Thursday, 17 August 2017

ASIYETAMBUA NAFASI YA BIKRA MARIA KTK UKOMBOZI SIO MKRISTU!

Bikira Maria mama wa Mungu, Utuombee

Tumsifu Yesu Kristu/Bwana Yesu asifiwe/Shaloom.  Nakusalimu ndugu yangu katika Kristu Yesu mwana wa Mungu ambaye kupitia yeye tumekuwa wamoja kwa namna fulani. Naomba kukuondoa hofu kama utakuwa ni mmoja kati ya waliokwanzika na kichwa cha somo hili, kwa maana utakuwa umejikwaza mwenyewe kwa kujikataa au kuenda kinyume na ukweli. Kuwa mpole na usome taratibu maelezo yangu , na kama una hoja au kitu cha kupinga basi utatiririka hapo chini kwenye eneo la ku-comment, namimi bila hiyana nitakuja kukuweka sawa.

KWANI BIKIRA MARIA NI NANI?
Biblia takatifu imedadavua na kukakavua kinagaubaga juu ya mama Maria, fungua  kwa muda wako Injili ya Luka kuanzia sura ya kwanza aya ya 26 na kuendelea. Kwa kifupi Bikira Maria ni mwanamke safi, aliyeteuliwa na Mungu ili kupitisha nafsi yake ya pili (Yesu Mwokozi), yani kuwa mzazi wa Yesu Kristu Mungu kweli na mtu kweli. Alijazwa neema, kutunzwa na kulindwa ili abaki bila doa hata kumbeba mkombozi tumboni mwake. 

  Kama hiyo haitoshi, hakuishia kumzaa tu mtoto Yesu na kumuacha akapambane na hali yake, NOOOOOOO, aliendelea kumlinda, kumtunza (kumbuka pale walipokuwa wanamtafuta roho juujuu Luka 2:43-52), usisahau pale walipomkimbiza mtoto kwenda Misri  ili asiuawe na Herode (Mathayo 2:12-21) mara anaambiwa maneno ya kumchoma moyo juu ya huyu mtoto (Luka 2:35) bado akaendelea naye hata katika safari ya mateso hadi msalabani (Yohana 19:26-27)

Mafundisho makuu manne (DOGMA) kuhusu Mama Maria
  1. Maria Mama wa Mungu
  2. Maria Bikira Daima
  3. Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
  4. Maria Mpalizwa Mbinguni


Leo sitaki kuanza kuyachambua hayo mnne kwa maana kila moja tu laweza kuwa mada ya kujaza kurasa nyingi. Angalau moja tu, kama huamini kuwa Bikira Maria makazi yake ni Mbinguni , nenda kasome Ufunuo sura ya 12 kuanzia aya ya kwanza na kuendelea na uje na jina la mwanamke anayezungumzwa hapo.

Wapo baadhi ya watu bila aibu mbele za Mungu wanasema kwao Maria sio kitu, wao wanamuangalia Kristu pekee kwa maana hakukuwa na ulazima wa Mungu kumtumia Maria na angeweza kumtumia hata mwanamke yoyote. Hivyo Maria alishamaliza kazi yake na hana umhimu wowote kwao. Hii ni kufuru mbele za Mungu ambaye ndiye aliyemtakatifuza huyu mama ili awe chombo kitakatifu kilichombeba mkombozi. Tatizo ni mafundisho yaliyokaa kimfumo wa kuoteshwa na vionjo vyenye ukakasi na kuwarithisha watoto uvuguvugu kisa tu hutaki kutafakari.

Maswali machache ya kujiuliza
  1. Kama unaamini kuwa Yesu Kristu ni Mungu kweli, nafsi ya pili ya Mungu Baba aliyeshikamana pamoja na Roho Mtakatifu bila kutengana, mbona unapata kigugumizi kusema Maria ni Mama wa Mungu (Yesu)?
  2. Kama Maria alishamaliza kazi yake ya kumzaa Yesu,na sasa hana umhimu wowote, basi na Yesu alishamaliza kazi yake na sasa hana umhimu wowote?
  3. Kama hakukukuwa na upekee wa Maria na Mungu angeweza kumtumia mwanamke yoyote, kumbe pia hapakuwa na ulazima wa Mungu kumtumia Yesu kutukomboa na angemtumia mtu yoyote?


Najaribu kuwaza kwa sauti hasa ninapoona wengi wakifanya mrejeo kwa wateule wengi wa zamani katika Biblia kama Musa, Elia, Daudi na wengine, lakini likija suala la Bikira Maria mhhhh, hapo wanaona mapichapicha. Wengi ukiwadodosa wanajing’atang’ata tu na kuishia kusema yeye anaangalia wokovu tu ulioletwa na Yesu, hataki kujua kuwa huyu Yesu hadi kutujia kuna watu ambao Mungu aliamua kushirikiana nao kujimwilisha (incarnation) ili tumuone na kumpokea katika umbo la kibinadamu. Kazi ya Bikira Maria ilitabiriwa tangu agano la kale huko Isaya  7:14 na kuelezewa matokeo yake katika agano jipya.

Angalau siku hizi kuna baadhi ya watu wa madhehebu yasiyo ya Kikatoliki wameanza kustuka na kujua kuwa walikuwa wanafanya makosa kutomheshimu mama wa Mkombozi wao hivyo kwa mbaliiiii wameanza kumtaja taja na kumheshimu, japo kwasababu ya kukosa msaada wa mafundisho au kuogopa wachungaji wao, basi wanashindwa kupata mang’amuzi ya hali ya juu na kujizolea neema kutokana na maombezi ya Mama huyu kwa mwanaye Yesu. Wapo ambao taratibu wameanza kusali Sala ya Salamu Maria na hata Rozali japo wanakuwa waoga kutokana na upande waliopo kutopigia chapuo sala hizi zenye nguvu ya kimungu ndani yake. Yeye mwenyewe kasema 'vizazi vyote tutamuita mbarikiwa' (Luka 1:48), sasa asijejua hili ni kizazi cha sayari gani?
Bikira Maria, Mama wa Amani, Utuombee


KUABUDU Vs KUHESHIMU.
Anayepaswa kuabudiwa ni mmoja tu (Kumbukumbu la Torati 5:7), naye ni Mungu muumba mbingu na nchi. Kuna watu pia wanapata ukakasi na kuwalishaa watoto wao matango poli kwa kusema wakatoliki wanamuabudu Bikira Maria, la hasha! Sio kweli, wao wanamuheshimu tu, tena heshima hiyo hatujakurupuka tu kumpa, bali ni Mungu kwanza ndiye aliyemuheshimu na kumkinga na doa la aina yoyote ili afanyike chombo cha kubeba nafsi yake kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Sasa jamani kama Mungu mwenyewe kamheshimu na kumpandisha hivi, sisi ni akina nani hata tumdharau? Ndio maana nimesema mtu asiyetambua nafasi ya Bikira Maria katika kuletwa kwa ukombozi huyo sio Mkristo bali anaigiza kuwa Mkristo.  

Bikira Maria ameshatokea mara kadhaa duniani hapa na ushahidi wa wazi kabisa upo. Maeneo kama Fatima, Lurdi Ufaransa, Kibeho Rwanda n.k yanatoa fundisho kwa dunia juu ya kumheshimu huyu mama. Hakuna mtu aliyewahi kupinga matokeo haya kwa maana ni matokeo ya wazi kabisa ambapo ni Mungu yule yule aliyemteua awe mama wa mwokozi anathibitisha kuwa uteule wake u hai hata leo huko mbinguni na duniani.
Bikira Maria ,kikao cha hekima, Utuombee

Kama unavyopata ujasiri wa kumwambia binadamu mwenzako akuombee kwa Mungu, sasa nakushauri utumie nafasi hii adimu kumwambia Mama Bikira Maria ambaye yuko Mbinguni uso kwa uso na Mungu akuombee kwa Mungu na mwanaye Yesu Kristu naye atafanya hivyo. Wewe omba kwa imani na matokeo utayaona.

TUOMBE:

Ee Mungu mwema, Baba wa Mataifa yote, kwa wema wako uliamua kumteua Mama Bikira Maria awe mama wa Mkombozi wetu Yesu Kristu, tunakuomba uturehemu na kutusamehe pale tunapokengeuka na kudharau heshima hiyo kubwa uliyompa mama huyu. Tena tunaomba msamaha na kwa mwanaye Yesu Kristu ambaye kabla ya kushuka duniani alikuwa kashikamana nawe kama nafsi yako, hivyo alishiriki kumteua mama Bikira Maria ili atusamehe na kutustahilisha baraka zako. Tena tunaomba msamaha na kwa Roho Mtakatifu ambaye mara kadhaa tumejigamba kujazwa naye kumbe ni vionjo vya kibinadamu na viini macho, na ndani mwetu tumejaa maasi hata kumdharau mama wa mkombozi. Nawe Maria Mtakatifu mama wa Mungu, utuombee kwa Mungu ili sala zetu ambazo mara kadhaa zinakwamishwa na maovu yetu ziweze kupokelewa, nasi kwa unyenyekevu tunaahidi kukuheshimu na kuthamini kazi yako ya kushirikiana na Mungu kutuletea Yesu, Bwana na Mwokozi wetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristu, anayeishi na kutawala  pamoja na Baba, Mungu daima na milele. Amina

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Asante kwa kusoma katika blog yangu.Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com


Thursday, 27 July 2017

NO FORGIVENESS, NO LOVE

Someone who cannot forgive, by default cannot love.

I find myself recalling the law of magnetism in physics subject during my time in secondary school even in my engineering courses. If the piece of magnet cannot attract the opposite side (unlike poles) of the other magnet (S&N), automatically it cannot repel the similar side (like poles) of the other magnet (S&S/ N&N). You know what? Someone who cannot forgive, by default cannot love.  I have purposely started with forgiveness because it is simple to say ‘I will love you in any situation’ but not ‘I will forgive you for any mistake’

My dear brothers and sisters, it’s better we understand this day time truth; in forgiveness there is love and in love there is forgiveness. They work together with similar properties but different names just like improper subsets. In simple logic, someone who can find it difficult to forgive, yet he/she says that he/she can love you, automatically it’s not true.

In love there if fear of God; that’s avoiding to cause pains to someone else, and when happens accidentally, by default it will be very easy to ask for forgiveness. Love and forgiveness cannot be separated. “We are told that people stay in love because of chemistry, or because they remain intrigued with each other, because of many kindnesses, because of luck. But part of it has got to be forgiveness and gratefulness. ” ― Ellen Goodman

Carol Davis (counsellor) says; Real love is total commitment with no separate parts or degrees and filled with harmony and joy. Hopefully, that feeling is reciprocated by someone.  Love cannot be taught. It is a natural expression coming from the heart or emotional makeup of the individual.   It is a gateway to connection with another human being, and if a person is a Christian, to God.
Forgiveness is a part of love. If a person is unforgiving, this is a block to love. The ultimate test of love is forgiveness. 

 When someone that a person loves hurts him, the response is the true record of that love; if there is true love here, the person will not hold a grudge (a strong feeling of anger and dislike for a person who you feel has treated you badly, which often lasts for a long time ) become resentful, or fill the heart with bitterness.  None of these responses connect with true love.  It blocks that emotion.  So what should the response be: to forgive.
The Oxford English Dictionary defines forgiveness as to grant free pardon and to give up all claim on account of an offense or debt. True forgiveness is doing the complete opposite of what the emotions tell a person to do.  'I will forgive you if…….' is not forgiveness.
Forgiveness to be real must be unconditional. It does not mean that the hurt that has been experienced is minimized.  Forgiveness cannot be earned, bought, or bargained.  It has to be absolute.

There are two hurtful situations that occur between people who love each other: a wound and a wrong. The wound does not require forgiveness.  It was unintentional and accidental.  Time and patience will take care of this situation.
The other situation though is a different story.  A wrong is when a person knows that what he is doing will hurt the other person and does it anyway. It is a moral dilemma that the person faces and fails. To wrong someone that a person loves requires forgiveness. Forgiveness is instant; but trust must be built over a long period of time. Forgiveness takes care of the damage done. It lets the person off the hook.  However, the true test of love will be how the person works to rebuild that loving relationship. 

Forgiveness may be the single most difficult act of love. It is the difference between forgetting and letting go. The brain never lets the person forget, but the heart will give forgiveness. Love and forgiveness walk hand in hand in a relationship.
If we really want to love we must learn how to forgive’-Mother Teresa

It’s where now Michael Ugulini (Educator) adds; Forgiveness is a manifestation of love. People who truly love each other, whether in a marital relationship, as friends, or as family members, as examples, will forgive one another because of their outgoing concern for each other. Forgiveness is one way of expressing love and commitment to another human being. Even though we may be upset, hurt, wronged, and/or angry, love provides us the capacity for forgiveness.

When we love someone, even though it may be difficult sometimes, we ultimately desire to forgive them for any perceived wrongs against us. If we do not ultimately wish to forgive someone we say we love, then we're fooling ourselves, and them, as we do not truly love them.
Not extending forgiveness is putting ourselves first, well ahead of the person we claim to love. We are seeking our own desires and are not taking into account theirs. We are acting selfish and are not willing to give them the benefit of the doubt - or another chance. If we love them, we will forgive them and try to set the relationship back on the right track.

Words like ‘I hate him/her, I will never forgive him/her’ are poisons which is going to kill yourself because they will lead to love malnutrition.  It is better you train your mind and soul to forgive, because it will automatically be a fertilizer to sustain your love to others. “Resentment is like drinking poison and then hoping it will kill your enemies.” ― Nelson Mandela


NOTE: To forgive someone doesn’t need him/her (who hurt you) to repeat explaining what he has done to you. The strong soul forgives even before being asked to do so.If we really want to love we must learn how to forgive’-Mother Teresa

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com (Also subscribe to YouTube Channels- 'Eng Herman Nguki' and 'WaterDropletTv' )

Wednesday, 5 July 2017

MBABE WA MBABE WANGU ALIPONIZUSHIA UONGO

Tuwafundishe watoto kusamehe, lakini tusiwape hofu.

Katika maisha ya ukuaji kuna vitu sio rahisi sana kuvisahau hata kama havina tija sana. Moja ya vitu ambayo nilikuwa naogopa sana ni kupigana. Sasa kuna jamaa mmoja wakati niko shule ya msingi alikuwa hakai mbali sana na nyumbani alifanikiwa kufahamu kuwa nina huo woga. Na kwa sababu hata familia yao ilikuwa juu kimaisha alikuwa na ujasiri wa ziada, na kama hiyo haitoshi alikuwa kanizidi madarasa kama matatu hivi (tulikuwa tunasoma shule moja ya msingi huko Idodi-Kitanewa) na umri kanizidi.

Lakini hivi vyote sio kisingizio kwa maana mbinu za kupigana zipo nyingi tu hata kama mtu kakuzidi nguvu, kwani kwenye Biblia Daudi alifanyeje kumpiga Goliath? Ndivyo ilivyo  ndugu yangu. Sasa huyu jamaa alikuwa akijisikia tu ananipiga, dah, ukizingatia hali yetu ya maisha ya nyumbani, nikawa najiona dhaifu sana kumfanya chochote huyu jamaa, tena mimi nilikuwa naishi na bibi yangu tu nyumbani.

Basi kila nikipigwa na yule jamaa, nikawa naenda kusema kwa bibi ili aliruhusu namimi nimgoliatishe huyu jamaa ambaye alitumia udhaifu wangu kunigeuza mimi ngoma yake ya mazoezi. Ajabu bibi alikuwa ananizuia na anaishia tu kusema ‘wewe muache tu , nitaenda kuwaambia wazazi wake wamuonye asirudie hiyo tabia’. Nikawa nayaelewa yale maneno, japo huyu jamaa aliendelea na tabia yake ya kunipiga akijisikia hasa mkienda kucheza mpira maeneo ya wazi au tukienda mtoni huko kuogelea kipindi cha maji mengi na kuchoma viazi ( vimbwegea).

Mnyonge ukibahatika kupokonyoka hapo, ni kutimua mbio hadi mafichoni huko.
Kiukweli pamoja na kwamba huyu jamaa alikuwa amenizidi mabavu kwa mfumo fulani, lakini laiti bibi angeniruhusu tu nijitutumue nitakavyoweza, hakika ningetafuta cha kufanya kama alivyofanya mwenzangu Daudi wa kwenye Biblia, hata kutumia mawe tu au manati (Kwa maana nilikuwa nayo na kokoto za kutosha muda wote). Ile hali ilikuwa inanichefua sana na kujikuta wakati fulani nawaka hasira na kuona kama bibi pia anaiogopa ile familia kwa maana mama yake mdogo yule jamaa ndio alikuwa balozi wa  mtaa. Dah, lakini kulikuwa na fundisho kubwa sana kwa bibi kunizuia kumrudi yule jamaa, maana alikuwa ananiambia sentensi moja tu ya kihehe; ‘umtesa neke twangule nongwa’, akimaanisha utamuumiza  na mwisho wa siku tutazua kesi.

Yule mbabe wangu alikuwa na kaka yake, ambaye kiukweli alikuwa mpole sana, japo alionekana na nguvu sana lakini hakuwa mgomvi kabisaa. Na wakati fulani betri zikigeukiana kwa huyu mbabe wangu, yule kaka yake alikuwa anananisaidia angalau nipate upenyo wa kufanya mazoezi ya kukimbia hadi nyumbani. Aisee, usiombe kuishi maisha ya unyonge na kujiona huwezi kufanya kitu. Kama ni mtoto ni afadhari sana uwe na akili za darasani, angalau unakuwa na watu wa kukuogopa kwenye kipengere hicho, hasa wale ambao ikitolewa kazi wanakuja uwashushie vitu, wenyewe wanasema ‘unawasovia’ hata kama hakuna hesabu humo. Hawa watakutetea siku ukibanwa na waonezi wako, na wakati mwingine unawashitakia ili wakawapige mkwala waonezi wako.

ZAMU YA MBABE KUKUMBANA NA DHAHAMA

Siku moja ilikuwa sikukuu, kama sijasahau sana ilikuwa kati ya Pasaka au Krismasi. Sasa pale kwao wakaweka mziki na watoto tukawa tunaserebuka pale. Nilikuwa nacheza kwa tahadhari sana maana nipo nyumbani kwa mbabe wangu, na likitokea la kutokea yule jamaa atakuja tu hata kunikanyaga kama kifaranga, wahehe tunaita kiswiya.
Ilikuwa siku ya kufurahi sana kucheza mziki,lakini kuna jamaa alikuwa ananinyima amani.
Wakati mambo yanaendelea ikatokea ugomvi kati ya yule mbabe wangu na kaka yake. Weee nikajivuta pembeni kabisa mnyonge mimi. Katika purukushani yule mkubwa akamtwanga kichwa cha mdomoni yule mbabe wangu na kufanikiwa kumng’oa jino la mbele, kisha nayeye kuumia kwenye paji la uso kwa kuchimbwa na jino. Dah, kwakuwa yule mbabe wangu ana asili ya ukorofi, watu waliokuwepo walimuacha pembeni hapo akilia na kuugulia maumivu, kisha wakachemsha maji haraka na kuanza kumkanda-kanda huyu kaka mtu aliyeumia paji la uso.

Kwakweli nilikuwa namuonea huruma pia yule kaka mtu, na sikumuonea huruma kabisa yule mbabe wangu ambaye alijipatia mwanya wa lazima siku ile baada ya kung’oka jino kwa kupigwa kichwa na kaka yake. Ni kwasababu niliwaza kuwa huenda huku kuumia kutampa kipindi cha mpito cha kuugulia maumivu hivyo kutopata muda wa kuninyanyasa au kukwaruzana naye. Maisha yaliendelea ambapo baada  ya muda fulani kupita yule jamaa aliendelea tu na ukorofi wake na bado bibi aliendelea kunisisitiza nimsamehe tu na kuna wakati kweli bibi alikwenda kuwaambia wazazi wake juu ya tabia ya kijana wao ya kuninyanyasa, ambapo wazazi wake walimkemea na kumuonya aache hiyo tabia. Yule kaka yake nilimuamini sana na kuona ni mtetezi wangu.


MBABE WA MBABE WANGU AKAJA KUZUA YAKE

Maisha yaliendelea na walimaliza shule wale ndugu wawili kwakuwa walikuwa darasa moja, kisha yule mkubwa kufanikiwa kujiunga na sekondari.
Tarehe 15/06/2005 ilikuwa siku ya gulio (mnada) kule kijijini kwetu. Hiyo siku nilikuwa na hela yangu elfu kumi (10,000/=). Ilikuwa ni pesa yangu kabisa kutokana na kazi fulani niliyofanya, ambapo nilitumia elfu moja kununua kitu fulani na ikabaki eflu tisa. Sasa katika uhifadhi wa ile elfu tisa na utoto kuchangia, ile hela iliyobaki waliniibia yote. Nililia sana, kwa maana ile hela ilikuwa kubwa sana kwangu. Basi nikawasimulia baadhi ya rafiki zangu juu ya ule mkasa nilioupata. Sasa yule kaka wa mbabe wangu ambaye nilikuwa namuamini sana nayeye alipata hizi habari kuwa nimeibiwa hela elfu tisa.

Katika hali ya kustaajabu na isiyo ya kawaida huyu jamaa niliyemuamini sana baada ya kupata zile taarifa alikwenda kwa wazazi wangu na kuongea uongo wa kiwango cha lami na unaofanana na uuaji kabisa. Alisema, nanukuu: ‘Herman alikuwa na hela leo na amechezea kamali za mnadani. Mimi nilikuwa naye wakati anaenda kucheza. Nilimkatalia sana kuwa hao watakutapeli hao, yeye akawa mbishi, nikamvuta mkono tuondoke pale, lakini yeye aling’aang’ania kucheza hadi hela ikaisha. Nyie subirieni tu atakuja huku analia hapa’

Duh, aisee, ukweli ni kwamba ile siku hatukuonana kabisa yule jamaa hata ile kawaida tu kusalimiana, lakini alikwenda kuupika uongo huo ambao kiukweli, dah inauma sana. Muda ukawadia wa mimi kurudi nyumbani, kama alivyosema yule jamaa, nilirudi navuja chozi na hela sina. Mama alikaa kimya ili anisikilize kwanza nini kimenikuta huko. Nikamuelekeza kuwa nimeibiwa na sijuwi nini kimetokea, mama akanipa pole, lakini akasema ‘mbona fulani kasema umecheza kamali na alikuzuia lakini wewe ukawa mbishi?’ Mh, jamani, mbona mimi hata sijaonana naye leo? Akanieleza maelezo yote aliyosema yule jamaa, kuna kitu kilinikaba shingoni kwa hasira kwa maana nilijikuta najiuliza, :

  • Alikuwa analenga nini kuongea uongo huu kwa wazazi wangu?
  • Je hii hela ingekuwa sio yangu na nimetumwa na wazazi kununua kitu fulani kwaajili ya familia angeniweka katika mazingira gani?
  • Je hii hela ingekuwa ya mtu hata asiye ndugu yangu labda aliniagiza nikamnunulie kitu fulani huko gulioni na akapelekewa uongo huu uliosukwa kwa ustadi mkubwa, angejisikiaje?

 
Nilijiuliza mengi bila kupata majibu
Nafsi yangu ilichafuka sana ghafla na nilijikuta kwa mara ya kwanza namchukia sana kwa maana alifanya jambo ambalo sikutegemea. Hasira zilinizidi na kujikuta nalia sana na wakati huo mama alinituliza na kuniambia nimsamehe tu, na nijifunze kuelewa kuwa wapo watu wa aina hiyo na nimapungufu yao, japo mtu unayewasikiliza kama ukichukua mamuzi ya haraka, unaweza kusababisha madhara makubwa kwa taarifa za uongo na badaye kujikuta unajutia maisha yako yote. Nikajikuta hata msaada wake kipindi ambacho nilikuwa naonewa na mdogo wake nausahau kabisa, kwa maana kafanya jambo la kuogofya kwa mdomo wake.

Sijawahi kumuuliza hata siku moja, na tangu ile siku tumeonana kama mara mbili au tatu pekee hasa baada ya yeye kuwa shule ya bweni na mimi kuhamia Iringa mjini  mwezi wa nane 2005,na kuanza sekondari 2006. Tangu kipindi hicho nilikaa kwa muda na baadaye kuwasamehe wote wawili japo kipindi cha nyuma bado kuna roho ilikuwa inanituma nimtafute ili aniambie nini kilimtuma kuupika uongo ule. Wote kwa sasa wanaishi maeneo tofauti tofauti na familia zao.

HITIMISHO

Ndugu zangu, hakuna mtu mkamilifu hapa duniani, sote ni dhaifu. Kitu cha msingi ni kutouendekeza huo udhaifu wako (kilema cha dhambi) ambao unaweza kuwa na madhara makubwa sana kwako binafsi, familia au watu wanaokuzunguka. Mfano ni mimi mtu niliyemuamini kupita kiasi akaja kudhihirisha udhaifu wake kwa namna tofauti, lakini hii haiondoi ukweli kuwa kuna mambo mazuri aliyofanya ikiwemo kunitetea kipindi cha nyuma. Hata yule mbabe wangu, lazima tu kuna eneo fulani anafanya vizuri hata kama mimi sikuona binafsi, huenda ni kwa mwingine. Kitu cha msingi ni kusaidiana, kurekebishana, na wewe unayeonywa kubali kubadilika kwa maana hujuwi lini utakutna na lipi. EPUKA UONGO NA UGOMVI KWA MAANA UNAWEZA KUSABABISHA KIFO CHA MWILI AU NAFSI KATIKA MAZINGIRA MADOGO SANA.

Naitwa Nguki, sijawahi kumpiga mtu zaidi ya mimi kupigwa mara kadhaa wakati niko shule ya msingi. Baada ya hapo (kuanzia sekodari) kwakweli ni mkwara tu wa maneno umenisaidia kuepuka mapigano , kutotilia maanane maneno chonganishi yenye uchochezi wa kupigana pia kuomba msamaha hata kama sijakosa mimi ili yaishe na kuepusha mapigano. Kiufupi sipendi hata kuona tu watu wanapigana na sina huo mpango kwakweli.

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

Wednesday, 28 June 2017

MWANAUME, KUMUOMBA MSAMAHA MWANAMKE NI HESHIMA.

Mwanaume anayejitambua haoni shida kuomba msamaha

Salamu. Leo nataka nizungmze na wanaume wenzangu. Hivi karibuni niliandika tafakari fupi juu ya mapishi na wanawake. Japo sikuweka huku kwenye blog, kule kule kwenye facebook, instagram na watsup kila mtu alitoa mtazamo wake, hasa watsup uliibuka mjadala mkali kwenye baadhi ya makundi ambako nilishirikisha. Na kiukweli lengo langu halikuwa kumaanisha kuwa mapishi ni ndoa, bali ndoa ni composite function ambayo ndani yake kuna vitu vingi sana, na lengo ni kuweka vitu vingine vyote sawa (keeping other factors constant /CETERIS PERIBUS) na kuangalia athali za mke ambaye hapendi au ni mvivu kupika.

Wakati wa kuchangia mada hiyo, wapo waliosema mbona umewazungumzia wasichana pekee? Nikaahidi kuja na ugonjwa unaowasumbua wanaume wengi kama compensation, kwa maana lengo ni kujenga na sio kushushua au kuhukumu. Sasa nizungumze juu ya suala la wanaume kuona ugumu kuomba msamaha kwa wanawake pale wanapowakosea. Ni ukweli usiopingika wanaume wengi hudhani wao kuomba msamaha kwa wanawake ni kujishushia hadhi au kuonesha udhaifu. Wengi hujitutumua na kuishia kusema ‘POTEZEA TU, au VUNGA, au YAISHE au KAUSHA’. Sasa sijui nini kinakaushwa hapa, ni mishikaki au chipsi? Sijuwi mimi.

Kwa haraka mtu anaweza kudhani hii ni kwenye ndoa tu, lakini hata kwa vijana ambao hawajaoa, inaweza kutokea mkakwaruzana au kukwazana na msichana yoyote mnayesoma naye au rafiki wa kawaida ambapo wanaume wengi hupata ukakasi kutamka neno ‘nisamehe dada yangu, nisamehe rafiki yangu’. Huu ni ujinga, na ujasiri wa hasara kwa maana haijaandikwa kuwa wanawake tu ndio watakuwa wanakosea. Ni vyema wanaume kujifunza kuomba msamaha pale unapomkosea mwanamke yoyote ili isikupe shida hata ukiingia kwenye ndoa na kufanya kosa fulani kwa mkeo, kisha kuanza kuona ukakasi kuomba msamaha. Ukiulizwa kitu ambacho unajua kabisa umefanya kosa, unaanza kujitutumua kuonesha hasira na kutengeneza mazingira kuwa kwa wanaume ni kawaida kufanya hicho kitu, hapana, hiyo sio kweli.
Kuomba msamaha hakukupunguzii kitu. Kwani hujuwi kuwa umekosa ?

Kwa mwanaume kuomba msamaha kwa mwanamke hakupunguzi uanaume wako wala kukudisqualify kutoka kwenye nafasi uliyopo, bali ni tendo la kijasiri na ukomavu kifikra , kimtazamo na maamuzi. Ile amani anayopata mwanamke baada ya kuombwa msamaha ni baraka kwako. Halafu masikini ya Mungu wanawake hata hawaoni kazi kusamehe, hasa ukionesha kweli umeelewa kosa. Mara nyingi kwasababu ya kujiona dhaifu hujikuta wanasamehe hata bila kuombwa msamaha, sawa hili ni zuri sana kuwa nalo hata kwa wanaume, lakini wakiombwa msamaha  inakuwa jema zaidi.

Hata huko kwenye ndoa mara nyingi baadhi ya dada zetu walioingia huko wanatushirikisha, utasikia ‘Weee baba fulani hata akirudi usiku usijaribu kuuliza, atakuwashia moto hadi ujikute wewe ndio unaomba msamaha kwa kumuuliza, amesema wanaume huwa hawaulizwi’, mhhh, hii sio sifa njema, sasa kama mnajiita nyie ni mwili mmoja, halafu unasema usiulizwe, basi na wewe usimuulize kitu. Ni kweli mwanaume ni kichwa cha nyumba na hilo ni agizo la Mungu mwenyewe, sawa lakini ukimkosea mkeo au mwanamke yoyote ufahamu kuna ubinadamu, na nafsi yake inafukuta na kujikuta anawaza  mambo mengi ya ajabuajabu ambayo angekufanyia kama angekuwa na huo uwezo.

Ushauri wangu kwa wanaume wote tujifunze kuomba msamaha kwa jinsia zote, na sio kwa mwanaume mwenzako tu kisa umeona ana minguvu kuliko wewe kwamba akiamua anaweza kukugeuzia betri na umeme ukashindwa kuwaka? Mhhh, hapana. Kama ambavyo inakukereketa mtu aliyekukosea asipoomba msamaha, ndivyo ilivyo kwa wanawake ukiwakosea na ukatia mgomo kuomba msamaha eti unaogopa kujishushia heshima, nani kakudanganya? Wewe omba tu msamaha kwa unyenyekevu wote, utajiongezea heshima kwake na kujitofautisha na wengine wanaochukulia kila kitu generally bila kuwa na unique behaviours.
Mwingine akijipapatua weee anaamua kuandika kaujumbe kamsamaha na kuweka mezani. Teh,teh, sawa ni jambo jema, lakini jifunze kutamka kwa kinywa chako then suppliment na hayo maandishi mazuri.

Kwa upande wangu sioni shida kuomba msamaha endapo nitagundua nimemmkosea mtu wa jinsia yoyote kwa maana hainipunguzii kitu chochote zaidi ya kuniongezea tu reputability na kutowaza kuwa hivi ananifikiriaje nilipofanya kosa au kumkwaza bila kuomba msamaha. Wafundisheni watoto wakiume kujua umhimu wa kuomba msamaha kwa vinywa vyao kwa jinsia zote pale wanapofanya makosa kama ilivyo kwa watoto wa kike. Hapo tutakuwa tunajenga jamii inayojielewa na kuifanya jamii kukalika na kuwa na mapatano pasi na kuwa na ubabe na unyanyasaji kwa watu fulani. Mtu anayeomba msamaha akikosa yupo kwenye nafasi nzuri ya kushirikishwa mambo mengi mazuri kwa maana anazungukwa na watu wasio na kinyongo. Usiombe mwanamke akuchukie kisawasawa kisa ulimkwaza na kugoma kuomba msamaha weeee, huwa wanachefuka hao balaa tupu. Tuwapunguzie mizigo ya kuwaza mengi, tuwaombe msamaha kila tuwakoseapo. OMBA MSAMAHA KILA UKIFANYA KOSA BILA KUJALI NI KUBWA AU DOGO. Tafakari njema.

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com

Thursday, 1 June 2017

USHIRIKINA-BAADHI YA WAKRISTO WANAUSUJUDIA

Chagua moja, usichanganye, usipotoshe. Mungu hana mshindani.

Ukiulizwa ushirikina ni nini labda utakuwa na tafsiri (definition) yako. Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi naweza kusema USHIRIKINA ni imani anayokuwa mtu kwa nguvu za giza ambayo huchagizwa kwa mafungamano na mizimu, wapiga ramli, tabiri chonganishi, uchawi, mazindiko na vyote vyenye undugu na hayo.

Naomba tuwekane sawa hapa, neno IMANI ZA KISHIRIKINA haliwahusu tu wanaofanya pekee, bali hata wanaosadiki, kutetemekea na kuyahusudu hayo ndio maana kuna neno IMANI. Kwa bahati mbaya baadhi ya Wakristu wanachanganya kati ya ushirikina na kutumia mitishamba kujitibu. Wapo wakristu wengi ambao wanajitokeza kifua mbele kusema Mungu anakataza kutumia miti, mbogamboga na matunda kujitibu kama havijatengenezwa katika maabara na kutolewa hospitali.

Hili ni tatizo kubwa la uelewa ambalo limewafanya baadhi ya watu hasa vijana kuwa limbukeni kwa kuaminishwa vitu vya kijinga kwa mgongo wa kuijua Biblia. Ni kweli Biblia imeutaja sana uchawi na ushirikina na imesem wazi kuwa vitu hivyo havina nguvu tena kwa wale wamuaminio Kristo.

Dawa zote tunazotumia malighafi zake ni miti, mbegu nakadharika, hivyo nitakubaliana na mtu anayepinga matumizi ya dawa za asili kwa sababu moja tu nayo ni uhakika wa vipimo kutokana na umri wa mgonjwa na ukubwa wa athari. Yaani zile 2x3, au 1x 4 ambazo huwa tunaziona zinaandikwa kwenye dawa za hospitali ni ngumu kuzifuata kwa dawa ya asili hivyo kuna uwezekano mkubwa waa kuzidisha kipimo (over dose), pia changamoto ya uhifadhi (storage) LAKINI SIO KWAMBA KUZITUMIA NI USHIRIKINA.
Dawa zote tunazotumia ni mazao ya miti, mbegu, matunda na mboga mboga. Tusiwadanganye watu kuwa kutumia miti kujitibu ni dhambi.

JE UCHAWI UPO?
Ndio, uchawi upo na ni dhambi, tena haujaanza leo, upo tangu enzi za agano la kale na ulishapigwa marufuku na Mungu. Tutazame mifano hii michache

Kwani kuasi ni kama dhambi ya UCHAWI, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.( 1 Samuel 15:23)

Lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kitimilifu, UCHAWI wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno.( Isaiah 47:9)

Nami nitakatilia mbali UCHAWI, usiwe mkononi mwako; wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana.( Micah 5:12)

Wala nuru ya taa haitamulika ndani yako tena kabisa; wala sauti ya bwana-arusi na bibi-arusi haitasikiwa ndani yako tena kabisa; maana hao wafanya biashara wako walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa UCHAWI wako.(Ufunuo 18:23)
Bado kuna kundi kubwa la Wakristo ambao hawataki kuachana na imani za kishirina moja kwa moja. Anamuamini Mungu bado kwa kujifichaficha anaamini juu ya nguzu za ushirikina na kutafuta njia za kujikinga nje ya Mungu


Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, UCHAWI, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.(Galatia 5:19-21)

Mungu ametuuumba tutawale  wanyama na mimea na tuvitumie vitufae. Kwa taarifa yako afya ndio mtaji mkubwa kuliko chochote. Kutumia miti, mbegu matunda mbogamboga kwaajili ya kujitubu sio dhambi. Kama hutaki kukubali hilo basi hata ukienda hospitali na daktari akikuambia ‘uwe unakula angalau machungwa mawili kwa siku maana yaasaidia moja, mbili tatu’ usikikubali kwa maana nao pia utakuwa ushirikina, unataka hadi chungwa waligeuze kiwe kidonge kinachoitwa chungwaolokwini ndio utakubali.

Jambo la ajabu kwa sasa ni hofu iliyotawala kwa wakristu kwa kuogopa habari za kufikirika kuhusu ushirikina na kupandikiza mbegu za hofu kwa watoto na kujikuta wakiabudu watu badala ya Mungu. Ni kawaida sana siku hizi kusikia Mkristu ambaye anaumwa kidogo tu na Malaria au magonjwa yakimazingira au kutokana na uzembe wake kufanya mazoezi au kuishi mazingira machafu, lakini utamsikia nimerogwa, ni majini haya, oohhh ni wachawi hawa washindwe kwa jina la Yesu. Heh, jamani mbona ni kituko hiki.

 Kuna waraka fulani nilisoma mtu fulani amewaandikia waumini wa dhehebu lake kuwa ‘Kwenda hospitali au kutumia dawa za asili vyote ni dhambi kwa maana Mungu anaponya na kwenda hospitali au kutumia dawa ni kuona kama Mungu hawezi’. Sasa huyu ana utofauti gani na wapiga lamli? Kwa maana imani yake imekaa kimazingaombwe na upotoshaji, kama wale waliowahi kusema wanataka kwenda Iraq bila viza wala paspoti, Mungu atafanya muujiza wa kuwatoa uwanja wa ndege hadi huko waende wakahubiri.

Ni kweli Mungu anaponya, lakini daktari anatibu na ndio maana tunasali kwaajili ya madaktari wetu na wauguzi wawe na moyo wa huruma na kutoa huduma safi kwa wagojwa, tena tunamuomba Mungu azibariki dawa ili ziwafae wagonjwa wetu kwa maana hata kama dawa ni sahihi, Mungu akiamua kuchuka uhai wake hakuna njia ya kuzuia hilo.

ANGALIZO: Kama mtu atakuambia haya majani ya mti ni dawa ya kidonda, ukisagasaga na kupaka unapona, lakini uende ukasagie na jiwe lililookotwa njia panda ya kwenda makaburini, au wakati wa kupaka kiuno kiwe kimeelekea linakozamia jua,, ooohhh uwe hujasalimiana na mtu yoyote, sijuwi nini na nini,,,,,,,,,, hapana huo ni ushirikina na uchawi kwa maana kuna mafungamano na nguvu za giza na sayansi pori ambayo imejificha na haielezeki vizuri.

Lakini mtu anakuambia pale nje kwenu kuna muarobaini au mlonge na unatibu kitu fulani, nenda kachume majani au mbegu, changanya na kitunguu swaumu kidogo na tangawizi na asali kwa mbali halafu unywe bila masharti yoyote, hivi hapa ushirikina uko wapi???. Tuko busy kuwadidimiza watu kimtazamo na kuwavuruga uwezo wao wa kufikiria kisa tuataka kuwakusanya na kuwafanya mtaji. Huo ni ushetani, tusiitumie Biblia kupotosha watu. Najua hofu ya watu wengi ni kwamba ‘Kama napewa dawa na mtu fulani, je najua ameinenea maneno gani huko wakati wa kuichimba au kuichuma?’ . Sawa hiyo ni tafakari nzuri, basi kama hiyo ndio ishu tumia zile ambazo unajichimbia au kujichumia mwenyewe au mtu unayemuamini.

 Lakini kwanza tukubaliane Mungu hawezi kumpa mtu kila kitu, hivyo hata utambuzi wa mti fulani unatibu kitu fulani hajampa kila mtu, hivyo ni uamuzi wa huyo mtu kuwaambia wengine au kuwachumia  yeye mwenyewe. Kama ambavyo leo unaamini (huenda ni kinyume kwako) kwamba ukisaga tangawizi ukachanganya na asali inatibu kifua, hasa kwa watoto, ujue ilianza kwa mtu mmoja kutambua naye akawaambia wengine. Nikukumbushe tu, Warumi 14:14 inasema Najua, tena nimehakikishwa sana katika Bwana Yesu, ya kuwa hakuna kitu kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake huyo kitu kile ni najisi.’ Hivyo ukiamini  pia ukisema nikila chungwa nitatoka vipele, vitakutoka kweli kwa maana ndipo imani yako ilipolala.
Matibabu ya hospitali ni ya muhimu, sio ya kubeza hata kidogo. Ukisema unamuamini Mungu hivyo hata ukiumwa huendi hospitali kisa Mungu atafanya, basi unajitakia kufa, na utakufa ndio kwa ujinga wako huku unamsingizia Mungu


*******************************************************************************************

Katika kusoma kitabu kinachoitwa ‘Busara za Mzee’ kilichoandikwa na Padre Titus Amigu  amesema haya kwenye baadhi ya maeneo ya kitabu chake;,

Hofu za kishirikina zinatukwamisha waafrika wengi weusi kupiga hatua za maendeleo ya kweli. Kuna wengine tunaamini sana katika ushirikina. Wengi tunataabika kutafuta nguvu na uwezo wa kufanya maajabu huku wengine wakitafuta kinga dhidi ya ushirikina, wengine tunaogopa laana, nasi tunataabika usiku kutaka kuivunja ile tunayoiita miti ya familia. Wengine tunaogopa mizimu hivyo kujitaabishaa kuitambikia ili kuituliza mizimu isije kutudhuru kwenye shughuli zetu za kila siku.

Jiamini kama mwana wa Mungu. Ondoa wasiwasi kwani wasiwasi ni chimbuko la magonjwa ya kisaikomatiki. Mungu amekuumba kwa hiari yake mwenyewe naa ndipo Mungu mwenyewe anakulinda mwili na roho. Ukijiamini katika ulinzi wa Mungu unaaweza hata ukanywa sumu nayo isikudhuru.

Usilimbukie habari za majini, usije ukakubali usanii. Uwe mbishi ukatafute uthibitisho wa ukweli wa vituko vya ajabu unavyosimuliwa.

Usichanganywe. Usikubali elimu yako izimwe hasa elimu ya afya na elimu ya viumbe. Kuna matukio mengi unaweza kuyachambua kisayansi ukaona ukweli au uongo wake. Elimu ya Baiolojia inaweza kukuelewesha mengi na ukapunguza kustaajabu kusiko na sababu ama kudai kupungwa mapepo hata pasipo takiwa.
*******************************************************************************************
Wakristo tupone jamani na haya maigizo ya watu kutuchezea akili na kujikuta nasisi tunawafundisha watoto uongo na ujinga. Makanisani siku hizi kumekuwa na kazi mbili tu, kuwapa watu utajiri na kuwapa habari za vitisho vya ushirikina. Hebu tuangalie maisha ya Yesu kwani alifanya mangapi? Suala la kuutafuta uzima wa milele siku hizi kwa baadhi ya makanisa halizungumzwi tena, wao ni kupokea miujiza ya majumba na magari, kuolewa na kuzaa basi. Sijasema kwamba watu wateseke, hapana, lakini kuna mahala fulani tunachezewa akili.

Unafahamu kuwa kuna magonjwa ya zinaa kama Kisonono mgonjwa asipotibiwa mapema huweza kuathiri hadi ubongo na mfumo wa fahamu kasha kumfanya mtu awe kichaa? Bado mtu uko busy kudanganya watu kuwa eti umeongea na Mungu kakwambia huyu mtu kalogwa na watu wanaomuonea wivu kwasababu ana akili sana na darasani huko chuoni? Kuna utaofauti gani kati yaw ewe unayeongea haya na mpiga ramli msituni huko? Huyu Mungu tunayemchezea hakika ni mvumilivu sana, maana tumefanya machukizo  mengi kwa mgongo wa neno lake huku lengo likiwa kujistawisha sisi na familia zetu kwa kuwakandamiza wenye matatizo na mahanagaiko ya dunia hii.

Mungu akusaidie, na ubadili  mtazamo wa kufikilia, acha kuwaza kulogwalogwa tu kila saa, matatizo mengine unayachikonoa wewe mwenyewe, tena ukumbuke wewe sio chuma au jiwe, chuma chenyewe hupata kutu, sembuse na wewe ambaye Biblia imesema kabisa kuwa unafanana na maua a mti? Jamani, tusijitafutie shari kwa Mungu wetu ambaye sifa yake ya kwanza ni huruma na kutukirimia neema zake ili tuweze kuwa salama na kuitakatifuza dunia hii na kuhudumiana kama wana wa Baba mmoja.
Tumsifu Yesu Kristo.

Eng Nguki Herman. M
Instagram: @eng.ngukiwamalekela
Twitter: @engngukiherman
Asante kwa kutembelea blog yangu..Unaweza kusoma mada mbalimbali kwa kuchagua mwaka/mwezi kwenye eneo la chini (footer block) ambapo baada ya kusoma bofya neno older post na zitakuja nyingine na uendelee kwa mfumo huo kupata mada za awali ambazo hukubahatika kuzisoma.Au kama hauoni hilo neno bofya kwanza 'view the web version' ndipo utakuja mfumo utakaokuonesha neno older post kwa chini. Kwa elimu na ujuzi kuhusu maji, kilimo, udongo na mazingira tembelea blog: www.wadcotanzania.blogspot.com