzi vichokozi vyenye mlengo wa kumuinua shetani. Kwani hujawahi kuona mtu anasema ‘nilimuua mume wangu ili niishi kwa amani na mtu NINAYEMPENDA’, Sasa huo ni upendo? Hapana, ni ushetani kwa maana huyu wasasa akibadilika kidogo tu na akaja anayejali zaidi, basi atamuua na huyu ili afurahie na huyo mwingine. Hivyo ndugu zangu ni bora tukafahamu jambo hili kinagaubaga ili tusichanganye mambo na kudhani kupenda ni hiari, hapana. KUPENDA NI LAZIMA, lakini KUHUSIANA NI HIARI YA MTU. Kumpenda mtu sio lazima muhusiane, au kuzoeana bila mipaka, hapana, tupendane, tushirikiane, lakini mipaka na heshima iwepo ili kulinda utu wa mtu, misingi ya kijinsia, utamaduni na uhuru wa kuamua juu ya msatakabali wa maisha ya baadaye ya mtu binafsi. Kama una swali, hoja au maoni, kuwa huru hapo chini eneo la comments. NAWAPENDA WOTE

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Phone: 0763 639 101/ 0679 639 101
Asante kwa kupitia na kusoma haya.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

Thursday 17 August 2017

ASIYETAMBUA NAFASI YA BIKRA MARIA KTK UKOMBOZI SIO MKRISTU!

Bikira Maria mama wa Mungu, Utuombee

Tumsifu Yesu Kristu/Bwana Yesu asifiwe/Shaloom.  Nakusalimu ndugu yangu katika Kristu Yesu mwana wa Mungu ambaye kupitia yeye tumekuwa wamoja kwa namna fulani. Naomba kukuondoa hofu kama utakuwa ni mmoja kati ya waliokwanzika na kichwa cha somo hili, kwa maana utakuwa umejikwaza mwenyewe kwa kujikataa au kuenda kinyume na ukweli. Kuwa mpole na usome taratibu maelezo yangu , na kama una hoja au kitu cha kupinga basi utatiririka hapo chini kwenye eneo la ku-comment, namimi bila hiyana nitakuja kukuweka sawa.

KWANI BIKIRA MARIA NI NANI?
Biblia takatifu imedadavua na kukakavua kinagaubaga juu ya mama Maria, fungua  kwa muda wako Injili ya Luka kuanzia sura ya kwanza aya ya 26 na kuendelea. Kwa kifupi Bikira Maria ni mwanamke safi, aliyeteuliwa na Mungu ili kupitisha nafsi yake ya pili (Yesu Mwokozi), yani kuwa mzazi wa Yesu Kristu Mungu kweli na mtu kweli. Alijazwa neema, kutunzwa na kulindwa ili abaki bila doa hata kumbeba mkombozi tumboni mwake. 

  Kama hiyo haitoshi, hakuishia kumzaa tu mtoto Yesu na kumuacha akapambane na hali yake, NOOOOOOO, aliendelea kumlinda, kumtunza (kumbuka pale walipokuwa wanamtafuta roho juujuu Luka 2:43-52), usisahau pale walipomkimbiza mtoto kwenda Misri  ili asiuawe na Herode (Mathayo 2:12-21) mara anaambiwa maneno ya kumchoma moyo juu ya huyu mtoto (Luka 2:35) bado akaendelea naye hata katika safari ya mateso hadi msalabani (Yohana 19:26-27)

Mafundisho makuu manne (DOGMA) kuhusu Mama Maria
  1. Maria Mama wa Mungu
  2. Maria Bikira Daima
  3. Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
  4. Maria Mpalizwa Mbinguni


Leo sitaki kuanza kuyachambua hayo mnne kwa maana kila moja tu laweza kuwa mada ya kujaza kurasa nyingi. Angalau moja tu, kama huamini kuwa Bikira Maria makazi yake ni Mbinguni , nenda kasome Ufunuo sura ya 12 kuanzia aya ya kwanza na kuendelea na uje na jina la mwanamke anayezungumzwa hapo.

Wapo baadhi ya watu bila aibu mbele za Mungu wanasema kwao Maria sio kitu, wao wanamuangalia Kristu pekee kwa maana hakukuwa na ulazima wa Mungu kumtumia Maria na angeweza kumtumia hata mwanamke yoyote. Hivyo Maria alishamaliza kazi yake na hana umhimu wowote kwao. Hii ni kufuru mbele za Mungu ambaye ndiye aliyemtakatifuza huyu mama ili awe chombo kitakatifu kilichombeba mkombozi. Tatizo ni mafundisho yaliyokaa kimfumo wa kuoteshwa na vionjo vyenye ukakasi na kuwarithisha watoto uvuguvugu kisa tu hutaki kutafakari.

Maswali machache ya kujiuliza
  1. Kama unaamini kuwa Yesu Kristu ni Mungu kweli, nafsi ya pili ya Mungu Baba aliyeshikamana pamoja na Roho Mtakatifu bila kutengana, mbona unapata kigugumizi kusema Maria ni Mama wa Mungu (Yesu)?
  2. Kama Maria alishamaliza kazi yake ya kumzaa Yesu,na sasa hana umhimu wowote, basi na Yesu alishamaliza kazi yake na sasa hana umhimu wowote?
  3. Kama hakukukuwa na upekee wa Maria na Mungu angeweza kumtumia mwanamke yoyote, kumbe pia hapakuwa na ulazima wa Mungu kumtumia Yesu kutukomboa na angemtumia mtu yoyote?


Najaribu kuwaza kwa sauti hasa ninapoona wengi wakifanya mrejeo kwa wateule wengi wa zamani katika Biblia kama Musa, Elia, Daudi na wengine, lakini likija suala la Bikira Maria mhhhh, hapo wanaona mapichapicha. Wengi ukiwadodosa wanajing’atang’ata tu na kuishia kusema yeye anaangalia wokovu tu ulioletwa na Yesu, hataki kujua kuwa huyu Yesu hadi kutujia kuna watu ambao Mungu aliamua kushirikiana nao kujimwilisha (incarnation) ili tumuone na kumpokea katika umbo la kibinadamu. Kazi ya Bikira Maria ilitabiriwa tangu agano la kale huko Isaya  7:14 na kuelezewa matokeo yake katika agano jipya.

Angalau siku hizi kuna baadhi ya watu wa madhehebu yasiyo ya Kikatoliki wameanza kustuka na kujua kuwa walikuwa wanafanya makosa kutomheshimu mama wa Mkombozi wao hivyo kwa mbaliiiii wameanza kumtaja taja na kumheshimu, japo kwasababu ya kukosa msaada wa mafundisho au kuogopa wachungaji wao, basi wanashindwa kupata mang’amuzi ya hali ya juu na kujizolea neema kutokana na maombezi ya Mama huyu kwa mwanaye Yesu. Wapo ambao taratibu wameanza kusali Sala ya Salamu Maria na hata Rozali japo wanakuwa waoga kutokana na upande waliopo kutopigia chapuo sala hizi zenye nguvu ya kimungu ndani yake. Yeye mwenyewe kasema 'vizazi vyote tutamuita mbarikiwa' (Luka 1:48), sasa asijejua hili ni kizazi cha sayari gani?
Bikira Maria, Mama wa Amani, Utuombee


KUABUDU Vs KUHESHIMU.
Anayepaswa kuabudiwa ni mmoja tu (Kumbukumbu la Torati 5:7), naye ni Mungu muumba mbingu na nchi. Kuna watu pia wanapata ukakasi na kuwalishaa watoto wao matango poli kwa kusema wakatoliki wanamuabudu Bikira Maria, la hasha! Sio kweli, wao wanamuheshimu tu, tena heshima hiyo hatujakurupuka tu kumpa, bali ni Mungu kwanza ndiye aliyemuheshimu na kumkinga na doa la aina yoyote ili afanyike chombo cha kubeba nafsi yake kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Sasa jamani kama Mungu mwenyewe kamheshimu na kumpandisha hivi, sisi ni akina nani hata tumdharau? Ndio maana nimesema mtu asiyetambua nafasi ya Bikira Maria katika kuletwa kwa ukombozi huyo sio Mkristo bali anaigiza kuwa Mkristo.  

Bikira Maria ameshatokea mara kadhaa duniani hapa na ushahidi wa wazi kabisa upo. Maeneo kama Fatima, Lurdi Ufaransa, Kibeho Rwanda n.k yanatoa fundisho kwa dunia juu ya kumheshimu huyu mama. Hakuna mtu aliyewahi kupinga matokeo haya kwa maana ni matokeo ya wazi kabisa ambapo ni Mungu yule yule aliyemteua awe mama wa mwokozi anathibitisha kuwa uteule wake u hai hata leo huko mbinguni na duniani.
Bikira Maria ,kikao cha hekima, Utuombee

Kama unavyopata ujasiri wa kumwambia binadamu mwenzako akuombee kwa Mungu, sasa nakushauri utumie nafasi hii adimu kumwambia Mama Bikira Maria ambaye yuko Mbinguni uso kwa uso na Mungu akuombee kwa Mungu na mwanaye Yesu Kristu naye atafanya hivyo. Wewe omba kwa imani na matokeo utayaona.

TUOMBE:

Ee Mungu mwema, Baba wa Mataifa yote, kwa wema wako uliamua kumteua Mama Bikira Maria awe mama wa Mkombozi wetu Yesu Kristu, tunakuomba uturehemu na kutusamehe pale tunapokengeuka na kudharau heshima hiyo kubwa uliyompa mama huyu. Tena tunaomba msamaha na kwa mwanaye Yesu Kristu ambaye kabla ya kushuka duniani alikuwa kashikamana nawe kama nafsi yako, hivyo alishiriki kumteua mama Bikira Maria ili atusamehe na kutustahilisha baraka zako. Tena tunaomba msamaha na kwa Roho Mtakatifu ambaye mara kadhaa tumejigamba kujazwa naye kumbe ni vionjo vya kibinadamu na viini macho, na ndani mwetu tumejaa maasi hata kumdharau mama wa mkombozi. Nawe Maria Mtakatifu mama wa Mungu, utuombee kwa Mungu ili sala zetu ambazo mara kadhaa zinakwamishwa na maovu yetu ziweze kupokelewa, nasi kwa unyenyekevu tunaahidi kukuheshimu na kuthamini kazi yako ya kushirikiana na Mungu kutuletea Yesu, Bwana na Mwokozi wetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristu, anayeishi na kutawala  pamoja na Baba, Mungu daima na milele. Amina

Eng Herman Nguki.M
Email: ngukiherman@ymail.com
Phone: 0763 639 101/0679 639 101
Instagram : @eng.ngukiwamalekela
Asante kwa kusoma katika blog yangu.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com


Thursday 27 July 2017

NO FORGIVENESS, NO LOVE

Someone who cannot forgive, by default cannot love.

I find myself recalling the law of magnetism in physics subject during my time in secondary school even in my engineering courses. If the piece of magnet cannot attract the opposite side (unlike poles) of the other magnet (S&N), automatically it cannot repel the similar side (like poles) of the other magnet (S&S/ N&N). You know what? Someone who cannot forgive, by default cannot love.  I have purposely started with forgiveness because it is simple to say ‘I will love you in any situation’ but not ‘I will forgive you for any mistake’

My dear brothers and sisters, it’s better we understand this day time truth; in forgiveness there is love and in love there is forgiveness. They work together with similar properties but different names just like improper subsets. In simple logic, someone who can find it difficult to forgive, yet he/she says that he/she can love you, automatically it’s not true.

In love there if fear of God; that’s avoiding to cause pains to someone else, and when happens accidentally, by default it will be very easy to ask for forgiveness. Love and forgiveness cannot be separated. “We are told that people stay in love because of chemistry, or because they remain intrigued with each other, because of many kindnesses, because of luck. But part of it has got to be forgiveness and gratefulness. ” ― Ellen Goodman

Carol Davis (counsellor) says; Real love is total commitment with no separate parts or degrees and filled with harmony and joy. Hopefully, that feeling is reciprocated by someone.  Love cannot be taught. It is a natural expression coming from the heart or emotional makeup of the individual.   It is a gateway to connection with another human being, and if a person is a Christian, to God.
Forgiveness is a part of love. If a person is unforgiving, this is a block to love. The ultimate test of love is forgiveness. 

 When someone that a person loves hurts him, the response is the true record of that love; if there is true love here, the person will not hold a grudge (a strong feeling of anger and dislike for a person who you feel has treated you badly, which often lasts for a long time ) become resentful, or fill the heart with bitterness.  None of these responses connect with true love.  It blocks that emotion.  So what should the response be: to forgive.
The Oxford English Dictionary defines forgiveness as to grant free pardon and to give up all claim on account of an offense or debt. True forgiveness is doing the complete opposite of what the emotions tell a person to do.  'I will forgive you if…….' is not forgiveness.
Forgiveness to be real must be unconditional. It does not mean that the hurt that has been experienced is minimized.  Forgiveness cannot be earned, bought, or bargained.  It has to be absolute.

There are two hurtful situations that occur between people who love each other: a wound and a wrong. The wound does not require forgiveness.  It was unintentional and accidental.  Time and patience will take care of this situation.
The other situation though is a different story.  A wrong is when a person knows that what he is doing will hurt the other person and does it anyway. It is a moral dilemma that the person faces and fails. To wrong someone that a person loves requires forgiveness. Forgiveness is instant; but trust must be built over a long period of time. Forgiveness takes care of the damage done. It lets the person off the hook.  However, the true test of love will be how the person works to rebuild that loving relationship. 

Forgiveness may be the single most difficult act of love. It is the difference between forgetting and letting go. The brain never lets the person forget, but the heart will give forgiveness. Love and forgiveness walk hand in hand in a relationship.
If we really want to love we must learn how to forgive’-Mother Teresa

It’s where now Michael Ugulini (Educator) adds; Forgiveness is a manifestation of love. People who truly love each other, whether in a marital relationship, as friends, or as family members, as examples, will forgive one another because of their outgoing concern for each other. Forgiveness is one way of expressing love and commitment to another human being. Even though we may be upset, hurt, wronged, and/or angry, love provides us the capacity for forgiveness.

When we love someone, even though it may be difficult sometimes, we ultimately desire to forgive them for any perceived wrongs against us. If we do not ultimately wish to forgive someone we say we love, then we're fooling ourselves, and them, as we do not truly love them.
Not extending forgiveness is putting ourselves first, well ahead of the person we claim to love. We are seeking our own desires and are not taking into account theirs. We are acting selfish and are not willing to give them the benefit of the doubt - or another chance. If we love them, we will forgive them and try to set the relationship back on the right track.

Words like ‘I hate him/her, I will never forgive him/her’ are poisons which is going to kill yourself because they will lead to love malnutrition.  It is better you train your mind and soul to forgive, because it will automatically be a fertilizer to sustain your love to others. “Resentment is like drinking poison and then hoping it will kill your enemies.” ― Nelson Mandela


NOTE: To forgive someone doesn’t need him/her (who hurt you) to repeat explaining what he has done to you. The strong soul forgives even before being asked to do so.If we really want to love we must learn how to forgive’-Mother Teresa

Eng Herman Nguki.M
Email: ngukiherman@ymail.com
Phone #: +255 763/ 679 -639 101
Instagram : eng.ngukiwamalekela
Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com (Also subscribe to YouTube Channels- 'Eng Herman Nguki' and 'WaterDropletTv' )