Tumsifu Yesu Kristu, leo hii natamani nikushirikishe kitu juu ya nguvu ya Novena. Bila shaka kwa Mkristo Mkatoliki neno hili novena sio geni, wala sihitaji kulidadavua kirefu. Kwa kifupi NOVENA NI SALA YENYE NGUVU ISIYOSHINDWA KAMWE KUTOA MAJIBU IWAPO UTASALI KWA IMANI. Zipo novena nyingi kama za Roho Mtakatifu, Pentekoste, za watakatifu kama Rita wa Kashia nakadharika. Kwa wanafunzi wa chuo novena ya Roho Mtakatifu najua lazima huwa inakumbukwa kipindi cha kukaribia mitihani. Ipo pia novena ya kushukuru baada ya kufungua chuo kwa kumshukuru Mungu kwa kurudi salama na matokeo ya kukuwezesha kuvuka mwaka, japo hii wengi huwa wanaipuuzia kwa kuwa hakuna wanachokiomba, walishapata tayari vyote.
Lakini kwa waliopo au waliotoka jumuiya ya TMCS SUA-New Hostels, tangu mwaka 2014 tulianza kusali Novena kwa Mt Rita wa Kashia ambayo huchukua siku 12, yaani kuanzia Jumatatu ya kwanza ya UE hadi Ijumaa ya mwisho ya UE kwenye vipindi vya sala za asubuhi. Yaani siku 9 za novena na 3 za shukurani, zote zipo ndani ya muongozo wa vitabu vya Mt Rita wa Kashia. Mara zote huanza na sakrament ya Kitubio. Novena ile kwa wenzangu ambao tumekuwa tukishiriki wote ni mashahidi, kila mtu kwa nafsi yake, Mungu amekuwa akijibu kwa upekee sana yale maombi takribani 15 kwenye muongozo wetu. Hakika Mungu atukuzwe.
AMENIJIBU TENA KWA MAOMBEZI YA MT RITA WA KASHIA
Kama binadamu mwenye malengo na mahitaji, niliazimia tena kujichotea baraka zilizopo bure kwa Mungu wetu kupitia maombezi ya mtakatifu huyu shujaa wa kujitoa sadaka ambapo tarehe 9/9/2016 nilianza novena kwa Mt Rita wa Kashia nikiwa na mahitaji 10 ambayo niliyaorodhesha kwenye karatasi yangu. Katika orodha yangu kulikuwa na shukurani na maombi. Yale maombi yalikuwepo yale ambayo majibu yake ni tangible (yani yakijibiwa nitajua moja kwa moja) na yalikuwepo ambayo ni intangible (siwezi kuthibitisha kwa macho kuwa kayajibu lakini kwa imani). Novena ile ilianza tar 9/9 Ijumaa na kwenda hadi 20/9/2016 na kukamilisha siku 12. Nilianza nikiwa Iringa nyumbani lakini tar 18/9/2016 Jumapili nilisafiri kwenda Mbeya kwaajili ya semina kwa wiki moja, hivyo niliimalizia nikiwa Mbeya.
Mungu anashughulika na mambo yetu usiku na mchana, wema wake watuzunguka pande zote |
MAAJABU.
- Baada ya kuanza novena tarehe 9/9/2016, kesho yake tarehe 10/9/2016 ombi la kwanza kuorodheshwa likatimilika vilevile nilivyoomba.
- Siku ya 7 ya novena yaani 15/9/2016 ,Ombi la pili kuorodheshwa kwenye karatasi yangu likatimia vilevile nilivyoomba na kuandika.
- Siku ya 10 ya novena tar 18/09/2016 Ombi la tatu kwenye orodha yangu lilitimia kwa mfumo uleule. Nilistaajabu mno, maana ombi hili niliwaambia hata baadhi ya marafiki zangu kuwa nimelifungia novena na lazima niibuke kidedea, likatimia vilevile.
- Baada ya novena kuisha, Mungu aliendelea kujibu orodha yangu ambapo yale tangible lilibaki moja ambalo ni la muda mrefu (long term goal) ambalo naamini Mungu ameshajibu lakini anasubiri tu siku nzuri ya kuniambia ili nipokee. Na yale ambayo siwezi kuona majibu kwa macho naamini Mungu ameshajibu yote kwa maombezi ya mama huyu Rita wa Kashia ambaye Kanisa katoliki kwa kusaidiana na shirika la Mtaktifu Agustino tunamuita MTAKATIFU WA MAMBO YALIYOSHINDIKANA NA MFANYA MIUJIZA MTEULE WA MUNGU.
- Watu wengi pia wameendelea kushuhudia mambo makubwa na yaajabu ambayo Mungu amejibu kupitia maombezi ya Mt Rita wa Kashia.
Hakika nakosa cha kusimulia zaidi, lakini jinsi Mungu alivyojibu tena kwa mtiririko uleule kama nilioandika kwenye karatasi yangu ya maombi, kweli niliamini Mungu yupo na anajibu waziwazi na tunajionea kwa macho.
LINI TUNASALI NOVENA KWA MT RITA WA KASHIA?
LINI TUNASALI NOVENA KWA MT RITA WA KASHIA?
- Kuanzia kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi. Siku ya 12 (ya mwisho) inadondokea Ijumaa ya wiki la pili la sala.
- MAALUMU KWA MWEZI WA MAY. Mt Rita wa Kashia alizaliwa Jumamosi ya 22/5/1377 na kufariki Jumamosi ya 22/5/1457. Hivyo kwa upekee wa mwezi huu wa tano NOVENA HUANZA SIKU 9 KABLA YA 22/5 AMBAYO NDIO SIKU YA KUMBUKUMBU YAKE (feast day), yaani tunaanza novena tarehe 14/5 ili siku ya 9 idondokee siku hiyo ya 22/5. Ukiongeza na siku tatu za shukurani (kwa mujibu wa muongozo) novena itakamilika tarehe 25/5. Tarehe hii 22/5 ni siku kubwa sana kukumbuka matendo makuu ya Mungu kupitia mteule wake huyu mkuu, ambapo kuanzia Kashia na dunia nzima misa mbalimbali hufanyika kwa heshima ya Mt Riata wa Kashia
- Waweza kusali wakati wowote unapokuwa na nia yoyote iwe shukurani, maombi ya kawaida, mfadhaiko mkubwa au changamoto nakadhalika. Usisahau pia kusali sala mbalimbali kupitia yeye. Jambo la msingi hakikisha unapata kitabu cha sala na novena.
Nisikilize ndugu yangu hapa chini |
USHAURI WA BURE
Mungu wetu ni tajiri, na vyote tunavyovitamani kwa haki ni vyakwake na sisi ni warithi wake (Rum 8:17, Gal 3:29, Tito 3:7) kwa maana hiyo tukiomba kwa imani anatustahilisha kuvimiliki si kwa sifa za duniani. bali kupokea kwa saburi, unyenyekevu na kuhudumia wengine. Wakati fulani Mungu anaweza asijibu maombi kwa wkati, lakini pengine anakuwa ameshafanya typing , anayo softcopy, hivyo yuko mbioni kuprint ili ukabidhiwe kwa maana anafahamu softcopy huna facility ya kuhifadhi. Sasa ukianza kulalamika na kuona kama Mungu hayupo utamtibua na kumfanya aahirishe kumtuma Malaika Gabiel kwenda stationary kuprint ujue. Tulia, kuwa mnyenyekevu, kuwa na subira, mchukie shetani na matendo yake, jitahidi kupenda kuhudumia kuliko kuhudumiwa. Pale unapopata ugumu, washirikishe watu unaowaamini wakusaidie, sio kila mtu wa kumshirikisha kila kitu. Kwa Kristo sisi ni washindi, kwa Kristo tuko salama. TUMSIFU YESU KRISTO: